24.6 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

WAZEE ACT-WAZALENDO KIGOMA WAMVAA NDUGAI

 

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

NGOME ya wazee wa Chama cha ACT-Wazalendo mkoani Kigoma, imesikitishwa na kauli zilizotolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alikaririwa akisema ana uwezo wa kumzuia Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, kutochangia chochote ndani ya Bunge mpaka mwisho wa ubunge wake.

Katika taarifa yao kwa umma jana, wazee hao walidai endapo Ndugai atatekeleza mpango huo dhidi ya Zitto, basi watamshtaki kwa Mwenyezi Mungu.

Mwenyekiti wa ngome hiyo, Alhaj Jaffar Kasisiko, alisema wazee hao baada ya kusikia kauli za Spika Ndugai   dhidi ya mbunge wao walimwomba arejee Kigoma kwa ajili ya kuelezea kiini cha kauli hiyo kabla ya kwenda  mbele kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.

“Baada ya kumsikiliza sisi wazazi wake tumemruhusu aende  mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ili aweze kuhojiwa.

“Ngome ya wazee imesikitishwa na  kauli ya Spika kitendo cha kumzuia Zitto ni sawa na kutuzuia sisi wazee na wananchi wa Kigoma kusemewa ndani ya Bunge,” alisema Alhaj Kasisiko.

Alisema kauli hiyo ya spika inaonyesha kumhukumu  mbunge huyo hivyo kuitwa kwake  kwenye kamati ni kama  anaenda kupoteza muda.

“Jambo hili halimtendei haki kijana wetu wala halitutendei haki sisi wazee tunaomtegemea, siku zote sisi wazee wa Kigoma tulikuwa tukimwona na kumchukulia Job (Spika) kama alivyo mtoto wetu, kusema kwamba Zitto hana cha kumfanya kimetufedhehesha na kinaendelea kutushangaza,” alisema Alhaj Kasisiko.

Alisema endapo Ndugai atatekeleza suala hilo, wao kama wazazi hawana chakumfanya kiongozi huyo zaidi ya kumshtaki kwa Mungu.

Majibizano baina ya Ndugai na Zitto yalianza baada ya kiongozi huyo wa ACT – Wazalendo kusema kwamba Bunge limewekwa mfukoni na mhimili fulani wakati alipotoa maoni kuhusu ripoti mbili za kamati ya Bunge za almasi na tanzanite.

Mbali na shutuma hizo, mbunge huyo aliandika katika akaunti yake ya Twitter kwamba: “Hatujawahi kuwa na Spika anayedhalilishwa na Rais kwamba aliuliza wajumbe gani awaweke kamati za uchunguzi za Bunge.”

Kauli za Zitto zilisababisha Spika Ndugai kuagiza mbunge huyo ahojiwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge huku akimshtaki kwa wapigakura wake akisema licha ya kwamba mbunge wao yupo nchini, hajafika bungeni kuwawakilisha na yeye (Spika) hana taarifa.

Baada ya Spika Ndugai kutoa mwongozo huo, baadaye jioni Zitto aliandika tena katika akaunti yake hiyo maneno kadhaa ikiwamo: “Bunge la 11 halitii mshawasha. Ndugai anajua namna Bunge la Tisa na 10 lilivyokuwa. Hata kamati hazina kazi. Zakutana wiki moja tu siku hizi.”

Zitto pia aliandika: “Spika Ndugai amekuwa Spika wa kwanza katika historia ya nchi yetu kushuhudia mbunge anapigwa risasi Mkutano wa Bunge ukiendelea.”

Baada ya kauli hizo, ndipo Spika Ndugai alipolitangazia Bunge kwamba Zitto apelekwe kwa mara ya pili katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuhojiwa kwa kulidharau Bunge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles