32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 1, 2023

Contact us: [email protected]

Magufuli: Viongozi wa michezo walikuwa wezi

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAMRAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amesema viongozi wa michezo walikuwa wa hovyo katika kipindi fulani, hali iliyofanya Shirikisho la Kimataifa la Soka la Kimataifa (FIFA) kusitisha  kutoa fedha kutokana na matumizi mabaya.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana, Ikulu, jijini Dar es Salaam, alipokutana na wachezaji wa Stars na viongozi wa Shirikisho la SokaTanzania (TFF), akiwamo Rais Wallace Karia.

Magufuli alisema viongozi wa michezo  wengi wamekuwa wezi,  ndiyo maana Rais wa Shirikisho la Soka, Karia alisema kuwa FIFA walikataa kutoa fedha ambazo zilitakiwa kutolewa kwa maendeleo ya soka kutokana na kubainika kwa  matumizi mabaya ya zile walizokuwa wanatoa.

“Viongozi wengi wa michezo katika kipindi fulani walikuwa ni wa hovyo na ndiyo maana nilipoingia madarakani nilisema hawa wanaohusika na rushwa hata kama ipo kwenye michezo, lazima wapelekwe mahakamani ili wakajifunze dhambi ya kula fedha za watu,” alifafanua Magufuli.

“Mtu anahangaika sana kuomba nafasi ya uongozi kwa  kuhonga, lakini wakishapata wanaenda kurudisha zile fedha walizotoa,” alisema.

Alisema  hali hiyo, imechangia kuwakatisha  tamaa wachezaji  na kushindwa  kujituma katika kufanya kazi yao ya kucheza, hasa wanapowaona viongozi wao wanavyotumbua fedha zinazopatikana na jasho la wachezaji.

Magufuli alisema kwa kitendo hicho, Tanzania imekosa fedha dola laki tatu kutoka FIFA kwa sababu ya rushwa wakati nchini nyingine wanaendelea kupewa.

“Matumizi mabaya ya fedha hayafanywi na viongozi wa michezo tu, hata kwenye klabu ni hivyo hivyo, nazungumza kwa dhati vitu hivi vimekuwa vikiwakatisha tamaa Watanzania,” alisema.

Magufuli aliwataka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Leodger Tenga, wawe wakali kwa watu wanaotumia fedha za michezo.

Alisema lazima waimarishe namna ya kutengeneza fedha hata katika makusanyo ya viwanjani kwa kuhakikisha kila uwanja unatumia tiketi za kielektroniki ambayo Serikali kupata kodi vizuri.

Akikumbushia kichapo cha Cape Verde, Magufuli alisema ni aibu kwa Tanzania kushindwa kupata wachezaji 11 watakaoweza kuleta kombe la Afrika nyumbani, hali inayomsononesha kila mara.

Alisema Watanzani wengi wamekata tamaa kutokana na matokeo mabaya na ndiyo maana wengi wao wanashabikia soka la nje kuliko hapa nyumbani.

“Mheshimiwa Waziri alipokuwa akishughulikia kutafuta ndege, mimi nilikuwa katika hatua za mwisho za kutoa ndege bure, lakini nikapata taarifa kuwa uwanja wa huko ni mdogo, nilipoanza kufuatilia mchezo dakika chache tu mmeshafungwa, nikasema ni nafuu  uwanja umekuwa mfupi na ndege yangu sikutoa.

“Sikutoa ndege ya Serikali ya Tanzania kupeleka watu ambao walifungwa dakika za mwanzo tu halafu wakamalizia na dina ya bao moja, inasikitisha sana.

“Machungu ninayoyapata mimi ndiyo wanayopata  Watanzania, tangu mwaka 1980, hatujafanikiwa kufika tena fainali  za Afrika, cha ajabu, mnaitwa bungeni wanawapa viburi kwa kuwapongeza kwa vikombe vya ajabu ajabu, lakini ukweli  kimchezo hatufai,” alisema.

Alifikiria kuweka wanajeshi kucheza Taifa Stars

“Nilipoingia madarakani nilianza kufikiria kama timu zote hazifanikiwi labda nichukue timu ya wanajeshi, ambao kazi yao iwe ni mpira kuanzia asubuhi hadi jioni bila kufanya mazoezi mengine.”

Alisema mwelekeo wa Taifa Stars umeanza kumpa matumaini na hasa walipopata kocha mkuu, raia wa Nigeria, Emmanuel Amunike, kwani wakati anachezea timu yake ya Nigeria alikuwa ni mchezaji mzuri.

“Siku zote tumekuwa tukichukua makocha wa nchi nyingine za Ulaya,  labda tutakapokuwa na kocha mweusi atakuwa wa tofauti na machungu kwa sababu na yeye ni Mwafrika,” alisema.

Alisema timu hiyo ilivyofungwa mabao matatu ugenini ilimnyong’onyesha, lakini walivyowafunga nyumbani   mabao 2-0, hakufurahia sana, kwa sababu kulikuwa na deni la bao moja.

Magufuli alisema anahitaji kuona mchezo dhidi ya Lesotho wakishinda ana matumaini michezo mingine iliyobaki watashinda.

“Huu ndio muda wa kubadilika, Amunike yupo hapa, nawaomba wachezaji tuichukue hii kama vita na viongozi wa michezo msiingilie majukumu ya kocha katika kupanga kikosi ili lawama iwe inaenda kwake,” alisema.

Wachezaji watakiwa kuacha uhuni

Aliwataka wachezaji kuacha kujihusisha na mambo ya ulevi na uhuni, ili kuwa na wachezaji wazuri, kwani yanawafanya washindwe kupata mabao.

Achangia Taifa Stars milioni 50

Rais aliahidi kutoa Sh milioni 50  kwa maandalizi ya mechi ya Lesotho na kusema  zitumike kwa watu  wanaohusika.

“Hili nawaambia ndugu zangu, mmeingia kwenye mkataba wa ajabu, si mmekubali kuja hapa, nitafuatilia kweli na hii hela milioni hamsini nitajua mpaka senti tano imeliwa wapi na ole wako uile, siwezi kutoa hela milioni hamsini ya walipa kodi niwalipe halafu iwapeleke watu wengine wakachezee tu.

“Nataka ikatumike kwenye matumizi ya hawa vijana, wakacheze kweli kama ni kula, mpaka msuli unenepe kama kiazi, ale mguu uwe mkubwa akafunge magoli.

“Lesotho nayo ikatufunge? Itakuwa ni aibu, nitajuta kwa nini nilikuja kuwaona kwa sababu watatoka pale na kusema Magufuli amewapa mkosi  wale vijana, wamepigwa 10, nawaambia siriasi, kufungwa ni aibu mno,” alisisitiza Magufuli.

Ataka Usimba na Uyanga usiwepo Stars

Magufuli aliwataka wachezaji Taifa Stars wanapokutana kuwa kitu kimoja na si kuangalia timu wanazochezea bila kujali Simba, Yanga au Azam.

Alisema Taifa Stars wamepata bahati kufundishwa na kocha ambaye ana historia nzuri katika mpira, hivyo  aliwataka viongozi  kuhakikisha wanaongoza vizuri ili waweze kuandika historia.

Atoa kipaumbele kwa wachezaji wa ndani

“Tusiwategemee wachezaji wanaocheza kwenye klabu za nje, kwa sababu wakati mwingine wanakuwa hawajajua muunganiko wa timu na hawa waliopo, kwani wanawakuta wenzao wameshafanya mazoezi, ila kwa sababu ya jina la mchezaji wanafikiri yeye ndio ataweza kushinda tu.

“Ila si vibaya kuwatumia kwa sababu Mbwana Samatta alifunga bao, lakini ni vema wawe wanawahi mapema ili wazoeane na timu, kwani tunataka ushindi, kamwe tusishindwe tena, hivyo nawatakia kila la heri.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles