NAIROBI, Kenya
AGIZO la kuyazuia mabasi ya abiria kuingia katikati mwa mji mkuu Nairobi lilianza kutekelezwa rasmi jana asubuhi na kusababisha adha kubwa kwa wasafiri baada ya polisi na mgambo kumwagwa katika njia kuu.
Hali hiyo ilisababisha misululu mirefu ya abiria ambao walikuwa wakishushwa mbali na mji hususan barabara ya Thika wakitembea kwa miguu kuelekea maeneo mbalimbali ya mji huu.
Katika agizo hilo, waendesha mabasi hayo maarufu kama matatu, wameagizwa kuendesha shughuli zao katika maeneo ambayo yametengwa bila kuingia katikati ya mji kuchukua ama kususha abiria.
Maofisa wa jiji wanasema wamekwisha kutenga maeneo maalum yenye maegesho 505 yanayoweza kutumika kwa kazi hiyo.
Hata hivyo waendesha mabasi hayo ya abiria wanaomba kupewa muda zaidi kujiandaa huku wakitishia kutafuta msaada wa sheria kama mamlaka husika hazitasikiliza kilio chao na kusimamisha kwa muda agizo hilo.
Katika malalamiko yao, waendesha mabasi hao wanadai wanahofia hali inaweza kuwa mbaya mvua itakapoanza kunyesha ikizingatiwa maeneo waliyotengewa kutokuwa na vibanda vya kujikinga mvua.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mjini hapa, agizo hilo ni mpango wa serikali wa kujaribu kuzuia msongamano wa magari katikati ya jiji hili.
Taarifa hizo zilieleza kwamba jana, zaidi ya maofisa 300, walipewa jukumu hilo kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa.