30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

Maeneo nane watakayopitia wafanyabiashara 2019/20

  • TRA yaeleza namna itakavyosimamia kila hatua

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

WAKATI mwaka mpya wa Serikali wa 2019/2020 ukiwa umeanza jana, utekelezaji wa mipango ya Serikali pia umeanza rasmi.

Mwaka huo unaanza huku Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wafanyabiashara kutokana na tozo mbalimbali za kodi, ikiwa imefanya mabadiliko baadhi ya maeneo, kama ilivyoainishwa katika bajeti ya Serikali iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango Juni 13, mwaka huu bungeni Dodoma.

Baada ya kuwasilishwa bajeti hiyo, wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiilalamikia TRA, wamepongeza hatua zilizochukuliwa, lakini wakitoa maoni kuhusu maeneo zaidi ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho.

Katika bajeti hiyo ambayo utekelezaji wake ulianza jana, Dk. Mpango alisema Serikali imeanzisha kitengo kipya cha kupokea malalamiko ya kodi na kitaratibiwa na Wizara ya Fedha na Mipango, kitakachohusisha kupokea malalamiko kutoka kwa walipakodi, yakiwamo ya kuombwa rushwa na watumishi wa TRA.

Katika maeneo nane ambayo yaligusa masilahi ya wafanyabiashara, Dk. Mpango alisema wananchi wataruhusiwa kutoa mizigo yao bandarini bila ulazima wa kutumia mawakala ili kupunguza gharama kwa wananchi, lakini mizigo inayokwenda nje itaendelea kuhudumiwa na wakala.

Alieleza kuwa Serikali imeamua kufuta ada ya matumizi ya maji kwa watumiaji wenye visima nyumbani ambayo ilikuwa inatozwa kuanzia Sh 100,000 na kuendelea kulingana na matumizi ya maji.

Dk. Mpango alisema tozo zote zilizokuwa zinatozwa kwa Dola za Marekani zitatozwa kwa Shilingi ya Tanzania, isipokuwa kwa shehena za kemikali zinazokwenda nje ya nchi.

 “Kufuatia mkutano wa Rais Magufuli na wafanyabiashara uliofanyika Ikulu Dar es Salaam, tumeazimia kufuta ada na tozo 54 zinazotozwa na idara na taasisi za fedha zinazojitegemea ili kuondoa kero kwa wafanyabiashara,” alisema Dk. Mpango.

Alipendekeza kuongeza muda wa leseni ya udereva kutoka miaka mitatu hadi mitano, kuongeza tozo ya leseni kutoka Sh 40,000 hadi Sh 70,000, ada ya usajili wa magari kutoka Sh 10,000 hadi Sh 50,000, bajaji kutoka Sh 10,000 hadi Sh 30,000 na pikipiki kutoka Sh 10,000 hadi Sh 20,000.

Pia aliagiza kufuta kwa msamaha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye taulo za kike kwa kuwa haujawezesha kupatikana kwa bei nafuu kwa bidhaa hiyo muhimu kwa walengwa, badala yake ni kuwanufainisha wafanyabiashara.

Dk. Mpango alisema Serikali itapunguza kiwango cha kodi kwa umeme unaouzwa kutoka Tanzania kwenda Zanzibar kutoka asilimia 18, hadi 0 ili kuwapunguzia gharama za maisha wananchi wa Zanzibar.

Alitoa amri kwa kuwasisitiza watumishi wa TRA kwamba hairuhusiwi kufunga biashara ili kushinikiza mfanyabiashara alipe kodi au malimbikizo ya kodi isipokuwa kwa kibali cha Kamishna Mkuu wa TRA.

Pia alitangaza kuanza kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye nywele za bandia zinazotengenezwa nchini na asilimia 25 kwenye nywele bandia zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali.

MSIMAMO WA TRA

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA,  Richard Kayombo, alisema mamlaka hiyo inaanza vyema mwaka huu wa Serikali, ikiwa imejipanga kusimamia maboresho ya mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

Alisema wamejipanga kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa walipakodi kuhakikisha watu wanaendelea kuhamasika katika kutoa kodi kwa hiyari na kushiriki ujenzi wa uchumi.

“Tumeweka utaratibu mpya wa kuwafikia walipakodi katika maeneo yao kwa mfumo tuliouita vitalu, ambapo wafanyabiashara watatambulika katika maeneo yao maalumu waliopo kupitia mfumo huu.

“Tunatarajia kuweka mazingira rafiki zaidi kwa walipakodi wote, kwa kuzungumza nao na kuwapa nafasi ya kuja wenyewe kujisajili katika mifumo yetu ambayo imerahisishwa zaidi,” alisema.

Alieleza kuwa wameweka mfumo wa kielektroniki kuwezesha wafanyabiashara kujisajili moja kwa moja na kuingia katika kanzidata ya TRA, nia ikiwa ni kufikia mahali wafanyabiashara waone fahari kujisajili na kuwa walipakodi.

Kayombo alieleza kuwa wameweka mfumo huo wa kujisajili ambao wakishajisajili wanapata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) moja kwa moja na waelewe kuwa TIN ni bure kabisa, haichajiwi chochote.

“Sasa hivi wataweza kupata TIN katika ofisi yoyote ya TRA tofauti na zamani ambapo walilazimika kuzifuata katika ofisi maalumu zilizoteuliwa,” alisema.

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa bajeti iliyopitishwa na Bunge, wafanyabiashara wote wapya wanapewa muda wa miezi sita kufanya biashara ndipo wasajiliwe TRA, kwa hiyo hii itawawezesha kulipa kwa uhakika kwa kuwa watakuwa tayari wameshajipanga.

Kayombo alisema jambo jingine ni kuongeza kasi ya matangazo katika maeneo yote, ikiwemo barabarani, mitaani na hata mitandaoni ili kuhakikisha kila mtu anapata ujumbe na hamasa ya kuendelea kushiriki kulipa kodi.

“Tumeweka pia mifumo ya kutoa maoni ambayo tunawaomba wananchi na wafanyabiashara wote waitumie kutoa maoni yao.

“Kuna wale wadaiwa ambao waliingia makubaliano na Serikali, ambao walikuwa wakidaiwa na kupewa miezi sita ya ziada ya kulipa, tutaendelea kuwahamasisha ili waendelee kulipa kodi hizo za malimbikizo ndani ya muda huo, ambao utamalizika Desemba mwaka huu,” alisema.

Alieleza kuwa mawasiliano yao yanaendelea kuwa yale yale, kwa ajili ya kutoa maoni kupitia namba 0800750075, 0800780078, Whatsapp namba 0744233333, email: [email protected] na katika facebook, twitter, instagram, youtube wanapatikana kwa TRA Tanzania.

WAFANYABIASHARA WANENA

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Abdallah Mwinyi, alisema wamepokea vyema mapendekezo yaliyotolewa na Serikali katika bajeti, ambayo yalikuwa na nia ya kusaidia wafanyabiashara.

Alisema wamefurahishwa na namna ambavyo Serikali imeanza kutambua umuhimu wa sekta binafsi katika kuchochea ukuaji uchumi wa nchi na namna ambavyo imeanza kushughulikia kero zilizokuwepo muda mrefu.

“Ni kweli kwamba ukiivuruga sekta binafsi, utakuwa ni mtu usiyetamani maendeleo kwa nchi yako. Tumepokea kwa moyo mkunjufu mabadiliko mema yaliyofanywa katika baadhi ya maeneo,” alisema.

Alisema hata hivyo tozo zilizoondolewa zimelenga sekta binafsi, lakini hazijatatuliwa moja kwa moja kwa kuwa inaonekana Serikali imeanza kutambua tatizo, hivyo kilichofanyika ni sehemu tu ya tiba ya matatizo ya kero zinazowakabili wafanyabiashara na sekta binafsi.

Mwinyi alisema matatizo yote yanayowakabili wafanyabiashara na ambayo wamekuwa wakilalamikia yana vyanzo vikuu viwili, ambavyo maeneo yake ni bandarini na TRA.

“Eneo la kwanza ni kwenye uthaminishaji na uondoshaji wa mizigo bandarini ambalo ndiyo chanzo kikuu cha udanganyifu kwa wafanyabiashara, kutokana na tozo kubwa za kodi,” alisema.

Mwinyi alisema mfumo uliopo unamlazimisha mfanyabiashara kudanganya kwa kuwa iwapo akiwa na mzigo ambao gharama yake ni Sh milioni 200, kodi yake itakuwa kubwa na hataweza kurudisha mtaji wake na kupata faida, kwa hiyo ili mzigo uweze kuuzika kwa bei ya soko la Tanzania wanalazimika kudanganya ili watozwe kodi ndogo.

“Viwango vinavyowekwa hapo bandarini ni vikubwa mno. Lakini pia sheria iliyopo inaruhusu mazungumzo ya pembeni baina ya mfanyabiashara na ofisa wa TRA ambaye anaweza kukadiria na kuamua ni kiasi gani Serikali ipate.

“Ni vyema sheria iamue kabisa kwamba Serikali inataka kiasi gani kwa mzigo wa aina gani na kazi ya ofisa wa TRA iwe kusimamia kupatikana kwa kiasi hicho, kwa kuondoa mamlaka ya ofisa huyo kukadiria,” alisema.

Akitoa ufafanuzi, alieleza kuwa viwango vya kodi za uingizaji magari viko wazi, na kwamba kila gari inayoingia nchini gharama yake ya kodi inajulikana wazi, hivyo ni vyema mfumo huo utumike kuweka wazi gharama za mizigo mingine yote na kuziweka wazi.

Mwinyi alisema eneo jingine ni katika suala la VAT, ambalo kodi hiyo imekuwa ikitoza mara nyingi kwa bidhaa moja na kusababisha kupanda kwa thamani ya bidhaa sokoni.

Alisema kwa kuwa kodi hiyo ni ya ongezeko la thamani, ilitakiwa itozwe pale bidhaa inapotoka kwa mzalishaji, aidha kama imeagizwa kutoka nje, au kutoka kiwanda cha ndani, lakini si katika kila hatua ya mauziano.

“Mimi naweza kuwa nimeagiza mzigo kutoka China, nimetoa kiwandani nimeuingiza nchini, ni sawa nikitozwa VAT. Unapotoka kwenye ghala langu kwenda kwa muuzaji mwingine inatozwa tena VAT. Ikitoka kwenye duka jingine kwenda duka jingine nako unakuta inadaiwa VAT, sasa sijui ni thamani gani inaongezeka hapo,” alisema.

Mwinyi alisema ili kuondoa kero hiyo, ni vyema iwekwe wazi kuwa VAT itozwe viwandani, bandarini, mipakani na kwenye viwanja vya ndege, ila isiwe ndani katika mauziano ambayo hayana ongezeko la thamani.

Aliongeza kuwa ni vyema VAT pia itozwe kwa viwango vidogo vinavyofikia asilimia 12 kwenye huduma za kijamii ikiwamo shule, hoteli na utalii ili kupunguza gharama wanazotozwa wateja na kuvutia watu wengi zaidi kutumia huduma hizo.

Mfanyabishara wa eneo la Kariakoo, Jailo Kisamo, alisema juhudi za Serikali zinastahili kupongezwa kwa kuwa ni hatua nzuri ya kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara, japokuwa si maeneo yote wanayolalamikia yaliyoguswa.

“Tumeona baadhi ya maeneo yameguswa, mimi ninaona ni hatua nzuri. Ninaamini Serikali kwa siku zijazo itaendelea kuangalia maeneo yote tunayolalamikia na itachukua hatua zaidi, hasa kwa hawa maofisa wanaotusumbua wakati wote,” alisema.

Mfanyabiashara mwingine wa Kariakoo, Msafiri Johnson, alisema ni hatua nzuri, lakini TRA wawe tayari kusikiliza kero na ushauri wa wafanyabiashara kwa kuwa ndio waanaoshughulika nao kila siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,195FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles