28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif kuvuka au kukwama 2020?

Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

CHAMA cha ACT-Wazalendo hivi sasa ndicho chama cha upinzani kinachoonekana kuibua mijadala mipana katika ulingo wa kisiasa nchini.

Joto la kisiasa limepanda zaidi baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi- CUF Maalim Seif Sharif Hamad, kuhamia ACT-Wazalendo huku akizoa wafuasi lukuki wa CUF, Bara na Visiwani.

Kiongozi huyo ambaye anaonekana kuwa mwiba wa siasa za upinzani nchini alikihama CUF mara baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutoa huku iliyoidhinisha uamuzi wa msajili wa vyama vya kisiasa nchini, kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF.

Kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2016, ilifunguliwa na kambi ya Maalim Seif ikipinga msajili wa vyama vya siasa kumtambua Lipumba baada ya yeye mwenyewe kujiuzulu na mkutano mkuu wa Chama hicho taifa kuridhia kujiuzulu kwake, hata hivyo Profesa Lipumba alirejea na kuitaka nafasi yake ya uenyekiti, hali iliyoibua mgogoro ndani ya Chama hicho na kufikishana mahakamani.

Baada ya uamuzi huo wa mahakama na Maalim Seif kujiunga ACT-Wazalendo, kuna matukio kadhaa wamejitokeza ambayo ndiyo msingi wa makala haya.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ni kama imeibua mgogoro mpya baada ya kuandika barua ya nia yake ya kutaka kukifuta Chama cha ACT-Wazalendo.

Katika barua hiyo ofisi hiyo ya msajili imekituhumu ACT kukiuka sheria baada ya picha za video kuwaonesha watu wanaodaiwa ni wanachama wa chama hicho wakichoma moto bendera na kadi za CUF.

Pia, Chama hicho kinatuhumiwa kutumia dini katika siasa zake, kutokana na kuonekana katika mitandao ya kijamii vijana wakipandisha bendera ya ACT-Wazalendo kwa kutumia tamko takatifu la dini ya Kiislamu (Takbir), kitendo kinachokiuka kifungu cha 9 (1)(C) cha sheria hiyo.

Chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei 5, 2014 kinatuhumiwa kutowasilisha taarifa za hesabu za ukaguzi za mwaka wa fedha 2013/2014, ambapo barua hiyo ilieleza kuwa kushindwa kuwasilisha hesabu hizo kinakuwa kimekiuka sheria ya vyama vya siasa sura ya 258. 

Hata hivyo Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amedai kuwa hesabu za mwaka huo wa fedha ziliunganishwa katika mwaka wa fedha 2014/2015 kwa kutumia kanuni za kimataifa za kihasibu pamoja na ushauri wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kuwa chama hicho kilipata usajili wake miezi miwili tu kabla ya kwisha kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Nijikite kuhusu tuhuma za wanachama wa ACT kudaiwa kuchoma bendera, hilo ni jambo la kufikirisha.

Katika hali ya kawaida na kwa kuzingatia mazingira yaliyoonekana kupitia video hizo wakishusha na kuchoma bendera za CUF ni watu walikuwa wameghadhabika na waliojawa hasira huenda ni kutokana na uamuzi wa kumridhia Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF. 

Hoja yangu ya kwamba tuhuma hizo zinafikirisha msingi wake ni kuwa kama kweli walikuwa wafuasi wa Maalim Seif basi si sahihi hata kidogo kukituhumu ACT-Wazalendo kwa sababu hawakuwa wanachama wake,  kwani kwa wakati ule hawakuwa wamejiunga na chama hicho, ikizingatia kuwa hata Maalimu Seif mwenyewe alipata kadi ya uanachama wa chama hicho siku moja baadaye.

Kwa mtu yeyote mwenye busara hawezi kuunga mkono vitendo vya uvunjifu wa sheria wa aina ile ambao unaweza kujenga chuki katika jamii. Lakini ofisi ya msajili ilipaswa kujiridhisha kabla ya hatua iliyoichukua ya kukituhumu ACT-Wazalendo moja kwa moja kwa sababu haitoshi kuishia kuona picha za mtandaoni na kuchukua hatua, ofisi hiyo ingelazimika kwa kubeba msalaba wa kuthibitisha ukweli kwa kuwathibitisha wahusika pasi na shaka kuwa walikuwa wanachama wa ACT tena hata kwa kuonesha sura na kadi zao za uanachama.

Kuna swali jingine hivi kwanini hili la hesabu linaibuka leo kwa ACT- Wazalendo? Je; ndicho chama pekee chenye hati chafu. Rekodi zinaonesha karibu vyama vyote vilivyokaguliwa havikupata hati safi na hakuna hatua hata moja iliyochukuliwa dhidi yao.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaonyesha wasiwasi kuhusu hoja hiyo ya uwasilishaji wa taarifa ya ukaguzi huku wakiitaja kama hoja iliyochomekwa kichakani ili isionekane kama anayeandamwa ni Maalim Seif.

Wasiwasi huu unatokana na hatua ya awali ya Ofisi ya Msajili iliyomtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF wakati pande hizo mbili zikiwa katika mgogoro ambao umefikia ukomo hivi karibuni baada ya Mahakama kumpa ushindi Profesa Lipumba.

Kwa barua ya hivi karibuni ni kama ofisi ya msajili inatumia mamlaka yake kuitisha ACT, na kudhoofisha demokrasia ya vyama vingi kwa kushindwa kusimamia jukumu lake kuwa mlezi wa vyama.

Inadhoofisha demokrasia kuchukua hatua kwa baadhi tu ya vyama huku vyama vingine vikiachwa na kuondoa usawa wa kidemokrasia kati ya chama kimoja na kingine. 

Kwa siku za karibuni kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu vyama vya upinzani kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara, maandamano huku hata mikutano ya ndani ambayo haijawekewa zuio lolote wakiishia kutawanywa na kukamatwa na polisi.

Mikutano ya wabunge katika maeneo yao pia imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo kunyimwa vibali na pale wanapopewa vibali hivyo huzuiwa na polisi kwa madai ya kutokuwapo kwa polisi wa kutosha kuimarisha usalama.

Katika mazingira hayo hayo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu Mkuu wake, Dk. Bashiru Ally na Katibu wa Uenezi Humphrey Polepole wamekuwa wakiendelea na mikutano kama hiyo na hata kudiriki kusema kuwa wananchi ndiyo huwafuata na si wao wanaowaita katika mikutano hiyo.

Katika mazingira haya ofisi ya msajili haiwezi kuepuka kikombe hiki cha lawama, endapo haitasahihisha kasoro hizo za wazi.

Je; hali hii inayoendelea sasa kati ya ofisi ya msajili na ACT-Wazalendo ni kiashirio kuwa ule mgogoro uliokuwa ukifukuta ndani ya CUF sasa unataka kuhamishiwa ACT-Wazalendo baada ya Maalim Seif kuhamia huko? Iwapo jibu ni ndiyo kwa manufaa ya nani hadi ofisi ya msajili itake kuifuta ACT?

Ni wazi kuwa Maalim Seif amekuwa na ushawishi mkubwa Zanzibar hali iliyofanya eneo lote la Pemba kuwa ni ngome muhimu kwa CUF ambapo majimbo yote 18 ya uchaguzi katika eneo hilo yako chini yake.

Majimbo yote 18 yaani tisa ya Kaskazini Pemba na mengine tisa ya Kusini Pemba yote yako chini ya CUF. Na kwa Zanzibar yote chama hicho kina jumla ya viti 22 kati ya viti 50 vya uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi la Visiwa hivyo.

Hakuna ubishi kuwa ushindi huo wa CUF ulichagizwa zaidi na Maalim Seif, kuliko hata CUF yenyewe kwa kuzingatia kuwa chama hicho kilikuwa kikikabiliana na vyama vingine katika chaguzi mbalimbali kikiwamo CCM ambacho kimekuwa na ushawishi kwa pande zote za Muungano. 

Ushindi wake ulitokana na imani kubwa ya wananchi kisiwani humo ambao huwatazama kama wenye kumwamini zaidi mtu kuliko chama. Je, ushawishi wake huo ndiyo unaozalisha hofu hii tunayoishughudia leo.

Kama kweli dhana hiyo inayojengeka miongini mwa watu kuwa ofisi ya msajili inamwandama kiongozi huyo mkongwe wa upinzani kiasi cha kutaka kuifuta ACT, je itakuaje endapo atahamia Chadema na vipi kama ataamua kurejea katika chama chake cha mwanzo CCM navyo pia vitafutwa na nini mwisho wake? 

Mgogoro wa sasa unaingia katika awamu nyingine huku wanachama na wafuasi wakiwa wamegawanyika, kwa hali ilivyo nini kitatokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani huko visiwani Zanzibar na Tanzania Bara?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles