24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA AFICHUA SIRI KUMALIZWA KISIASA

Na Mwandishi Wetu-KENYA


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema vitendo anavyofanyiwa na mamlaka za Serikali nchini zina lengo la kupunguza nguvu yake ya  siasa.

Hata hivyo  amesema anajivunia uzoefu alionao hali inayochangia na umaarufu wake katika medani za siasa.

Lowassa  ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema hayo wakati akihojiwa na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Serena mjini Nairobi, Kenya jana.

Lowassa alikuwa Kenya kuhudhuria mazishi ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Nkaissery, ambaye alifariki dunia wiki mbili zilizopita.

Katika mahojiano hayo, Lowassa alisisitiza kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2015 ulichakachuliwa kwa ajili ya Rais Magufuli, lakini amejipanga kupambana siku nyingine.

“Imekuwa uzoefu mzuri ulioambatana na nyakati nzuri na ninafurahia uzoefu huu kwa sababu mimi bado ni maarufu miongoni mwa Watanzania wengi na marufuku hii ya shughuli za siasa ililenga kupunguza nguvu yangu,” alisema Lowassa.

Lakini aligoma kutoa tathmini yake juu ya utendaji wa Rais John Magufuli, akisema ni Watanzania watakaoamua mwishoni mwa muhula wake wa kwanza mwaka 2020.

“Pamoja na kwamba Dk. Magufuli alichaguliwa katika mfumo wenye shaka, bado tunamheshimu kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”  alisema Lowassa na kuongeza:

“Utendaji wa Magufuli utaamuliwa na watu mwishoni mwa muhula wake wa kwanza mwaka 2020. Nachagua maneno kwa uangalifu kwa sababu naweza kukaririwa vibaya na kujikuta katika matatizo nitakaporudi nyumbani.”

Polisi wamepiga marufuku mikutano ya  siasa mwaka 2016 wakisema kuwa matukio hayo yanayofanywa na upinzani ni haramu na yana uwezekano wa kuvuruga amani.

Rais Magufuli ambaye alisema hakuna shughuli za siasa hadi uchaguzi mkuu 2020 na kuwataka watu   wajikite kufanya kazi, alilegeza msimamo kwa kuruhusu viongozi wa kuchaguliwa kuendesha mikutano katika majimbo yao.

Lakini Lowassa alisema marufuku hiyo ya shughuli za siasa ni changamoto kubwa katika maisha yake ya siasa za upinzani.

Alisema mtu unaweza kulazimika kutumia mahakama kuingilia kati iwapo marufuku hiyo itazidi kuuma.

“Marufuku hii si ya demokrasia na si ya haki. Tumeiomba serikali ifikirie upya  lakini bado haiko tayari,” alisema.

Wakati Lowasa akikiri kuwa maisha katika upinzani yana changamoto kwake, aligusia kwamba kuna nyakati nzuri na  anafurahia kuwa upande huo.

Awali,  Lowassa alieleza kwa nini anamuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta kuchaguliwa tena katika Uchaguzi Mkuu wa Kenya Agosti 8.

Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini kitoa tamko la kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta  kikisema ni mgombea urais sahihi na chaguo bora kwa demokrasia ya Kenya.

“Tulikuwa na mikutano rasmi kama chama na kwa kauli moja tulikubaliana kuunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Uhuru Kenyatta.

“Ni mtu mzuri, anaunga mkono mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na anaheshimu viongozi wa upinzani,” alisema.

Hata hivyo, Lowasa alisema uamuzi wa nani atakuwa Rais wa Kenya utafanywa na Wakenya wenyewe   watakapopiga kura mwezi ujao.

Aliongeza kuwa Uhuru ameonyesha heshima kwa jamii ya Wamasai na kwamba uhusiano baina ya Kenya na Tanzania utakuwa mzuri   Kenyatta akiwa madarakani.

Kitendo cha Chadema kumuunga mkono Rais Kenyatta kinaaminika ni  kutokana na uhusiano wa karibu uliopo baina ya Kiongozi wa upinzani wa Kenya, Raila Odinga na Rais Magufuli.

Chama hicho kilielezwa kusikitishwa na Odinga kumuunga mkono Dk. Magufuli wakati wa kampen za urais mwaka 2015  kitu ambacho kiliona kuwa ni usaliti.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwahi kukaririwa akimueleza Odinga kuwa msaliti kwa kumuunga mkono Rais Magufuli.

“Tulimuunga mkono Odinga wakati wa uchaguzi wa Kenya mwaka 2013   lakini kwa mshangao wetu wakati ilipokuwa zamu ya Tanzania kufanya uchaguzi mwaka 2015, alimuunga mkono mgombea urais wa CCM. Odinga ni msaliti,’’  alisema Mbowe   Mei mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles