29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Madiwani Bariadi waagiza kuondolewa kwa Watendaji Idara ya Biashara

Na Derick Milton, Bariadi

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, wamemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Halid Mbwana kufanya mabadiliko makubwa ya watendaji kwenye Idara ya Biashara kwa kile walichoeleza kuwa hawaridhishwi na utendaji kazi wake.

Madiwani hao wameelekeza hayo kabla ya kikao cha Robo ya Tatu ambacho kitafanyika hivi karibuni, idara hiyo iwe imefanyiwa marekebisho waliyoagiza na katika kikao hicho waletewe taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Lucas Shiminji kwenye kikao cha kupitisha Rasimu ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika leo Ijumaa Februari 11, 2022 ambapo ameagiza idara hiyo ifumuliwe na kupata watendaji wengine wapya.

Shiminji amesema kuwa wao kama madiwani hawako tayari kuona mambo yanakwenda ovyo hasa kwenye idara hiyo ambayo ni tegemeo katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Amesema kuwa idara hiyo imekuwa haitekelezaji vyema majukumu yake hasa ukusanyaji wa ushuru kwenye leseni za biashara, na kueleza kuwa wafanyabiashara wengi wenye maduka wanafanya biashara bila leseni.

Wamesema kuwa katika bajeti, watalaamu walileta makisio ya kukusanya Sh milioni 50, lakini madiwani kupitia kamati ya fedha walikataa na kuongeza kiwango hadi kufikia Sh milioni 100 kiasi ambacho nacho amesema bado ni kidogo.

“Tunakuagiza leo Mkurugenzi, nenda kafanye mabadiliko idara ya Biashara….hatutakubali kuona mambo yanakwenda ovyo, mkiangalia mtaona, mkurugenzi nenda kalifanyie kazi, ikiwezekana vikao vya kawaida vijavyo tupokee hayo mabadiliko tuliyoaagiza,” amesema Mwenyekiti.

Hata hivyo, katika kikao hicho madiwani hao wamepitisha rasimu ya bajeti ya Sh bilioni 30.87, ambapo wamewataka watalaamu kuwekeza zaidi nguvu zao katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Diwani kata ya Dutwa, Mapolo Mukingwa akichangia rasimu hiyo ameshauri kuongezwa nguvu katika ukusanyaji wa ushuru wa stendi ambazo sipo kwenye halmashuari kwani mapato mengi yanapotea.

Awali, akiwasilisha rasimu hiyo ya bajeti Afisa Mipango, Regina Shashi amesema kuwa bajeti hiyo imezingatia vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuwezesha wananchi kiuchumi, pamoja na kuhakikisha stahiki na motisha kwa watumishi na madiwani zinapatikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles