26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI AWAGEUKIA  WALIODANGANYA UMRI

*atangaza vita dhidi yao kuanzia sasa

*Aahidi nyongeza ya mishahara mwakani


UPENDO MOSHA NA SAFINA SARWATTI – MOSHI

RAIS Dk. John Magufuli, amesema baada ya kukamilika kwa kazi ya uhakiki kwa watumishi wa Serikali walioghushi vyeti, sasa anawageukia waliodanganya umri wa kustaafu kwa wakati.

Pia amesema Serikali yake imepanga kupandisha nyongeza ya mishahara ambayo ilisimama kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na promosheni kwa watumishi wa umma.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa alipokuwa akihutubia katika kilele cha Sikukuu ya Wafanyakazi Mei Mosi.

Rais Magufuli alisema katika taasisi mbalimbali za umma kumekuwa na baadhi ya watumishi ambao kwa mwonekano wana umri mkubwa na wanatakiwa wawe wameshastaafu ili kupisha watu wengine wenye sifa wakiwemo wasiokuwa na ajira.

Alisema pamoja na kuwa na umri mkubwa, bado watumishi hao wamekuwa wakiendelea kufanya kazi kwa muda mrefu hali ya kuwa siku zao za utumishi zimekwisha.

“Wapo watumishi ambao wamekuwa wakidanganya umri wa kustaafu ili waendelee kufanya kazi kwa muda mrefu kwa kuwa siku zao zimekwisha,” alisema Rais Magufuli.

Akizungumzia mishahara ya watumishi, alisema kuwa Serikali haijaiongeza kwa sababu ya watumishi hewa, huku akiahidi mambo kuwa mazuri mwakani.

Aidha Rais Magufuli alisema uamuzi wa Serikali kuanza kutoa promosheni, unatokana na kukamilika kwa kazi ya uhakiki wa wafanyakazi, ambapo zaidi ya 19,000 walibainika kuwa ni hewa.

“Yale mambo yote yaliyokuwa pending (yaliyoachwa), ikiwa ni pamoja na promosheni, ni kwa sababu tulishindwa. Unaweza kupromoti mfanyakazi hewa hayupo, kwa sababu tungetoa promosheni wakati kuna wafanyakazi 19,000 hewa, maana yake tungepromoti na hao 19,000 na si ajabu na watu waliowaandika mle, ndio wangeletwa katika mapendekezo ya promosheni,” alisema.

Rais Magufuli alisema kuwa watumishi hewa waliobainika, waliisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 19.9 kwa mwezi ambayo kwa mwaka ingekuwa ni zaidi ya Sh bilioni 230.

Alisema Serikali haina nia mbaya na watumishi, na walioghushi vyeti wanaongoza ni watoto wa vigogo.

 

AJIRA MPYA

Rais Magufuli, ametangaza neema za ajira mpya 52,000 katika sekta mbalimbali za umma kwa Watanzania wenye sifa kwa mujibu wa sheria.

“Kukamilika kwa uhakiki wa watumishi hewa, kumeisaidia Serikali kujua kwamba kuna upungufu wa kiasi gani wa watumishi, sasa nasema tutaajiri wafanyakazi wapya 52,000,” alisema.

Akizungumzia changamoto za wafanyakazi nchini Rais Magufuli alisema baadhi zimekwisha fanyiwa kazi na Serikali.

Alisema Tanzania ilikuwa sehemu ya kutupa takataka na baadhi ya mambo mabaya yaliyokuwa yakiendelea, wengi wanaohusika ni vigogo wakubwa wa juu serikalini.

 

MADENI

Akieleza madeni ya walimu, alisema hadi sasa yaliyolipwa na Serikali ni ya Sh bilioni 14.23, ikiwemo mishahara Sh bilioni 42.48.

Alisema madeni ya utekelezaji wa miradi yaliyolipwa ni Sh trilioni 3.68. Kati ya hizo, Sh trilioni 1.7 ni deni la wakandarasi wa barabara na Sh bilion 80 zimelipwa kwa wazabuni wanaotoa huduma sehemu mbalimbali, ikiwamo magereza.

BIMA YA AJIRA YAJA

Rais Magufuli, alisema kwa sasa Serikali inaendelea na mchakato wa kuanzisha bima ya ajira kwa lengo la kuwawezesha wafanyakazi kulipwa sehemu ya michango yao pindi watakapoachishwa kazi na waajiri wao.

“Utaratibu wa kaanzishwa kwa bima hiyo unaendelea vizuri, wadau na waajiri wamekwisha kutoa maoni yao na nimearifiwa kuwa muswada wa kuanzishwa kwa fao hilo utapelekwa bungeni na Bunge likipitisha nitasaini siku hiyo hiyo,” alisema.

Rais Magufuli pia aliwataka wafanyakazi kutokubali kuhamishwa katika sehemu zao za kazi kabla ya kulipwa posho za uhamisho ili kutatua changamoto ya kudai posho hizo ambazo zimekuwa ni kero sugu.

Alisema kuhusu mifuko ya hifadhi ya jamii, Serikali itahakikisha inapunguza utitiri wa mifuko hiyo na kubaki miwili kwa lengo la kupunguza gharama za undeshaji ikiwa ni pamoja na kulinda masilahi ya wafanyakazi.

Mbali na hilo, alisema Serikali itashughulikia changamoto ya  wafanyakazi ya uchelewashwaji wa mafao na kwamba suala hilo limekuwa likisababishwa na waajiri kuchelewa kuwasilisha michango ya watumishi.

“Suala hili limekuwa likiwakwaza wafanyakazi, lakini pia nipende kusema ukweli kuwa sisi Serikali tumekuwa ni tatizo katika uwasilishaji wa michango yenu.

“Lakini sasa tumejirekebisha na tumetubu, kwani nilipokuwa naingia madarakani Serikali ilikuwa ina deni la Sh trilioni 1.5 na sasa tumeshalipa Sh trilioni 1.25… naahidi tutakamilisha lengo,” alisema.

Rais Magufuli alisema mfanyakazi ana uhuru kisheria wa kujiunga katika chama chochote cha wafanyakazi na kwamba hakuna mwajiri aliye juu ya sheria katika suala hilo.

Aliongeza kuwa suala la mikataba ya ajira ni la lazima kwa wafanyakazi na kwamba Serikali haitaendelea kuwafumbia macho waajiri ambao hawatoi mikataba ya ajira.

 

MFUMUKO WA BEI

Kuhusu suala la mfumuko wa bei wa bidhaa mbalimbali, Rais Magufuli, alisema Serikali itashughulikia changamoto hiyo ili kupunguza ugumu wa maisha kwa wafanyakazi na Watanzania kwa ujumla.

“Mfumuko wa bei wakati naingia madarakani ulikuwa asilimia saba na ukashuka mpaka asilimia 4.5 na baadae baada ya ukame mfumuko umepanda hadi kufikia asilimia 60, lakini naamini utashuka,” alisema.

 

MIKOPO ELIMU YA JUU

Rais Magufuli alisema tangu utaratibu wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu uanze mwaka 1994 hadi 1995, Serikali tayari imekwisha toa Sh trilioni 2.9 ambazo zimeiva na kwamba mikopo yote ina thamani ya Sh trilioni 7.

Alisema mikopo ambayo ilipaswa kurejeshwa ni Sh bilioni 425 na kwamba kati ya hizo zilizorejeshwa ni Sh bilioni 141.4 .

“Wapo watu walionufaika na mikopo hii, lakini hawataki kurejesha na wakati tunaendelea kusomesha watoto wengine, sasa hivi tumeongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo kutoka 98,000 hadi kufikia 172,000 na ndiyo maana katika bajeti ya mwaka huu tumetenga Sh bilioni 483,” alisema.

 

NDEGE, UJENZI WA RELI

Alisema Serikali hadi sasa imekwisha nunua ndege sita kwa lengo la kuisaidia Tanzania kukua kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya utalii.

“Tunaponunua ndege maana yake ni kwamba tunawasaidia Watanzania wote na tunapojenga reli lengo ni hilo la kukuza na kuinua uchumi wetu, ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira,” alisema.

 

ELIMU BURE

Rais Magufuli alisema kila mwezi Serikali imekuwa ikitoa zaidi ya Sh bilioni 18 ambazo zimekuwa zikielekezwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari kwa lengo la kutekeleza dhana ya elimu bure kwa Watanzania.

“Haya tunayoyafanya kwenye Serikali tunayafanya kwa nia njema ili kuhakikisha Tanzania yetu tunaipeleka mbele,  mpaka sasa tumeongeza bajeti yetu ya maendeleo kutoka asilimia 29 hadi asilimia 40 na ya afya na ada ya kununulia madawa kutoka Sh bilioni 31 hadi bilioni 250, lengo letu ni hilo hilo kuboresha maisha ya Watanzania,” alisema Rais Magufuli.

 

WAZIRI WA KAZI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema wataendelea kufanya vikao mbalimbali na vyama vya wafanyakazi, kuhakikisha Serikali inatekeleza wajibu wake katika kutatua kero za wafanyakazi.

“Tutaendelea kutii agizo lako na hatutaacha utaratibu mzuri tuliouanza wa mazungumzo ya utatu baina yetu na Tucta na chama cha waajiri,” alisema Mhagama.

Pia alisema wataendelea kusimamia sheria zilizopo nchini ambazo zinaelekeza kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu na nia njema ya Serikali katika kujenga uchumi wa viwanda.

“Tutaendelea kusimamia sheria mbalimbali, zikiwamo sheria ya ajira na mahusiano kazini, sheria ya taasisi za kazi, sheria inayoratibu ajira za wageni, sheria ya huduma za ajira, sheria ya fidia kwa wafanyakazi.

“Sheria ya kusimamia na kudhibiti mifuko ya hifadhi ya jamii, sheria ya utumishi wa umma na sheria zingine zote ambatanishi ambazo mwisho wa siku zitaifanya kaulimbiu ya mwaka huu iweze kutekelezeka,” alisema.

 

RAIS TUCTA

Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi (Tucta), Tumaini Nyamhokya, alimwomba Rais Magufuli kuendelea kuvifanyia kazi vilio vya watumishi wa umma.

“Hivi karibuni ulitukaribisha Ikulu na tukazungumza kuhusu matatizo yanayowasibu wafanyakazi wa nchi hii, tuliongea mengi zaidi ya saa tatu. Tunaomba tukija tena utusikilize, utupe ushirikiano na vilio vya watumishi uvisikilize,” alisema Nyamhokya.

Alisema walipokutana aliwaahidi kushughulikia masuala kadhaa, yakiwamo kupandishwa madaraja kwa wafanyakazi na suala la nyongeza ya mwaka kwa watumishi, ambayo ilisimama kwa muda mrefu.

 

SPIKA WA BUNGE

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema watahakikisha haki zote za wafanyakazi zinapatikana kupitia sheria mbalimbali zitakazotungwa.

“Tumepokea maelekezo, tutayafanyia kazi kwa wakati na mambo yenu yataenda vizuri,” alisema Ndugai.

 

WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema watasimamia kwa dhati wakurugenzi wote wa halmashauri na makatibu wakuu, ili wazingatie maagizo yaliyotolewa ya kutowahamisha watumishi bila kuwalipa stahiki zao.

“Maelekezo yako yote tutayasimamia kwa kina, wafanyakazi endeleeni kuwa na imani na Serikali ya Awamu ya Tano,” alisema Majaliwa.

 

MWENYEKITI WA BUNGE

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ambaye pia ni Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu (CCM), alisema watasimamia kwa umakini sheria zote zitakazopelekwa bungeni, zinazohusu masuala ya wafanyakazi.

 

RC KILIMANJARO

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Meck Sadiki, alimwomba Rais Magufuli kufufua viwanda vilivyokufa mkoani humo ili kutoa fursa za ajira kwa wananchi wake.

“Kulikuwa na viwanda vingi vinavyotoa ajira zaidi ya 10,000, lakini sasa vimekufa havifanyi kazi. Kibo Match (kiwanda cha kutengeneza viberiti na karatasi) ameuziwa mtu kutoka Nigeria, lakini ni mwaka wa nne sasa hakuna kinachofanyika.

“Kiwanda kingine ni kile cha kutengeneza magunia… tunaomba viwanda hivi vifufuliwe haraka na vingine vijengwe vipya,” alisema Sadiki.

 

KATIBU MKUU TUCTA

Katibu Mkuu Tucta, Yahya Msigwa, alilaani baadhi ya viongozi kujichukulia madaraka makubwa kwa kuwaweka ndani viongozi bila kufuata utaratibu jambo ambalo alieleza kuwavunja moyo wafanyakazi.

Alizungumzia pia suala la viwango vya mishahara kuwa vidogo kwa wafanyakazi kiasi cha kwamba kinashindwa kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Lakini pia aliishukuru mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa ya umma na binafsi, huku akihitaji kuwapo na uboreshwaji wa vikokotoo vimsaidie mtu anapostaafu.

Alisema suala la fao la kujitoa pia linatakiwa kuwekwa sawa ili Watanzania wengi waweze kunufaika na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Nyongeza ya habari imeandaliwa na Asha Bani na Nora Damian (Dar)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles