28.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Tanzania yang’ara Benki ya Dunia

Na Mwandishi Wetu,

 -Washington DC Marekani

TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika kukabiliana na tatizo la makazi holela duniani.

Takwimu zinaonyesha zaidi ya watu bilioni 1 kati ya bilioni 7.4 duniani wanaishi katika makazi holela bila kuwa na umiliki halali wa maeneo yao huku wakikabiliwa pia na hali duni ya miundombinu, uhaba wa huduma za kijamii na migogoro sugu ya ardhi.

Hata hivyo, hatua ya Serikali ya Tanzania kushirikisha sekta binafsi katika kupangilia miji, kupima viwanja na kumilikisha ardhi kwa hatimiliki imeleta tija na kuongeza kasi kubwa katika kurasimisha na kuboresha makazi holela nchini.

Hayo yameelezwa na Mratibu Mwandamizi wa Miradi wa Kampuni ya Mipango Miji ya HUSEA, Edward Kinabo, katika Mkutano Mkuu wa Benki ya Dunia unaohusu ardhi na umasikini, unaoendelea jijini Washington nchini Marekani.

Akiwasilisha mada jana, kwa niaba ya Kampuni ya HUSEA iliyohusu mafanikio ya ubia baina ya sekta binafsi na jamii katika kurasimisha makazi kwa kutumia fedha zinazochangwa na wananchi wenyewe, Kinabo, alisema kwa miaka mingi ongezeko la idadi ya watu na ukuaji wa kasi wa miji dhidi ya uhaba wa bajeti, nguvu kazi na vitendea kazi, vilisababisha kuwepo kwa kasi ndogo ya upangaji miji na hivyo kukithiri kwa makazi holela mijini kwa zaidi ya asilimia 70.

Hata hivyo, alifafanua kuwa kupitia mazoezi shirikishi ya kuchangia gharama yanayotekelezwa na kampuni binafsi sasa maelfu ya wananchi wanapata fursa ya kumiliki maeneo yao kisheria.

Alisema hatua ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushirikisha kampuni binafsi, imeleta tija na kasi kubwa katika kukabiliana na makazi holela nchini.

“Tunampongeza Waziri wetu wa ardhi kwa uamuzi sahihi wa kushirikisha sekta binafsi na kuwa mhamasishaji mkuu wa urasimishaji wa makazi, jitihada hizi zimeleta tija na kasi kubwa,” alisema Kinabo.

Mkutano huo wa Benki ya Dunia unashirikisha wadau wa maendeleo  kutoka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo viongozi na maofisa wa Serikali, Asasi za Kiraia na wawakilishi kutoka sekta binafsi wakiwemo watoa mada walioalikwa kutoa uzoefu juu ya namna bora ya kushughulikia masuala yahusuyo ardhi na umasikini.

Akifafanua kuhusu kasi ya urasimishaji makazi nchini, Kinabo, alisema Kampuni ya HUSEA pekee imeweza kuandaa ramani za mipango miji na kuratibu upimaji wa zaidi ya viwanja 30,000 katika mitaa mbalimbali ya Manispaa za Ubungo, Kinondoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam, huku kampuni hiyo ikiwa katika hatua za awali za kufanya kazi kubwa zaidi katika Jiji la Mbeya, Arusha na Mkoa wa Songwe.

Awali, akichambua takwimu za hali halisi ya nchi kuhusu ongezeko la watu na makazi holela, Kinabo, alisema Ripoti ya Hali ya Maendeleo ya Binadamu Tanzania iliyotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) mwaka 2017, inaonyesha idadi ya watu nchini inaongezeka kwa zaidi ya asilimia 2.7, sawa na ongezeko la watu milioni 1.2 kwa mwaka. 

Aidha, akinukuu Ripoti ya Shirika la Makazi Duniani (UN Habitat) ya mwaka 2016 kuhusu Ukuaji wa Majiji, alisema wakati theluthi mbili ya watu wote duniani watakuwa wanaishi mijini ifikapo mwaka 2050, huku asilimia 90 wakitarajiwa kutokea ndani ya Bara la Afrika na Asia, Tanzania itakuwa ni nchi ya tisa kwa kuwa watu wengi waishio mijini, ikitanguliwa na India, China, Indonesia, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  

“Kwa kadiri idadi ya watu inavyozidi kuongezeka mijini kuliko vijijini, ndivyo  kiini cha umasikini wa dunia kinavyozidi kuhamia mijini kutoka vijijini. Ile dhana iliyozoeleka kuwa umasikini umekithiri vijijini tu sasa imepitwa na wakati,”  alisema Kinabo.

Mkutano huo ulioanza Machi 25 na kumalizika juzi, ulihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Kampuni ya Mipangomiji  ya HUSEA na Makamu wa Rais wa Chama cha Wataalamu wa Mipango Miji nchini, Renny Chiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,908FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles