25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mama amchoma mtoto kwa kudokoa chakula

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia Eliza Denis (23) mkazi wa Makulu mkoani hapa kwa tuhuma za kumpiga sehemu mbalimbali za mwili na kumchoma moto mikononi mtoto wake wa kambo, Jackson Denis (5) kwa madai ya kudokoa chakula.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba Jeshi la Polisi linamshikilia mama huyo.

Kamanda Muroto alisema watu wamekuwa wakiendelea kujihusisha na matukio ya ukatili wa kijinsia, hususani kwa watoto hivyo Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

“Huko maeneo ya Dodoma Makulu amekamatwa mama mmoja ajulikanae kwa jina la Eliza Denis ambaye ni mkulima na mkazi wa Dodoma Makuli kwa makosa ya kumpiga sehemu mbalimbali za mwili na kumchoma mikononi mtoto wake wa kambo aitwae Jackson Denis mkazi wa Dodoma Makulu,” alisema Kamanda Muroto.

Alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu shtaka hilo siku za hivi karibuni.

MTOTO ASIMULIA

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili juzi, mtoto huyo alidai kuwa mama yake huyo wa kambo amekuwa akimpiga mara kwa mara pamoja na kumchoma sehemu za mikononi kwa sababu amekuwa akidokoa chakula.

Alidai kuwa mama huyo amekuwa akimnyima chakula hivyo kujikuta wakati wote ana njaa na hivyo kukimbilia kwa majirani ili aweze kula.

Jackson alisema amekuwa akiishi kwa tabu kutokana na kutokumuona baba yake ambaye anadai kwamba ameondoka na kwenda kusikojulikana.

“Huwa nanyimwa chakula hivyo nikidokoa kile ambacho kipo ananipiga, njaa huwa inanishika, hata nikienda kwa watu pia ananipiga,” alidai mtoto huyo.

MAJIRANI WAELEZEA

Wakielezea tukio hilo, majirani wa mtoto huyo wamedai kuwa amekuwa akinyimwa chakula na mama huyo ndiyo maana amekuwa akikimbilia kwao ili aweze kula.

Mmoja wa majirani hao, Semeni Juma, alisema mama huyo ana watoto watatu wa kuwazaa pamoja na Jackson ambaye ni mtoto wake wa kambo.

Alidai kuwa watoto wake hao watatu amekuwa akiwapa chakula, lakini Jackson anamnyima pamoja na kumpiga mara kwa mara.

“Amekuwa akipigwa sana na mara nyingi amekuwa akija kwetu na sisi tunampatia chakula, lakini hatukujua kama ana makovu kama haya,” alidai.

Jirani huyo alisema sababu ya kugundua majeraha aliyonayo katika mwili ni siku moja alikuja nyumbani kwake asubuhi huku akiwa amelowana na akitetemeka.

Alisema ilibidi wambadilishe nguo ili wamvalishe nyingine na hapo ndipo walipoona makovu mwilini, hivyo kumpeleka kwa mjumbe wa mtaa.

“Alikuwa na majeraha, hivyo nikashtuka kwani yanaonekana ni ya kuchapwa fimbo pamoja na mengine ya kuchomwa,” alisema.

Alisema pia mtoto huyo tumbo lake limejaa kutokana na kukosa chakula na anaonekana ana dalili za ugonjwa wa utapiamlo.

MJUMBE WA MTAA

Kwa upande wake, mjumbe wa mtaa huo, Nazalena Mdede ambaye ni maarufu kwa jina la Mama Kufakunoga, alisema alimpokea mtoto huyo akiwa dhaifu, hivyo walimpeleka hospitali kupatiwa matibabu.

“Ni kweli alionekana amedhoofu, tulimpa chakula chakula tukamhifadhi na kumpeleka hospitali,” alisema.

MAMA AFUNGUKA

Akizungumza juzi mara baada ya kukamatwa na polisi, Eliza alisema ni kama vile wanamwonea na kwamba taarifa hizo si za kweli.

“Mimi sijui kwani yeye kawaambia nini? Mnanizushia na taarifa hizo si za kweli,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles