24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

NIT kulisaidia Taifa kunufaika na uchumi wa bluu

NA MWANDISHI WETU

Katika kuunga mkono juhudi za taifa za kukuza uchumi wa bluu, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimepanga kuanza kutoa kozi za ujenzi na utengenezaji wa meli.

Kozi hiyo maalumu katika kukuza uchumi wa bluu ama ‘Blue economy’ inatarajiwa kuanza kutolewa chuoni hapo kwa ngazi ya astashahada katika mwaka huu wa masomo wa 2020/21.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kampasi kuu ya Chuo hicho Mabibo jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Chuo Profesa Zacharia Mganilwa amesema kuwa “Uchumi wa bluu ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa nchi, ndiyo maana baada ya kuliona hilo Chuo kimeamua kuanza kutoa kozi hiyo muhimu kwa mwaka huu wa masomo”.

Profesa Mganilwa alisema pia,  mbali na kuanzisha programu hiyo ya astashahada katika ujenzi na utengenezaji wa meli,  Chuo kitaanzisha shahada ya kwanza ya Usimamizi na Usafirishaji katika Bandari (BSPLM).

“Katika mwaka huu wa masomo wa 2020/21, tutaanza kutoa astashahada itakayohusu shughuli za usafirishaji Bandarini pamoja na shahada ya mafundi na wahandisi ambao wataweza kujenga meli,” alisema.

Injinia Mganilwa amesema kuwa vigezo vingine kwa mwanafunzi kuweza kujiunga na kozi hiyo, lazima awe amemaliza kidato cha nne na kufaulu angalau masomo manne ukiondoa somo la dini.

Katika astashahada  ya ujenzi na ukarabati wa meli, alisema mwanafunzi lazima awe amemaliza kidato cha nne na kufaulu masomo 4 au alama D katika fizikia / uhandisi, sayansi, hisabati, kemia na Kiingereza .

“Katika kuweza kusoma kozi hii, mwanafunzi anatakiwa ama awe amemaliza elimu ya ufundi (NVA) kwa kiwango cha level 3 katika nyanja zinazohusiana na uhandisi kama vile ufundi wa umeme pamoja na ufaulu kwa somo la hisabati kidato cha nne.

“Mbali na kuanzisha kozi hizo katika mikakati ya chuo kusaidia kukuza uchumi wa bluu, tutaleta kozi zingine kusaidia mpango huu ikiwa ni pamoja na stashahada ya kawaida katika shughuli za usafirishaji wa barabara na reli pamoja na Shahada  katika usimamizi na usafirishaji wa barabara na reli (BRRTLM),” alisema.

Akifafanua, Prof Mganilwa alisema wameanzisha kozi hizo kwa maana kuwa unapoimarisha bandari, basi ni lazima kuwepo na usafirishaji na usimamizi wa bidhaa kutoka bandarini ama kusafirisha nje ya nchi.

“Chuo kimejipanga kiuhakika kuhakikisha kuwa bidhaa zote ambazo zinazalishwa na viwanda vyetu, zinasafirishwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia hilo ndiyo maana tumeanzisha kozi hizi ambazo zitazalisha wahitimu bora katika nyanja za usafirishaji,” alisema.

Alisema, NIT ni Taasisi mahiri yenye uwezo wa kutoa mafunzo ya kada mbalimbali za usafiri kwa kutumia teknolojia za kisasa na zenye viwango vya kimataifa.

Profesa Mganilwa amewataka wazazi na vijana wa Kitanzania kuchangamkia fursa hii ya mafunzo kwa sababu sekta ya uchukuzi inakuwa kwa kasi na ina uhitaji mkubwa wa rasilimali watu hivyo kusoma kozi hizi watajitengenezea mazingira mazuri ya kupata ajira na kujiajiri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles