23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA AKAWARIBISHA UKAWA KINA SOPHIA SIMBA

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amekaribisha waliokuwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba kujiunga na Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyasema hayo jana katika taarifa yake.

Alisema  wanachama hao walikuwa  mashujaa wa kutetea haki, demokrasia na taratibu kwa kupinga dhuluma ndani ya chama chao cha CCM.

“Nafsi yangu imenisukuma kushika kalamu na kuandika haya kutokana na kile kilichotokea Dodoma katika vikao vya CCM.

“Ni takriban miezi 20 sasa toka nilipojitoa  CCM, lakini nasikia bado naendelea kutajwatajwa huko katika vikao vyao.

“Wamewatimua wanachama na viongozi wao ambao wengi wao walitumia demokasia yao kupinga upindishwaji wa kanuni na sheria za chama chao.

“Nataka kuwaambia kuwa wakati wakifanya hivyo walikuwa mashujaa wa haki na demokrasia na misingi ya utawala bora nchini,” alisema Lowassa katika taarifa yake

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu alisema   wanachama hao wa CCM walisimamia kile walichokiamini bila ya kuvunja sheria, wamekata minyororo ya unyonge na uonevu.

“Mbegu ile waliyoipanda itamea na kuzaa matunda demokrasia ya kweli nchini kwetu.

“Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba upinzani wa kweli utatokea CCM, naamini usemi huo sasa unatimia kwa kasi kubwa.

“Nawakaribisha Chadema na Ukawa kwa jumla huku kuna maisha mazuri sana, hakuna minyororo ya utumwa wa siasa. Kilichowapata ni sawa na kumpiga chura teke unamuongezea kasi tu.

“…waje wajiunge nasi katika safari ya kuleta demokrasia ya kweli na siasa zenye ukomavu, safari hii inahitaji umoja na mshikamano kufikia malengo,” alisema.

Lowassa alisema anashangazwa na namna hatua ya CCM kujinasibu kuwa CCM ikiyumba. 

Alisema nchi itayumba lakini anaamini  kinachotokea  na jinsi CCM inavyoyumba  ndivyo wananchi wanavyozidi kukomaa katika siasa na kuimarika katika harakati za kutafuta mabadiliko ya kweli.

Alisema Watanzania wa sasa hawawezi tena kuvumilia ukandamizaji wa haki zao za msingi unaofanywa na watawala.

“Nidhamu ya woga haina tena nafasi katika kujenga nchi yenye  kuheshimu misingi ya haki demokasia na utawala bora,” alisema.

Juzi, CCM kilitangaza kuwafukuza wanachama wake 12, akiwamo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba, ambaye wiki iliyopita alitangaza kutogombea tena nafasi hiyo.

Wengine waliofukuzwa ni wenyeviti mikoa ambao ni Jesca Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga), Ramadhan Madabiba (Dar es Salaam) na Christopher Sanya (Mara).

Waliofukuzwa wengine  ni Willfred ole Mollel ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha Mjini, mjumbe wa NEC wa Wilaya ya Babati Mjini, Ally Sumaye na Mathias Manga wa Wilaya ya Arumeru.

Katika orodha hiyo pia wamo wenyeviti wa wilaya wa chama hicho ambao ni Omari Awadhi (Gairo), Ally Msuya (Babati Mjini), Makolo Laizer (Longido) na Salumu Madenge (Kinondoni-Dar es Salaam).

Wanachama wengine waliochukuliwa hatua baada ya kufanya makosa kama hayo kuwa ni Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye amepewa onyo kali na anatakiwa kuomba radhi.

Wakati Nchimbi akipewa onyo, Adam Kimbisa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma na Mbunge wa Afrika Mashariki   amesamehewa.

Kutokana na uamuzi huo Sophia atalazimika kupoteza ubunge.  Ilielezwa kuwa amefukuzwa baada ya kupatikana na makosa ya maadili kinyume na Katiba na kanuni za chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles