30.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA YATOA KIPIGO KWA NDANDA, MTIBWA YAPETA

Na THERESIA GASPAR-DAR ES SALAAM


 

pg-32MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jana walirejesha furaha kwa mashabiki wao baada ya kuifanyia mauaji timu ya Ndanda FC ya Mtwara na kuchomoza na ushindi mnono wa mabao 4-0.

Yanga waliokuwa wenyeji wa mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, walipania kulipiza kisasi baada ya wapinzani wao kuwabana na kutoka sare ya bila kufungana walipokutana katika mzunguko wa kwanza wa ligi.

Matokeo ya ushindi wa jana yameiongezea kasi Yanga na kufanikiwa kupunguza tofauti ya pointi kati yao na vinara wanaoongoza katika msimamo wa ligi hiyo, kwa kufikisha pointi 40 huku Simba wakiwa wamejikusanyia pointi 41.

Ushindi wa jana ni wa pili kwa kikosi cha Wanajangwani hao kikiwa chini ya kocha wao mpya Mzambia, George Lwandamina, ambaye alikiongoza walipotoa kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya JKT Ruvu kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 na African Lyon.

Mshambuliaji Donald Ngoma aliyerejea uwanjani kwa kasi baada ya kukosa mchezo uliopita, aliwanyanyua mashabiki wa Yanga dakika ya nne ya mchezo baada ya kufunga bao la kuongoza kwa kichwa akiunganisha vyema mpira wa kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima.

Dakika ya 20, Amissi Tambwe, alikuwa katika nafasi nzuri ya kuifungia timu yake bao la pili lakini shuti alilopiga akiwa nje ya eneo la hatari baada ya kupokea pasi ya Emmanuel Martin lilipaa juu ya lango.

Ngoma aliyeingia uwanjani akiwa na uchu wa kusaka mabao, aliandika bao la pili kwa timu yake katika dakika ya 21 baada ya kupokea pasi ya Martin ambaye alionyesha makali ndani ya kikosi cha Yanga baada ya kusajiliwa kwenye dirisha dogo.

Ngoma alifunga bao hilo baada ya kuachia shuti kali akiwa ndani ya eneo la 18 ambalo lilipitiliza moja kwa moja langoni mwa Ndanda baada ya kipa kuhama kwenye eneo lake.

Dakika ya 25, Tambwe alifanikiwa kufunga bao lake ya tisa msimu huu na kulingana na Simon Msuva na Shiza Kichuya wa Simba, baada ya kuwapiga chenga mabeki wa Ndanda na kuambaa na mpira hadi kwenye eneo la hatari na kuachia shuti lililotinga moja kwa moja nyavuni.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Salum Telele, nusura aipatie Ndanda bao la kuongoza dakika ya 35 baada ya kuambaa na mpira hadi katika eneo la hatari, lakini hesabu zake ziligonga mwamba baada ya kipa Deogratius Munishi kuuwahi mpira na kuokoa hatari hiyo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Ndanda kufanya shambulizi la kushtukiza dakika ya 58 kupitia kwa Right Hamis, lakini shuti alilopiga lilidakwa na kipa wa Yanga.

Yanga walifanikiwa kuongeza karamu ya mabao baada ya mlinzi, Vicent Bossou, kufunga bao la nne katika dakika ya 89 akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Juma Abdul.

Mchezo mwingine wa ligi hiyo ulichezwa katika Uwanja wa Manungu, Morogoro ambapo wenyeji Mtibwa Sugar waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Majimaji FC ya Songea.

Matokeo hayo yameiwezesha Mtibwa kupanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi baada ya kufikisha pointi 30 na kuishusha Kagera Sugar yenye pointi 28 hadi nafasi ya nne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles