26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

MAKALA: Kwanini Rwanda?

NA MARKUS MPANGALA

VITA vya maneno baina ya utawala wa Kigali na ule wa Kampala vimekuwa vikubwa, kiasi kwamba majibizano hayo yamefikia hatua ya kukomoana kibiashara. 

Vita hivyo pia ni kati ya utawala wa Kigali na Bujumbura, hali hiyo imefikia hatua ya kuwapiga marufuku wananchi wanaoishi mipakani kutoshirikiana wala kufanya biashara yoyote baina yao. 

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, hivi karibuni imeripoti kuwa Serikali ya Rwanda imewasihi wananchi wake walioko karibu na mpaka kati ya nchi hiyo na Burundi kusitisha biashara zao. 

Hatua hiyo ilikuja baada ya Rwanda kuwakataza wananchi wake kwenda nchini Uganda. Rwanda inashutumu nchi hizo kusaidia makundi ya waasi yanayoipinga.

Wito wa kuwakataza wananchi wa maeneo ya mpakani mwa Rwanda na Burundi kutokwenda nchini humo umetolewa na Ofisa wa Jeshi la Rwanda, Jenerali Mbarac Muganga, wakati wa mkutano wa usalama baina yake, wananchi na viongozi wa maeneo ya mpakani upande wa Kusini Mashariki.

Imeelezwa kuwa Jenerali Muganga amewataka kusitisha shughuli zote zinazoweza kuwalazimisha kwenda nchini Burundi hata kama itakuwa ni kuoa au kuolewa na mtu kutoka upande wa pili.

Ikumbukwe kuwa miaka mitatu iliyopita Burundi ilitangaza kusitisha biashara yake na Rwanda hasa mboga na matunda na pia kusitisha misafara ya mabasi ya abiria kutoka Rwanda.

Wakati hayo yanatokea jina la Paul Kagame Rais wa Rwanda linasimama katikati ya migogoro hiyo hali ambayo inatishia ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Rais wa Uganda Yoweri Museveni, amewahi kukiri kuwa uhusiano mbovu baina ya mwanachama yeyote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unaathiri masuala ya kiuchumi ikiwemo soko la pamoja. 

“Nakiri kuwa mgogoro baina ya Rwanda na Burundi unapaswa kujadiliwa. Hilo ni kwa mantiki ya soko la pamoja. Suala la soko la pamoja ni muhimu, linahusu usafirishaji au usambazaji wa bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine na kinyume chake. Uhuru wa watu na kufanya biashara miongoni mwa nchi wanachama. Iwapo kuna mgogoro, ni kwa kiasi gani familia, wafanyabiashara, kampuni zinaweza kuwa na maendeleo?” aliandika Yoweri Museveni katika barua yake kwenda kwa Rais Pierre Nkurunziza Desemba 8, mwaka 2018.

Maelezo ya Museveni yanaturejesha kwenye uhusiano mbovu uliopo katika nchi tatu kwa sasa, ambazo ni Uganda, Burundi na Rwanda. Tunafahamu kuwa nchi za Uganda na Rwanda zimekuwa kwenye msuguano muda mrefu sasa, hali kadhalika uhusiano wa Burundi na Rwanda ni mbaya. 

Ikumbukwe Februari mwaka 2017 wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaowakilisha Burundi walikataa kuhudhuria vikao vya Bunge vilivyofanyika jijini Kigali, Rwanda kwa kuhofia usalama wao kutokana na uhusiano mbovu baina ya nchi hizo.

Matukio hayo yanaongezeka zaidi katika kipindi ambacho Rais wa Rwanda, Paul Kagame amekuwa Mwenyekiti Mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mbali ya Mwenyekiti huyo kutembelea Tanzania siku chache zilizopita, lakini amewahi kuingia kwenye mgogoro kati ya nchi yake ya Rwanda na Tanzania.  Ikumbukwe Oktoba mwaka 2013 Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alitangaza kuwa mgogoro wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Rwanda umemalizika. 

Chanzo cha mgogoro huo ni hatua ya Kikwete kuishauri nchi ya Rwanda pamoja na Uganda kuzungumza na waasi wa nchi zao waliopo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Jambo lililopingwa vikali na Rwanda kwa madai kwamba Rais Kikwete aliingilia mambo ya ndani ya nchi yao kwa kuwashauri kufanya mazungumzo na watu walioua raia wa nchi hiyo.

Ingawa Kikwete wakati huo hakutaja ni kwa namna gani mgogoro huo uliokuwa umefukuta baina ya Tanzania na Rwanda na vipi umepata ufumbuzi na kumalizika, lakini rekodi iko dhahiri kuwa Rwanda na Tanzania zilikuwa na mgogoro wa kidiplomasia.

Shutuma mpya za Rwanda dhidi ya Uganda zinaibua hoja ileile ya kuwafadhili waasi wanaoisumbua Serikali ya Kagame.  Burundi imeshutumiwa kufadhili waasi wanaopigana dhidi ya Serikali ya Rwanda. Uganda nayo inashutumiwa kwa jambo hilo hilo dhidi ya Rwanda.

Mwanzoni mwa mwaka 2018 kulikuwa na minong’ono ya mgogoro baridi kati ya Rwanda na Uganda. Duru za kisiasa nchini Uganda zilibainisha kuwa uamuzi wa Rais Museveni kufuta safari ya kwenda mjini Kigali, nchini Rwanda kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Mikataba ya Kibiashara barani Afrika uliotokana na ushauri aliopewa na wana usalama wake. Mataifa 55 ya Afrika yalialikwa. 

Taarifa za ulinzi na usalama zinasema Uganda haikuridhishwa na utaratibu wa kuwalinda marais waliotakiwa kuhudhuria mkutano huo. Wana usalama wa Uganda walikagua njia ya kuelekea makazi ambayo yangetumiwa na viongozi katika kipindi chote cha mkutano na barabara zilizopangwa kutumika. 

Taarifa zilizoritopitiwa na gazeti la Daily Monitor la Uganda toleo la Machi 21, 2018 zimesema kuwa wana usalama wa Rwanda walikataa kutoa ushirikiano wa timu ya ulinzi ya Uganda hali ambayo ilitoa dalili mbaya za usalama wa Museveni katika siku ambazo angekuwepo Rwanda.

“Kwa kawaida walinzi wa viongozi wanaotembelea nchi husika wanafanya kazi mapema na vikosi vya usalama vya nchi mwenyeji kuandaa masuala muhimu kwa rais anayetembelea nchi husika. Lakini kwa wakati huu (mwezi Machi) hali ilikuwa tofauti, hapakuwa na ushirikiano wala uwazi,” kilisema chanzo cha habari kilichozungumza na Daily Monitor.

Kikosi cha usalama cha Uganda kiliwasili Machi 12 mjini Kigali, lakini hadi Machi 18, 2018 hawakuwa wameambiwa ni hoteli ipi angefikia Rais Museveni wala magari ambayo angetumia katika msafara wake kipindi chote cha mkutano.  

Aidha, inaarifiwa hapakuwa na mkutano wowote wa wana usalama baina ya pande mbili hizo kama sehemu ya kuweka sawa masuala ya ulinzi wa kiongozi. Baada ya kushindwa kuendelea kuvumilia huku muda ukiyoyoma kikosi cha usalama cha Uganda kilitoa taarifa kwao kuwa hakukuwa na ushirikiano waliopata kutoka kwa wenyeji. Hapo hapo Rais Museveni akafuta ziara ya kwenda Rwanda mkutanoni. 

Hii ni moja ya ishara za mgogoro baina ya vikosi vya ulinzi na usalama, mgogoro baina ya nchi na nchi na zaidi kiubinadamu inawezekana kukisia kuwa ‘hii ni dharau’. 

Kwa upande wa Rwanda walilalamikia idadi ya ujumbe wa Uganda wa watu 60 ambao ni mkubwa mno kinyume cha taarifa iliyotumwa awali iliyotumwa Kigali. Ikumbukwe kwa miaka kadhaa uhusiano wa Rwanda na Uganda haukuwa mzuri hadi mwaka 2010 ambapo ulirejeshwa kama kawaida.

Hivi karibuni Rais Kagame amekaririwa na gazeti la The East Africa, kuwa mgogoro wao na Uganda umetengenezwa Afrika Kusini, kwamba Museveni anawasikiliza zaidi Afrika Kusini kuliko Rwanda. 

Mantiki inaleta maswali hapa, ni kwanini iwe Rwanda kila mara? Kwa sababu hadi sasa Rwanda imegombana na Tanzania, Burundi na Uganda, pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika eneo la maziwa makuu. Hii ina maana Rwanda haijagombana na Kenya peke yake. 

Wakati Rwanda sasa ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inaleta mkanganyiko kuwa ni namna gani Rais Kagame ataweza kusuluhisha migogoro inayomhusu moja kwa moja. 

Viongozi wetu wa EAC,wanao wajibu wa kuandaa maisha na mazingira mazuri kwa vizazi vijavyo. Hali ilivyo sasa inatia wasiwasi kuhusiana na mustakabali wa EAC kutokana na migogoro ya wanachama wenyewe kwa wenyewe. Je watamudu vipi kukabiliana na adui wa nje ikiwa wenyewe hawapatani?

Baruapepe; [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,663FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles