26.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 26, 2022

JPM ATISHIA KUZIFUTA HALMASHAURI, MANISPAA

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli ametishia kuivunja halmashauri yoyote itakayotishia kumfukuza kazi mkurugenzi aliyemteua.

Alisema hayo juzi Ikulu ndogo ya mjini Moshi, alipokuwa akielezea tatizo la ofisa wa ardhi wa halmashauri hiyo, ambaye anadaiwa kuzungusha wananchi kutoa vibali vya ardhi.

Dk. Magufuli alisema kama mkurugenzi ataamua kumfukuza mtu na madiwani wakaendelea kumng’ang’ania, huku wakitishia kumsimamisha kazi, basi atalivunja baraza zima la madiwani.

“Kama ofisa wa ardhi analalamikiwa kwa kushindwa kutoa vibali, huku mkurugenzi akiwa na mamlaka ya kumfukuza kwa mujibu wa sheria namba 3, kwa nini aendelee kuwa hapo?

 “Wakurugenzi wengine mkitaka kuchukua maamuzi madiwani wanatishia, chukueni maamuzi ya kuwasaidia Watanzania na kama likitokea Baraza la Madiwani linataka kumsimamisha mkurugenzi niliyemteua mimi, nalivunja baraza hilo.

“Kama nilikuteua mimi nani wa kukufukuza? Mimi nazungumza ukweli na hiyo ndiyo ‘principle’ (utaratibu) yangu. Na ninyi ni lazima kuendelea kuwatumikia wananchi,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliponda Halmashauri ya Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na hatua ya kuipa tenda kampuni ya kukusanya ushuru wa maegesho ya nchini Kenya (KAPS).

Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Moshi na ile ya Dar es Salaam zote zinaongozwa na vyama vinavyounda Ukawa.

“Mimi hawa Parking System wanajisahau, wanashindwa kuheshimu watu wa umri mkubwa, utakuta hata sheikh au mchungaji au mzee anasimama kidogo wanakuja wanafunga gari yake bila kuwa na utaratibu, huo ni ushetani, wanashindwa kuheshimu utu wa Watanzania.

“Kitendo cha kuweka makampuni ya nje kukusanya fedha za parking ni uroho wa pesa usiojali utu na masilahi ya Watanzania,” alisema Rais Magufuli.

Wakati Rais Magufuli akichukizwa na hatua hiyo ya kupewa tenda kampuni ya kigeni, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, aliusifia mfumo wa ukusanyaji fedha za maegesho wa kampuni hiyo.

Alisema wakati ushuru huo unakusanywa na Watanzania, makusanyo yalikuwa kati ya Sh milioni 380 hadi 420, lakini kwa sasa yamepanda hadi kufikia Sh milioni 500.

Hata hivyo, wakazi wa Dar es Salaam walilalamikia kiwango cha ushuru wa maegesho kutoka Sh 300 hadi 500.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
176,803FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles