26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Uti wa mgongo watesa zaidi wanawake kuliko wanaume

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAMUTAFITI uliofanywa na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), umeonesha wanawake wanakabiliwa zaidi na matatizo ya uti wa mgongo ikilinganishwa na wanaume.

Moi walifanya utafiti huo kati ya kipindi cha Novemba, mwaka juzi hadi Septemba, mwaka jana na ulihusisha wagonjwa wapatao 100 waliohudhuria matibabu.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa Moi, Dk. Nicephorus Rutabasibwa, alisema watu wengi huhusisha hali hiyo na uzee bila kujua kwamba ni ugonjwa unaopaswa kutibiwa mapema.

Alisema tatizo hilo kitaalamu linaitwa ‘Degenerative Spine Diseases’ na huwakumba zaidi watu wanaokaa eneo moja kwa muda mrefu bila kushughulisha miili yao.

“Kwa mfano wanaokaa ofisini kwa muda mrefu au wale ambao hufanya shughuli zinazowalazimu kuinama kwa muda mrefu, kimsingi binadamu ameumbwa kusimama tofauti na wanyama wengine,” alisema.

Alisema ingawa kiuhalisia huwakumba watu wa jinsi zote, lakini matokeo yameonesha kati ya wagonjwa waliowapokea wanawake ni wengi zaidi ya wanaume.

“Tunadhani labda wanaume wanavumilia maumivu zaidi kuliko wanawake. Wanawake tulipowahoji wengi walitueleza wao ni mama wa nyumbani, wana shughuli nyingi zinazowalazimu kuinama kwa mfano kufua, kuchota maji na nyinginezo,” alisema na kuongeza:

“Vile vile, kibaiolojia wanawake wanapokoma hedhi hupata tatizo liitwalo kitaalamu osteoporosis ambalo hufanya mifupa inakosa nguvu kwa sababu inakosa yale madini ya calcium ambayo huimarisha mifupa.

“Hivyo, hali hiyo huongeza ule uwezekano wa wanawake kupata tatizo zaidi ya wanaume, katika utafiti huu asilimia 78 walikuwa ni wanawake kati ya wagonjwa wote.”

Alisema tafiti zinaonesha tatizo hilo huwapata zaidi watu wenye umri wa kuanzia miaka 35, lakini kwa upande wa Moi wagonjwa wanaopokewa wana umri kuanzia miaka 60 na kuendelea.

Alisema kati ya wagonjwa waliopokewa asilimia 58 walikuwa wakihisi maumivu ya mgongo, asilimia 78 walikuwa wanashindwa kutembea umbali wa kawaida pasipo kupumzika.

Alisema asilimia 58 walikuwa wanakabiliwa na tatizo la ganzi miguuni, asilimia 20 walikuwa wanashindwa kabisa kutembea na asilimia mbili wakiwa wanashindwa kuzuia haja ndogo.

“Yaani mtu anajikuta tayari amepata haja ndogo bila kujizuia jambo ambalo si kawaida, kibaiolojia mkojo huwa upo ‘controlled’ na mishipa ya fahamu na huwa kuna aina tatu za mishipa ya fahamu.

KUHUSU KIBOFU CHA MKOJO

“Kwenye kibofu kuna mishipa ya fahamu autonomic nervous system ambayo hufanya kazi ya kufunga na kufungua kibofu, yaani sypathetic na parasympathetic, ipo mishipa mingine ya fahamu ‘sokatic nerves’ kazi yake ni kuminya kibofu ili kisukume nje mkojo na hizo nerves zina supply misuli ya kibofu iitwayo detrusa muscles,” alisema na kuongeza:

“Hivyo uti wa mgongo unapokuwa umebana ile ‘supply’ ya ‘nerve’ kwenye kibofu nayo inapata shida na mtu kujikuta mkojo ukitoka bila kujitambua au anashindwa kabisa kupata mkojo, unabaki katika kibofu.

“Hii ni dalili mojawapo ya tatizo la uti wa mgongo, ingawa wengi hudhani kushindwa kupata haja ndogo ni matatizo ya mfumo wa mkojo au saratani ya tezidume kumbe la! Hata tatizo la uti wa mgongo hupelekea tatizo la mkojo.”

Pia alisema tatizo hilo hutibiwa ama kwa upasuaji au tiba ya mazoezi na dawa na mtu hupona kabisa.

“Changamoto tunayokumbana nayo, ni baadhi ya wagonjwa wengi kuogopa tiba ya upasuaji, kuna dhana potofu kwamba uti wa mgongo unapoguswa mgonjwa huwa haponi kabisa jambo ambalo si kweli,” alisema na kuongeza:

“Wanapona, wanatembea tena na wanarudi kuendelea na shughuli zao kama kawaida, mara nyingi wagonjwa tunaowafanyia upasuaji ni ya asilimia 10 ya wote wenye matatizo ya mgongo tunaowapokea, si lazima kutibiwa kwa upasuaji wagonjwa wote.

“Utaona zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa tunawatibu kwa tiba ya mazoezi na dawa, kupitia matibabu haya ndiyo tunaweza kubaini yupi anahitaji upasuaji, waje hospitalini wasiogope, tunatumia kipimo cha MRI kinachotuwezesha kubaini tatizo.

“Upasuaji huchukua kati ya saa mbili hadi tatu na kukamilika na mambo yakienda sawa sawa kama tulivyopanga tunao uwezo wa kuwafanyia upasuaji wagonjwa watatu hadi wanne kwa siku. Kipindi cha Januari hadi Agosti, mwaka huu tumewafanyia upasuaji wagonjwa zaidi ya 170.”

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,277FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles