30.5 C
Dar es Salaam
Sunday, May 12, 2024

Contact us: [email protected]

Wawekezaji wa viwanda waaswa kuzingatia sheria na miongozo ya kazi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wawekezaji wa Sekta ya Viwanda wametakiwa kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali ya kazi nchini ikiwemo kuboresha mifumo ya usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi ili kuwalinda wafanyakazi dhidi ya athari wanazoweza kuzipata wakiwa kazini.

Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii (hawapo pichani) katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambapo kilifanyika kikao kifupi kabla ya kuanza ziara ya kutembelea viwanda Mkoani humo.

Wito huo umetolewa Juni 19, mwaka huu na Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maenedeleo ya Jamii ya kutembelea viwanda Mkoani Arusha akiambatana na  kamati hiyo ili kujionea utekelezaji wa sheria na miongozi mbalimbali ya kazi ikiwemo Sheria Na.5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003.

“Kwanza kabisa tunapenda wawekezaji waje nchini kwa wingi na wanapowekeza basi waendeshe shughuli zao zote kwa kuzingatia sheria mbalimbali za nchi ikiwemo sheria na miongozo mbalimbali ya kazi, huwa tunafurahi sana tunapoona wawekezaji wanatengeneza ajira kwa vijana wetu lakini pia wakiendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria za nchi,” amesema Prof. Ndalichako. 

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Manendeleo ya Jamii, Riziki Saidi Lulida amewataka wawekezaji hao kuhakikisha wanaweka miundo mbinu rafiki katika maeneo mbalimbali ya viwanda vyao kwa watu wenye ulemavu.

“Tunazo sheria za nchi zinazoelekeza viwanda kujenga miundo mbinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, kwa mfano mimi leo nimeshindwa kuingia ndani katika baadhi ya viwanda tulivyotembelea kutokataka na ulemavu wangu wa miguu kwasababu maeneo mengi yana ngazi, naamini kuna wafanyabishara wengi wenye ulemavu ambao pengine wanatamani kuingia katika maeneo ya viwanda na wakashindwa kutokana na miundombinu kutokuwa rafiki kwao hivyo wito wangu kwa wawekezaji wote nchini katika sekta hii ya viwanda waboreshe miundommbinu ili kuwapa fursa wenye ulemavu,” amesema Lulinda.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamiii, Fatma Hassan Toufiq pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wakipata maelekezo kwa muwakilishi wa kiwanda cha kutengeneza transfoma cha TANALEC Limited kuhusu hatua mbalimbali za uzalishaji wa bidhaa zao.

Naye Mjumbe wa Kamati hiyo na Mbunge wa Jimbo la Jang’ombe, Ali Hassan King ameishauri taasisi ya OSHA kuendelea kuimairisha mifumo ya usimamizi wa usalama na afya katika ameneo ya kazi nchini huku akiahidi kuwa wataendelea kuishauri serikali juu ya uimarishaji wa mifumo ya usalama na afya katika viwanda.

“Kupitia ziara hii tumepata mengi ya kujifunza na kuishauri serikali na katika maeneo yote tuliyotembelea kwa kiasi kikubwa tumeridhishwa na hali ya utekelezaji wa sheria na miongozo ya usalama na afya na kuna mambo mbalimbali tumehoji katika viwanda hivi na tumewaelekeza kutoa majibu kwa kuandikia taarifa nasisi tutaiandikia ripoti ili kuiwasilisha bungeni kwa lengo la kuishauri serikali” alisema Mhe. Ally Hassan

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi wa OSHA, Dk. Jerome Materu amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa sana kwa wawekezaji wote kuzingatia taratibu na miongozo yote ya usalama na afya kwasababu huongeza tija na kupunguza gharama za uendeshaji wa maeneo yao ya kazi.

“Unapowekeza katika masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kuna mahusiano makubwa kati ya upunguzaji wa gharama na uendeshaji wa eneo la kazi hivyo tunaishukuru sana Kamati hii ya Bunge kwasababu na wao wamekuwa ni jicho la tatu katika kuangalia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi na wametupatia ushauri ambao tutautumia katika kuboresha usimamizi wa mifumo ya usalama na afya katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini,” amesema Dk. Materu

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamiii, Fatma Hassan Toufiq (wa kwanza kulia) pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wakimsikiliza Mkurugenzi wa Usalama na Afya wa OSHA, Dk. Jerome Materu (wakwanza kushoto) alipokuwa akijibu hoja inayohusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi iliyoibuliwa na wawekezaji wa kiwanda cha Fides Tanzania.

Aidha, wawakilishi wa viwanda vilivyotembelewa wameishukuru kamati hiyo kubainisha kuwa ziara hiyo imewapa funzo kubwa huku wakiahidi kuendelea   kuboresha zaidi mifumo ya usimamizi ya usalama na afya mahali pa kazi.

Katika Ziara hiyo Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendelea ya Jamii imetembelea viwanda vitatu Mkoani Arusha ambavyo ni: Kiwanda cha kuzalisha Transifoma cha TANELEC Limited, Kiwanda cha kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo nguo cha A to Z Textiles Mills Ltd pamoja na kiwanda cha maua cha Fides Tanzania. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles