24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA: SERIKALI INASHUGHULIKIA MATUKIO YA UHALIFU

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

SERIKALI imewataka wananchi na wabunge waendelee kuwa watulivu wakati inaposhughulikia matukio ya uhalifu hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa bungeni jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipowasilisha hoja ya kuahirisha Bunge hadi Novemba 7, mwaka huu.

“Nitumie fursa hii kuungana na Rais Dk. John Magufuli kutoa pole nyingi kwa Meja Jenerali mstaafu, Vincent Mritaba, kutokana na tukio la kushambuliwa kwa risasi, Septemba 11, mwaka huu.

“Serikali inalaani vitendo hivyo na matukio hayo ya kinyama, ingawa ni mwezi na nusu sasa, tumeanza kuwa na utulivu kufuatia vifo vya raia na askari wetu wa Jeshi la Polisi waliouawa kikatili huko maeneo ya Mbagala, Dar es Salaam, Mkuranga, Rufiji na Kibiti, mkoani Pwani.

“Nisisitize tu kwamba, kwa matukio haya, Serikali haitayafumbia macho na tayari vyombo vya ulinzi na usalama vimeshaagizwa kuwatafuta kwa mbinu zote wale wote waliohusika katika uhalifu huo.

“Kwa hiyo, nawasihi wameshimiwa wabunge na Watanzania wote, wavute subira wakati Serikali na vyombo vya dola vikishughulikia matukio haya kwa umakini, ingawa jambo la msingi ni kila mmoja kudumisha ulinzi na usalama nchini,” alisema.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Majaliwa alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kuimarisha uzalishaji wa mazao makuu matano ya biashara, yakiwamo pamba, tumbaku, korosho, chai na kahawa.

Pia aliyataja mazao mengine ya biashara yatakayowekewa mkazo na Serikali kuwa ni katani, ufuta, alizeti, mbaazi na ngano.

Kuhusu sekta ya elimu, aliwataka viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri zote nchini, kuhakikisha fedha za kugharamia elimu bila malipo zinatumika vizuri na kwa makusudi yaliyokusudiwa.

Akizungumzia sekta ya afya, alisema hadi kufikia Agosti, mwaka huu, Serikali ilikuwa imesambaza hospitalini vitanda 3,208 katika halmashauri 162, magodoro 3,189 katika halmashauri 160, mashuka 7,570 katika halmashauri 159 na jumla ya vitanda 322 vya kujifungulia katika halmashauri 69 nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles