Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
Mahakama ya Rufani Tanzania imetupilia mbali rufaa iliyofunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko ya kupinga dhamana zao.
Uamuzi huo umesomwa na Msajili wa Mahakama hiyo, Sylvester Kainda na kuiagiza mahakama kurudisha jalada la kesi hiyo Mahakama Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kuendelea na hatua ya usikilizwaji wa rufani iliyokatwa na Mbowe na Matiko baada ya kufutiwa dhamana zao na Mahakama ya Kisutu.
Katika kesi ya msingi, Mbowe na viongozi wengine wa Chadema wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018 jijini Dar es Salaam.
Viongozi wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu ambao wote walikuwepo mahakamani.