27.4 C
Dar es Salaam
Thursday, December 9, 2021

Tunakemea wanaojichukulia sheria mkononi

MIONGONI mwa habari iliyopewa uzito hususani katika magazeti makubwa nchini matoleo ya jana, ni ile ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwahukumu kifungo cha maisha jela washtakiwa wanane baada ya kutiwa hatiani katika kesi ya kuchoma moto Kituo cha Polisi Bunju A.

Hakimu aliyesoma hukumu hiyo, Thomas Simba alisema kitendo hicho walichofanya washtakiwa hao ni cha kinyama na hawezi kuwaonea huruma kwa kuwa walihatarisha usalama wa nchi.

Alisema kabla ya kutoa hukumu hiyo, mahakama ilifika katika eneo la tukio na kuona kituo hicho kilichomwa moto hadi kuwa majivu na ndani yake kulikuwa na silaha, mahabusu na waliona damu zimeganda eneo la tukio.

Msingi wa hayo yote ni matakwa ya wananchi kuwekewa matuta barabarani baada ya ajali ya gari iliyoua mwanafunzi ambayo ilitokea eneo la Bunju A.

Hukumu hii ambayo imeonekana kushtua wengi imetoka katika wakati ambao ipo orodha ndefu ya wananchi kujichukulia sheria mkononi ikiwamo kuchoma moto vituo vya polisi.

Kimsingi siku zote sisi tumekuwa mstari wa mbele kukemea vurugu na zaidi watu wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi.

Pamoja na hayo, katika kuripoti kwetu matukio mbalimbali, hasa yale ya watu kujichukulia sheria mkononi, yakiwamo haya ya kuchoma moto vituo vya polisi, mara nyingi si mara zote tumebaini matatizo huwa yanakuwa yameanzia upande wa polisi.

Baadhi ya matukio yanayothibitisha hilo ni lile lililotokea Simiyu mwaka jana ambako wananchi walivamia kituo cha polisi na kufanya uharibifu mkubwa, msingi ukidaiwa ni tuhuma za askari kudaiwa kuhusika na kifo cha kijana mmoja waliyekuwa wakimshikilia.

Tukio jingine lenye sura ya watu kujichukulia sheria mkononi ni lile lililotokea miezi ya hivi karibuni la polisi mwenye namba E.1156 Koplo William Marwa kudaiwa kumuua ndugu wa Mbunge wa Tarime, John Heche aliyefahamika kwa jina la Suguta Marwa mwenye umri wa miaka 27.

Tumelazimika kutoa mifano hiyo michache ya matukio yenye sura ya watu kujichukulia sheria mkononi ili kuonesha kwamba jambo hili si zuri na halipaswi wakati mwingine kutazamwa juu juu bali kuangalia mzizi unaosababisha hayo.

Tunasema hivyo kwa sababu siku zote tumekuwa tukisisitiza kuwa unapoteuliwa kuwa kiongozi katika eneo lolote, liwe la Serikali ya mtaa, kituo cha polisi, shule, mtaani nakadhalika tunapaswa kutambua kuwa jukumu letu ni kuondoa matatizo na si kuyaongeza.

Wakati mwingine matatizo yanatokea kwa sababu tu watu fulani fulani na hasa wale waliopewa mamlaka kushindwa ama kuchukua hatua au kutumia busara.

Sisi hatudhani kama udhaifu wa sheria unaweza kuwa sababu inayoongoza kusababisha matukio hayo, bali udhaifu wa wasimamizi wa sheria kama polisi, mahakama na vyombo vingine, pamoja na jamii kwa ujumla wake.

Tukifika mahali hasa viongozi wakatambua wajibu wao kwa maana ya kutumia busara katika kutatua matatizo, kuchukua hatua haraka, kufuata sheria, kuheshimu utu wa wanaowaongoza, tunaamini tutapunguza matatizo mengi na hivyo kujikita zaidi katika shughuli za maendeleo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,659FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles