28.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

Machinga kutengenezewa toroli za kisasa

JacobVeronica Romwald na Herieth Faustine, Dar es Salaam

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imesema ipo katika mchakato wa kutengeneza vibanda vya kisasa (vitoroli) kwa ajili ya wafanyabiashara wamachinga  kuwaondolea adha ya kupanga bidhaa zao chini.

Kauli hiyo ilitolewa   Dar es Salaam jana na Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob (Chadema) alipozungumza na wafanyabiashara aliowatembelea,   Kimara Mwisho na Mwenge.

Alisema vitoroli hivyo maalum vya kisasa  vitakuwa vikijifunga na kujifungua huku   vikiwa na sehemu ya kuwekea mwavuli wa kujikinga mvua, sehemu ya kuwekea bidhaa na baadaye   jioni kuvihifadhi.

Ili kumudu gharama hizo, meya huyo alisema manispaa itachangia nusu ya bei na mfanyabiashara atalazimika kulipia nusu iliyobaki.

“Tupo kwenye mchakato wa kutengeneza vitoroli hivyo na tayari tumealika wataalam kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM  watupatie mawazo ya namna vitakavyokuwa.

“Tunataka viwe vya kisasa, mtu aweze kukisukuma hadi eneo lake la kufanyia biashara, aweze kukifungua sehemu ya juu ili asipigwe na jua, apange bidhaa zake katika hali ya usafi lakini pia asichafue mazingira,” alisema Jacob.

Alisema pamoja na kukutana na wataalam hao wa SIDO na UDSM,   Manispaa inawaalika wafanyabiashara hao kupeleka mawazo yao  waweze kuboresha mradi huo.

“Jana nilikuwa safarini nikajulishwa kwamba wanataka kuja kuwaondoa kwa kutumia polisi hususan waliopanga bidhaa kwenye barabara za Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (DART) nikawasihi wasifanye hivyo ili nije kuzungumza nanyi.

“Wakati wa kampeni   mgombea wetu, Edward Lowassa aliahidi kwamba serikali itakayoundwa na Ukawa itakuwa rafiki wa wafanyabiashara ndogondogo, ingawa alishinda Rais John Magufuli bado tutaendeleza ahadi yetu ile.

“Jambo zuri ni kwamba Rais Magufuli naye ameahidi kwamba serikali yake itakuwa rafiki wa wafanyabiashara ndogondogo hivyo yeyote atakayewabughudhi nitamshtaki kwa kumuandikia barua Rais Magufuli   amchukulie hatua,” alisema.

Aliwataka wafanyabiashara hao kupanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara bila kusababisha bughudha kwa watembea kwa miguu.

Kauli hiyo ya Meya Jacob ilipokelewa kwa vifijo na nderemo na wafanyabiashara hao ambao walisikika wakisema wanamuombea kwa Mungu aishi maisha marefu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles