29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, October 21, 2021

MAALIM SEIF AFANYA ZIARA KIMYA KIMYA DAR

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amefanya ziara kimya kimya jijini Dar es Salaam, kwa kutembelea wagonjwa na kutoa pole kwa wafiwa wa chama hicho.

Ziara hiyo aliifanya jana huku akiwa ameongozana na baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwamo Mbunge wa Temeke, Abdalah Mtolea (CUF), Naibu Meya wa Jiji, Mussa Kafana na Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Omar Kumbilamoto.

Katibu mkuu huyo alifanya ziara hiyo katika kata za Gongolamboto, Majohe, Kigamboni na Upanga, ambapo alizungumza na wananchi mbalimbali aliowakuta katika maeneo husika kwa kuwataka kuwa watulivu, huku akiahidi changamoto zinazokikabili chama hicho zitamalizika hivi karibuni.

Mbali na hilo pia aliwaahidi wanachama wa chama hicho kujiandaa kuchukua ofisi yao Buguruni muda wowote kuanzia sasa kwani wamefikia katika hatua nzuri.

Akizungumza na MTANZANIA jana Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari Mahusiano na Umma, Mbarara Maharagande, alisema ziara ya kukagua uhai wa chama na kufungua matawi jijini Dar es Salaam ipo kama ilivyopangwa na tarehe husika itatangazwa kwa umma.

“Hii ni ziara ya kawaida na inalengo la kuwatembelea wanachama wetu ambao walipatwa na matatizo mbalimbali ikiwemo maradhi na hata wengine kufiwa. Kwa hiyo Katibu Mkuu alikwenda kuwapa mkono wa pole jambo ambalo ni kawaida kwa binadamu yeyote na kama unavyofahamu Maalim Seif ni kiongozi wa watu na siku zote amekuwa akiishi uungwana huo,” alisema Maharagande.

Ziara hiyo ya kimya kimya imekuja siku chache baada ya Jeshi la Polisi kuzuia wanachama wa chama hicho, waliokuwa wamehamasishwa na Mbunge wa Temeke kwenda kufanya usafi katika ofisi za CUF Buguruni, Aprili 30, mwaka huu.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilimzuia kwa Maalim Seif na wafuasi wake kufanya hivyo kwa maana ya kuweza kuhatarisha amani kwa wananchi iliyopo.

Juzi waaliodaiwa wafuasi wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba walimdhibiti mtu mmoja ambaye walidai ni wa upande wa Maalim Seif aliyefika katika ofisi hiyo kwa ajili ya kufanya usafi.

“Sisi tulishazuiwa kufanya hivyo na tulikuwa tunajipanga kwa ajili ya kufanya ziara katika tarehe nyingine hao waliofika katika eneo hilo watakuwa wametumwa na wametengenezwa ,” alisema Maharagande.

Hivi karibuni wafuasi wa Profesa Lipumba walivamia Hotel ya Vina iliyopo Mabibo Wilaya ya Ubungo na kuzua vurugu zilizosababisha waandishi wa habari kupigwa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,682FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles