PRETORIA, AFRIKA KUSINI
MAHAKAMA ya Juu zaidi nchini Afrika Kusini imeamuru kuwa kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma inaweza kufanywa kwa siri.
Mahakama ya Katiba ilisema kuwa spika wa bunge ana haki ya kuamuru hatua kama hiyo, ikipingana na madai kuwa hakuwa na mamlaka kama hayo.
Vyama vya upnzani vinaamini kuwa chini ya kura ya siri, wabunge kutoka chama tawala cha Zuma cha African National Congress (ANC) wanaweza kupiga kura ya kumpinga.
Zuma amekuwa akiponea kura za kutokuwa na imani katika kile kilichoonekana woga wa baadhi ya wabunge wa chama chake kumpinga hadharani.
Amekuwa chini ya shinikizo kufuatia shutuma nyingi ikiwemo madai ya ufisadi na mabadiliko tata ya baraza la mawaziri.
Akitoa uamuzi huo Jaji Mkuu Mgoeng Mgoeng, alisema spika wa bunge ana mamlaka ya kuamua ni njia gani kura hiyo itafanyika.
Spika wa Bunge, Baleka Mbete ni afisa wa cheo cha juu ANC na alikuwa amedai sheria za bunge haziruhusu kufanyika kura ya siri,
Kwa sasa tarehe mpya ya kufanyika kura hiyo ya kutokuwa na imani itatangazwa baadaye.