24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Maadili ya uchaguzi, wajibu wa vyama na wagombea

NPa HUSSEIN MAKAME

AMOJA na kuwapo sheria na kanuni za uchaguzi, historia ya chaguzi nchini Tanzania imedhihirisha umuhimu wa kuwapo kwa Maadili ya Uchaguzi ili kuepuka migogoro inayoweza kufifisha upatikanaji wa uchaguzi huru, haki, wazi na unaoaminika.

Hii inatokana na ukweli kwamba ili haki ipatikane ni lazima kuwapo uwanja sawa wa ushindani na kujenga mazingira yatakayokiwezesha kila chama cha siasa, mgombea kushiriki kwenye uchaguzi kwa kutekeleza matakwa ya sheria na kanuni za uchaguzi bila ya kikwazo chochote.

Umuhimu huo ndio umeyafanya Maadili ya Uchaguzi kupewa uzito wa ki- pekee kisheria kwa kuwepo sharti kwa kila mgombea kuanzia nafasi ya urais, ubunge na udiwani kutoa tamko la kuheshimu na kutekeleza Maaadili ya Uchaguzi kwa kusaini Fomu Na. 10 ya Maadili, tena mbele ya Tume.

Maadili ya Uchaguzi ni makubaliano ya pamoja baina ya vyama vya siasa, Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) yanayoeleza mambo yanayotakiwa kufanywa na yasiyotakiwa kufanywa katika wakati wa kampeni za uchaguzi, upigaji kura, hadi kutangaza matokeo.

Ili kuhakikisha maadili ya uchaguzi yanatekelezwa, vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Serikali, walisaini na kukubaliana Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2020 Mei 27 mwaka huu na kutoa tamko la pamoja kwamba:

“Sisi vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa pamoja, tumekubaliana kuwa na uchaguzi huru, wa haki, uwazi na wa kuamika.

“Na kwamba amani, ustawi wa nchi, usalama wa raia, uhuru wa vyama vya siasa na utii wa Sheria, Kanuni na taratibu za Uchaguzi ndio msingi wa Uchaguzi uliohuru, haki na wenye kuzingatia ushiriki wa

makundi yote ya jamii katika Uchaguzi. “Tunakubaliana kuwajibika kuyatekeleza Maadili haya yanayotokana na kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343.Tutafanya jitihada za wazi kuhakikisha maadili haya yanajulikana na kuheshimiwa na wagombea na wanachama wote wa vyama vya siasa.”

Makubaliano haya yalisainiwa na Katibu Mkuu Tixon Nzunda kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyekiti wa NEC Jaji Mst. Semistocles Kaijage na viongozi wa vyama vyote 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Kwa mujibu wa maadili hayo kila chama cha siasa na wagombea huwajibika kusaini maadili hayo wakati wa uchaguzi na chama ambacho hakitasaini kitazuiliwa kushiriki kampeni za uchaguzi na mgombea atakayekataa kusaini ataondolewa kushiriki uchaguzi.

Kila chama cha siasa, mgombea, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Serikali kinapaswa kutekeleza wajibu wake na kuzingatia mambo yanayotakiwa kufanywa na yasiyotakiwa kufanywa kuanzia wakati wa kampeni hadi kutangazwa kwa matokeo.

Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na ile ya Uchaguzi ya Serikai za Mitaa imeyafungamanisha Maaadili ya Uchauzi na kampeni za uchaguzi lengo ni kuweka uwanja sawa wa ushindani na kuwawezesha wananchi kupata nafasi ya kusikiliza Sera za wagombea na vyama vya siasa wakati wote wa kampeni za uchaguzi.

Sehemu ya pili ya maadili hayo, inabainisha wajibu wa kila chama cha siasa na mgombea anayeshiriki katika uchaguzi kuheshimu na kutekeleza ipasavyo maadili yafuatayo katika kuendesha shughuli za siasa wakati wa kampeni.

Chama cha siasa na mgombea anatakiwa kuheshimu na kutekeleza sheria za uchaguzi, kanuni za uchaguzi, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na sheria nyingine za nchi katika kipindi chote cha uchaguzi.

Kama hiyo haitoshi, viongozi wa vyama vya siasa na wagombea wanatakiwa kuwaelimisha, kuwahamasisha na kuwasisisitiza wanachama wao kutekeleza sheria za uchaguzi, sheria zingine za nchi, kanuni na taratibu zingine zilizowekwa.

Vyama vinatakiwa kufanya mikutano ya kampeni kwa kuzingatia ratiba rasmi iliyoratibiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi au wasimamizi wa uchaguzi na vinatakiwa vifanye mikutano yote kati ya saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.

Bila ya kuathiri muda uliopangwa kwa ajili ya kampeni, vyama vya siasa pia, vinaweza kutumia vipaza sauti kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 2:00 usiku kutoa matangazo ya mikutano itakayofanyika wakati wa kampeni.

Vyama vya siasa, wagombea, wanachama na wafuasi wao, wanatakiwa kuhakikisha kwamba wanachukua hatua za makusudi kufanya uchaguzi uwe wa amani, huru na wa haki, kwa kuepuka na kulaani vitendo vinavyoashiria vurugu.

Vyama vya siasa na wagombea wanatakiwa kuhakikisha wanaepuka na kukataa aina yoyote ya ubaguzi katika misingi ya jinsia, ulemavu, ukabila, udini au rangi na kueneza taarifa sahihi kuhusiana na mchakato wa uchaguzi.

Maadili ya uchaguzi pia yanawataka viongozi wa vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao kuzingatia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na vyombo vya habari katika kutekeleza shughuli za uchaguzi.

Wanatakiwa kuhakikisha vijitabu, vipeperushi, vitini, mabango na machapisho ya aina yoyote wanayochapisha yanayoelezea sera zao na kabla vitu hivyo havijatumika vinatakiwa kuidhinishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Wanatakiwa kutumia vyombo vya habari vya umma kutangaza sera zao kwa kuzingatia sheria za vyombo vya habari, sheria za uchaguzi ambapo vyombo hivyo vinaweza kutumiwa na wagombea wa urais na kugharamiwa na Serikali.

Vyama vyote vya siasa na wagombea wao wanatakiwa kujenga mazingira yatakayowezesha uchaguzi kufanyika kwa uhuru na haki ikiwa ni pamoja na kuwezesha makundi maalum ya wazee, wajawazito, wenye watoto wachanga na wenye ulemavu, kushiriki vyema katika uchaguzi.

Mwandishi ni Afisa Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa maswali, maoni na ushauri tuma kwenda hussein. [email protected] au sms 0737357524.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles