30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

MAAJABU YA MAGADI SODA MBALI NA KUTUMIKA KUPIKIA

Na MWANDISHI WETU


magadi-sodaMAGADI soda (Baking soda/Bicarbonate of soda), ni hitaji la kawaida kabisa jikoni, hutumika katika vyakula vya kuoka kama keki na mikate pia hutumika katika maandazi, chapati na vyakula vingine vingi.

Magadi soda wakati mwingine hutumika kulainisha vyakula ambavyo ni vigumu kuiva au visivyolainika haraka vinapopikwa kama mahindi yasiyokobolewa, mboga za majani za kienyeji kama mgagani, msusa na majani ya kunde yaliyokomaa. Hapa nchini Baking soda inayofahamika zaidi ni ile inayoitwa Simba.

Hupatikana kwa wingi madukani na hata sokoni, kuna ile ambayo imepita kiwandani na kusindikwa kitaalamu na ile ya kienyeji ambayo iko kiasili zaidi. Siri kubwa ambayo wengi hawaijui kuhusu magadi soda, ni ambavyo huweza kutumika kufanya shughuli nyingi za usafi. Uwepo wa alkalini ndani yake huipa uwezo wa kuondoa uchafu wenye asili ya asidi.

Kusafisha kibao cha kukatia nyama au mboga

Kwa wale mnaotumia kibao cha plastiki au mbao kukata nyama mnajua ambavyo hushika uchafu na hata kubadilika rangi, hata baada ya kukiosha. Kutatua tatizo hilo na kufanya kibao chako kiwe safi na cheupe tena, nyunyuzia baking soda ya kutosha kisha sugua na dodoki hadi kiwe safi, kama ni uchafu wa muda mrefu loanisha kibao na maji kisha nyunyuzi magadi soda na uache kwa dakika 15 ndipo usugue na dodoki
Kuzibua sinki la jikoni
Sinki la jikoni mara nyingi huziba na kugoma kupitisha maji machafu kwa sababu ya mafuta na uchafu wa chakula. Mwaga kikombe kimoja cha magadi soda kwenye tundu la sinki, kisha mwaga vikombe vitatu vya maji ya moto. Acha kwa angalau saa nne kabla hujatumia sinki. Ni vyema ukafanya hivyo usiku unapokwenda kulala ili lisitumike hadi asubuhi.
Kukata harufu ya mkojo chooni
Kama unasafisha choo lakini bado kuna harufu mbaya ya mkojo. Chukua nusu kikombe cha magadi soda changanya na nusu kikombe cha vinegar nyeupe kisha mwaga ndani ya choo na unyunyuze kwenye sakafu… baada ya nusu saa unaweza kudeki sakafu ili pabaki safi.
Kusafisha na kung’arisha sinki na malumalu
Ingawa wengi hupenda kuweka malumalu na masinki kwenye nyumba zao, hawajui namna ya kuzifanyia usafi, unakuta sinki au malumalu nyeupe zimebadilika rangi na kuwa za njano kwa uchafu. Chukua nusu kikombe cha magadi soda changanya na nusu kikombe cha sabuni ya maji changanya vizuri ili kupata kama uji mzito. Kisha tumia
kusugua sinki au malumalu zako.
Kusafisha oven
Kawaida unapooka vyakula kama nyama, samaki, mboga za majani na matunda kama nanasi, mchuzi au umajimaji kutoka kwenye vyakula hivi humwagika ndani ya oven. Wakati mwingine unapounga mchuzi, mafuta huruka na kuchafua oven.

Kwa Uchafu wa aina hii huganda haraka mno. Ili kusafisha, weka magadi soda ya kutosha kwenye sehemu ya chini kabisa ya oven, kisha iloanishe na maji, usiweke maji mengi bali kiasi cha kutosha kuloanisha magadi soda. Fanya hivi usiku kabla yakulala na ifikapo asubuhi uchafu wote ulioganda utakuwa umelainika, tumia dodoki kusafisha.
Kuondoa harufu mbaya ndani ya friji
Kutokana na uwekaji wa vyakula vya aina mbalimbali vyenye harufu tofauti tofauti, mara nyingi friji huwa
na harufu isiyoeleweka.

Chukua boksi la magadi soda, lifungue na kisha fungua mfuko wa plastiki wenye baking soda ili ukae wazi, kisha iweke kwenye sehemu ya chini ya friji yako, itanyonya harufu yote ndani ya friji na kuiacha ikiwa safi.

Ukiweka boksi lenye baking soda kidogo utendaji wake huwa wa taratibu mno, hivyo ni vyema ukaweka boksi
jipya.
Kukata harufu kwenye nguo mpya
Mara nyingi unaponunua nguo mpya inakuwa na harufu ya upya, ndiyo maana watu wengi huzifuakabla ya kuzivaa. Nguo za mtumba nazo huwa na harufu kali inayolazimu kufua kabla haijavaliwa, hizi zote ni harufu za kemikali zilizotumika katika utengenezaji wake, na kwa nguo za mitumba ni harufu ya dawa zenye kemikali zinazotumika kuhifadhi nguo.

Ili kuondoa harufu hizo, pima kikombe kimoja cha magadi soda changanya kwenye maji lita tano, kisha loweka nguo kwenye maji hayo kwa saa tatu au zaidi, baada ya hapo suuza na uanike.

Mbali na matumizi hayo magadi soda pia husaidia kung’arisha meno, kusafisha kucha na hata kuondoa chunusi usoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles