28.4 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

Madini ya Kinywe kuwanufaisha wananchi Lindi, Waziri Biteko awataka kutoa ushirikiano

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko na Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, Nape Nauye (CCM) wamesema mradi mpya wa uchimbaji madini ya Kinywe katika Kijiji cha Namangale mkoani humo utaufungua mkoa huo kiuchumi kwa kuongeza ajira na kuchochea maendeleo kwa wananchi wa kijiji hicho.

Wametoa kauli hizo Juni 18, 2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Namangale mkoani Lindi, huku Waziri Biteko akiwataka wananchi wa kijiji hicho kilichopo Halmashauri ya Mji wa Mtama kutoa ushirikiano kwa mwekezaji wa Madini ya Kinywe Volt Resources Limited ili aweze kulipa fidia kwenye maeneo yatakayo jengwa mgodi.

Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye ambaye pia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akizungumza kwenye mkutano huo.

Waziri huyo amesema Kampuni ya Volt Resources Limited kutoka nchini Australia itakayochimba madini hayo inatarajiwa kuwekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 40 katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa mgodi huo ambapo inakadiriwa kuwa na hifadhi ya zaidi ya tani milioni 461 za madini ya Kinywe katika kijiji cha Namangale Mkoani Lindi.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ambaye ni Mbunge wa jimbo la Mtama, ameiomba Wizara ya Madini kuisimamia kwa karibu Kampuni ya Volt Resources Limited ili kuhakikisha mradi wa uchimbaji wa madini ya Kinywe katika kijiji cha Namangale unaharakishwa ili wananchi wa Mkoa wa Lindi wapate ajira.

Nauye amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameufungua mkoa wa Lindi ambapo kwa sasa Taifa linashuhudia miradi mingi ya maendeleo ikifanyika mkoani humo ukiwemo mradi wa uchimbaji madini ya Kinywe unaotarajiwa kujengwa katika kijiji cha Namangale.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Namangale mkoani Lindi waliohudhuria mkutano huo wa hadhara.

Katika ziara hiyo, Waziri Biteko ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kuhakikisha mradi huo unaanza kulipa fidia wananchi ili uanze uzalishaji kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles