26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TANGA WALIVYOTHUBUTU KUWAKOMBOA WASICHANA 700 WALIOSHINDWA KUHITIMU SHULE

Na Amina Omari, Tanga


SERIKALI imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha mtoto wa kike anakombolewa na kupata elimu sawa na mtoto wa kiume. Lengo ni kumuwezesha kumudu maisha hapo baadae kwani maisha bila ya elimu hayawezekani.

Mikakati hiyo imekuwa ikichukuliwa kwa kuhakikisha kunakuwapo mazingira bora na shawishi ili mtoto wa kike aweze kupata fursa ya elimu kwa ufanisi mkubwa.

Licha ya mikakati hiyo, bado mtoto wa kike amekuwa akipatwa na changamoto nyingi ambazo zimechangia kurudisha nyuma juhudi hizo.

Moja ya changamoto kubwa inayomkabili mtoto wa kike ni mimba za utotoni. Watoto wengi hukwamisha ndoto zao za kuendelea na masomo na kuishia kuwa mama wa nyumbani baada ya kupata mimba.

Mwaka 2015 Mkoa wa Tanga pekee ulifanikiwa kudahili  wasichana 10,995 kwa masomo ya sekondari, lakini walioweza kufanikiwa kufanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne walikuwa 10,055.

Hii inamaana kuwa kuna wasichana zaidi ya 900 ambao hawakupata fursa ya kumaliza elimu ya sekondari na sasa wako mitaani wakiwa hawana kazi za kufanya kwa kukosa sifa ya kuajiriwa.

Baada ya kuona changamoto hiyo, Shirika la Maendeleo la BRAC walilazimika kuja na mradi wa kuwajengea uwezo na kuwapatia fursa ya kukuza na kujiendeleza kiuchumi wasichana waliokosa fursa ya masomo na wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Tanga.

Meneja Mipango na Elimu,  Amina Shaaban anasema kuwa lengo la kuja na mradi huo kwa mkoani Tanga ni kusaidiana na serikali katika kupunguza tatizo la ajira na changamoto za elimu kwa watoto wa kike.

Anasema kuwa kwa kuanzia mradi huo umeweza kuwafikia jumla ya wasichana 1200 ambao baadhi yao waliweza kupata fursa ya kujiendeleza kimasomo na kujifunza stadi za maisha.

Anasema kuwa kupitia mradi huo wasichana hao waliweza kupata fursa ya kurudia mitihani ili kupata sifa za kurudi darasani na wengine kupatiwa mafunzo  mbalimbali ya ujasirimali.

“Hadi sasa jumla ya wasichana 116 wanaendelea na masomo ya kidato cha nne na wengine zaidi ya 900 wanaendelea kupatiwa mafunzo ya ujasirimali pamoja na uanzishwaji wa biashara na kuzisimamia,”anasema Shaaban.

Anasema miongoni mwa mambo waliyojifunza ni ufugaji wa kuku, upishi, ushonaji wa nguo, kilimo cha mbogamboga, kutengeneza batiki na mabegi.

Meneja huyo anasema kupitia mafunzo hayo wasichana wameweza kufaidika na kupatiwa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuanzisha biashara zao ili waweze kujiongezea kipato.

“Shirika limewakabidhi jumla ya vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 153 kwa ajili ya msaada wa vifaa vya kuanzisha biashara kwa wasichana 700 mkoani humo,” anasema Shaaban.

Anataja vifaa walivyovitoa kuwa ni pamoja na vyerehani 90, mashine za kukaushia nywele 90 (hairdriers), vifaa kwa ajili ya ufugaji, kilimo, vifaa vya upishi pamoja na vifaa kwa ajili ya kutengenezea batiki na mabegi.

“Tunaamini vifaa hivyo vitaweza kutumika katika harakati za kujikwamua kiuchumi pamoja na familia zao,  pia watapata ari ya kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizoko mkoani hapo,” anasema meneja mradi huyo.

Shaaban anasema licha ya vifaa hivyo, wasichana hao wataweza kuunganishwa na fursa ya mikopo inayotolewa na shirika hilo ili kuweza kukuza mitaji yao.

“Licha ya kuwapa vifaa lakini pia tunataka wakope fedha taslimu kupitia BRAC ili iwasaidie katika kuimarisha bidhaa zao,” anabainisha meneja huyo.

Nao baadhi ya wasichana walioweza kunufaika na mradi huo wamesema umeweza kuwakwamua kutoka katika lindi la umaskini na kuamsha chachu ya kujiendeleza kiuchumi.

Mmoja wa wasichana walionufaika na fursa hiyo, Aisha Mohamed anasema baada ya kumaliza masomo mwaka 2013 na kufeli alikaa nyumba bila ya kazi yoyote.

“Nilikata tamaa ya kuendelea na masomo baada ya kufeli lakini nilipopata fursa ya kushiriki katika mradi wa BRAC imenisaidia kutimiza ndoto yangu ya kuwa fundi cherehani,” anasema.

Aisha anasema wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumwendeleza kielimu hivyo baada ya kupata vitendea kazi ataweza kujikwamua kiuchumi kwa kufanya kazi ya ufundi wa kushona nguo.

“Niwaombe wasichana wenzangu tukimbilie fursa iliyopo, badala ya kujiingiza kwenye tabia hatarishi ambazo zinaweza kutuletea madhara makubwa kijamii na kiuchumi ni heri tujifunze kufanya kazi za mikono,” anawaasa wasichana wenzake.

Naye Joyce Michael anawaasa wazazi kuhakikisha wanatoa fursa kwa watoto wao wa kike ambao wameshindwa kuendelea na masomo, wajifunza ujasirimali ili waweze kujikomboa kiuchumi.

Anasema ili kumkomboa mtoto wa kike ni muhimu kumlinda, kumwezesha na kumwendeleza ili asiweze kujiingiza katika tabia hatarishi kama uhuni na unywaji pombe.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Zena Said anasema wasichana ni kundi linalohitaji kuangaliwa kwa jicho la tatu ili asiweze kujiingiza katika vishawishi na kuishia kupata maradhi.

Anasema kuwapo kwa mradi huo kutaleta ukombozi wa kweli kwa mtoto wa kike kwa kuwa utamsaidia kuanza kujitegemea kupitia elimu ya stadi za kazi alizozipata.

Anaongeza kuwa mradi huo unaosimamiwa na shirika hilo umeonyesha njia ya kumkomboa  mtoto wa kike kwani kwa kiasi kikubwa amekuwa ni muhanga katika tatizo la ukosefu wa ajira.

“Mradi huu umekuja wakati mwafaka ambapo serikali ya mkoa ipo katika maandalizi ya kupokea fursa mbalimbali za kiuchumi zinazokuja ikiwamo ujio wa bomba la mafuta,” anasema katibu tawala huyo.

Zena anaamini kuwa mradi huo ni fursa pekee kwa wasichana wa mkoa huo kuweza kujiendeleza kiuchumi na kuwasaidia kuwaepusha na kujiingiza katika tabia hatarishi.

“Kuwakomboa wasichana 700 si jambo dogo ni jambo la kishujaa na kutiwa moyo. Serikali tutahakikisha tunaunga mkono juhudi hizo mlizozianzisha ili kuweza kumjenga mtoto wa kike aweze kujitegemea,” anasema.

Anawaagiza maofisa maendeleo ya jamii mkoani hapo kuhakikisha wanawaunganisha wasichana hao na fursa za mikopo ya asilimia 5 za halimashauri ili waweze kuchangamkia fursa hiyo katika kukuza mitaji yao.

Anasema kuwa wanahitaji wasichana hao kuwa na maendeleo endelevu hivyo ni vema kuanza kuwafuatilia katika hatua zote ili biashara zao ziimarike.

“Tumezoea kuona miradi mingi ikiishia hewani lakini kwa huu wa kuendeleza wasichana naomba maofisa maendeleo muhakikishe mnawafuatilia kwa ukaribu vijana hao ili kujua maendeleo yao,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles