31 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

MASTAA 10 WALIOTIKISA USAJILI MAJIRA YA JOTO

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO


HATIMAYE dirisha la usajili barani Ulaya lilifungwa mwishoni mwa wiki iliopita na kushuhudia baadhi ya klabu zikiwapoteza wachezaji wao katika dakika za mwisho.

Hata hivyo zipo klabu zilizofanikiwa kufunga usajili wao kwa kuzinafasa saini ya wachezaji nyota, ila wapo mastaa waliohusishwa kutaka kuondoka lakini hadi usajili unafungwa walijikuta wakisalia kwenye klabu zao.

Baadhi ya wachezaji ambao walikuwa wanahusishwa kutaka kuondoka na hatimaye wamebaki ni pamoja na nyota wa klabu ya Liverpool, Philippe Coutinho, Alexis Sanchez, Mesut Ozil wa Arsenal, Ivan Perisic wa Inter Milan, Riyard Mahrez wa Leicester City na wengine wengi, lakini klabu ambazo zilikuwa zinawania saini za wachezaji hao wanaweza kuendelea na nia hiyo katika usajili wa Januari mwakani.

SPOTIKIKI Jumatatu hii imekuandalia mastaa 10 waliosajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha katika kipindi hiki cha majira ya joto.

Neymar

Huyo ni mchezaji wa pekee ambaye ameweka historia mpya ya usajili duniani, nyota huyo alikuwa anakipiga katika kikosi cha Barcelona kwa jumla ya misimu minne, lakini hatimaye amejiunga na matajiri wa soka la Ufaransa.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 mwezi uliopita alikamilisha uhamisho wake kutoka Barcelona kujiunga na PSG kwa kitita cha pauni milioni 200, ambazo ni zaidi ya bilioni 573 za Kitanzania.

Hii haijawahi kutokea katika ulimwengu wa soka, hivyo ni mchezaji wa kwanza kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha duniani.

Ousmane Dembele

Baada ya klabu ya Barcelona kumuacha Neymar akiondoka katika kikosi chao, klabu hiyo ilihakikisha inapambana ili kumpata mchezaji ambaye ataziba nafasi hiyo.

Waliamini kuwa kiungo mshambuliaji wa Liverpool, Coutinho angeweza kufaa kuziba nafasi hiyo, lakini hawakufanikiwa kuipata saini yake, hatimaye wakaipata ya Dembele mwenye umri wa miaka 20 kutoka klabu ya Borussia Dortmund.

Mchezaji huyo ameweka historia ya aina yake ya kuwa mchezaji wa pili duniani kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha, amejiunga na Barcelona kwa kitita cha Euro milioni 102.6, ni zaidi ya bilioni 268.

Romelu Lukaku

Huyo ni mchezaji mpya wa klabu ya Manchester United akitokea Everton, amekuwa mchezaji wa tatu kwa kuhamishwa kwa fedha nyingi ikiwa uhamisho wake umetumia Euro milioni 82.7, zaidi ya bilioni 215.

Mchezaji huyo aligoma kuongeza mkataba ndani ya kikosi cha Everton katika kipindi hiki cha majira ya joto, hivyo kocha wa Man United, Jose Mourinho akaamua kumsajili kwa kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa kuwa alikuwa anahusishwa kutaka kujiunga na klabu yake ya zamani ya Chelsea.

Alvaro Morata

Baada ya Chelsea kuchukua ubingwa msimu uliopita, kocha wa klabu hiyo Antonio Conte aliamua kuongeza nguvu katika safu yake ya ushambuliaji kwa kumsajili mshambuliaji wa klabu ya Real Madrid, Morata.

Kocha huyo aliamua kutumia kiasi cha Euro milioni 60.6, ambazo ni zaidi ya bilioni 158 ili kukamilisha uhamisho wake, wawili hao waliwahi kufanya kazi pamoja wakiwa katika klabu ya Juventus.

Mchezaji huyo aliamua kuondoka ndani ya Real Madrid baada ya kukosa namba ya mara kwa mara chini ya kocha wake Zinedine Zidane, hivyo amekuwa mchezaji wa nne kwa kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha.

Benjamin Mendy

Kwa sasa ni nyota mpya wa klabu ya Manchester City akitokea klabu ya Monaco, mchezaji huyo amejiunga na klabu hiyo kwa uhamisho wa kitita cha Euro milioni 56.2 zikiwa ni zaidi ya bilioni 147.

Mchezaji huyo alikuwa anawindwa na klabu mbalimbali ikiwa pamoja na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Chelsea.

Alexandre Lacazette

Huyo ni nyota mpya wa klabu ya Arsenal, amejiunga na kikosi hicho akitokea Lyon, amekuwa mchezaji wa sita kusajiliwa kwa fedha nyingi katika kipindi hiki cha majira ya joto.

Mshambuliaji huyo amejiunga na Arsenal kwa uhamisho wa kitita cha Euro milioni 51.8 ni zaidi ya bilioni 134.

Kyle Walker

Baada ya kushindwa kutwaa taji la Ligi Kuu msimu uliopita kama watu walivyofikiria, kocha wa klabu ya Manchester City, Pep Guardiola ameamua kufanya makubwa katika usajili wa kipindi hiki cha kiangazi, ameweza kumsajili staa kutoka Tottenham, Walker kwa kitita cha Euro milioni 49.8 zikiwa ni zaidi ya bilioni 129.

Bernardo Silva

Nyota huyo alikuwa anakipiga katika klabu ya Monaco, lakini kocha wa klabu ya Manchester City, Pep Guardiola aliamua kutumia kiasi cha Euro milioni 48.8 ambazo ni zaidi ya bilioni 126 ili kumuongeza kikosini.

Gylfi Sigurdsson

Alikuwa nyota wa klabu ya Swansea City msimu uliopita, lakini kwa sasa ni mchezaji mpya wa klabu ya Everton, aliyejiunga kwa kitita cha Euro milioni 48.3 ni zaidi ya bilioni 126.

Nemanja Matic

Huyu ni mchezaji aliyeshika nafasi ya 10 kwa kusajiliwa fedha nyingi, alikuwa mchezaji wa Chelsea, lakini kocha wa Man United, Jose Mourinho aliamua kumsajili kwa kitita cha Euro milioni 43.7 ni zaidi ya bilioni 113.

Kutokana na hali hiyo jumla klabu za Ligi Kuu nchini England zimeonekana kutumia kiasi kikubwa cha usajili msimu huu ikiwa jumla ya pauni bilioni 1.4, wakati huo Ligi ya Italia ikitumia pauni bilioni 1.03, huku Ligi ya Ujerumani ikitumia pauni milioni 720.9, Ligi ya Ufaransa imetumia pauni milioni 931.3, Hispania ikitumia pauni bilioni 1.03.

Kwa upande wa England, klabu ya Man City imeongoza kwa kutumia fedha nyingi kwenye usajili, jumla ya pauni milioni 220 wakizitumia katika kipindi hiki cha majira ya joto, Chelsea Pauni milioni 192, Man United, pauni milioni 146, Everton pauni milioni 135.8, Tottenham pauni milioni 88, Liverpool pauni milioni 80,

Leicester pauni milioni 78.85, Watford pauni milionin 55.25, Arsenal pauni milioni 46.5, West Ham pauni milioni 44, Newcastle pauni milionin 36.2, Brighton pauni milioni 34.25, Huddersfield pauni milioni 43.5, Crystal Palace 34. Stoke City pauni milioni 25.7, West Brom pauni milioni 41.9, Burnley pauni milioni 41.5, Bournemounth pauni milioni 30 sawa na Southampton na Swansea City.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles