Magufuli mapumzikoni Chato

0
919
Rais Dk. John Magufuli akishuka kwenye Ndege ya Shirika la Ndege baada ya kuwasili Uwanja Ndege wa Chato mkoani Geita jana.

MWANDISHI WETU-CHATO

RAIS Dk. John Magufuli amewapongeza wananchi wa Wilaya ya Chato mkoani Geita kwa kuitikia wito wa Serikali wa kuongeza juhudi katika kazi za uzalishaji mali, hali iliyoiwezesha wilaya hiyo kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, pongezi hizo alizitoa wakati akiwasalimu wananchi katika eneo la Njiapanda, muda mfupi baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Chato akitokea Dar es Salaam.

Alisema kuwa akiwa angani kabla ya kutua amefurahishwa kuona jinsi wananchi wa Chato walivyochangamka kimaendeleo kwa kujenga nyumba za kuishi za kisasa, majengo ya biashara, majengo ya huduma za jamii na mashamba ya mazao mbalimbali.

“Nawapongeza sana wananchi wa Chato, mnachapa kazi kwelikweli na maendeleo yanaonekana, Chato inabadilika. Nilishasema asiyefanya kazi na asile, kwa hiyo tuendelee kushikamana kufanya kazi na kujenga nchi yetu,” alisema Rais Magufuli.

Alitoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa, kushikamana na kutobaguana ili kwa pamoja waijenge Tanzania ambayo ina rasilimali nyingi.

Kabla ya kuwasalimu wananchi wa Njiapanda, Rais Magufuli alizungumza na kuwashukuru wananchi wanaofanya kazi za ujenzi katika Uwanja wa Ndege wa Chato.

Rais Magufuli aliwasili jana katika Kijiji cha Mlimani wilayani Chato kwa mapumziko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here