MITAMBO IPTL YAZIMWA

1
640

*Wakwama kufanya biashara ya umeme

NA NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


NI wingu zito. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya maombi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kukwama, huku wakilazimika  kuzima rasmi mitambo yao ya uzalishaji umeme.

Hatua hiyo imekuja baada ya kukwama kwa maombi ya kuongezewa muda wa miezi 55 ya leseni yake ya uzalishaji umeme kutokana na kusubiri uamuzi wa Ikulu.

Hali hiyo inajitokeza wakati mmiliki wa Kampuni ya Pan Afrika Power (PAP), Harbinder Singh Sethi na Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira wakiwa tayari wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya uhujumu uchumi, kutakatisha fedha na kuisababishia hasara Serikali.

Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana zilisema mitambo hiyo kwa sasa haizalishi umeme.

MTANZANIA lilitembelea mitambo hiyo iliyoko Tegeta na kukuta wafanyakazi wachache ambao walikiri mitambo hiyo kutofanya kazi.

“Mitambo ilizimwa tangu siku ile walipomkamata Sethi,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazetini.

Pamoja na hatua hiyo inaelezwa kuwa kuna hatari ta kuitaifishwa kwa mitambo hiyo hasa baada ya Serikali kuweka ngumu katika utoaji wa leseni mpya ya biashara ya kuzalisha umeme kwa kampuni hiyo.

Licha ya hali hiyo leseni ya kampuni hiyo ilimalizika muda wake Julai 15, mwaka huu ambapo hadi sasa uamuzi wa kuitaisha mitambo hiyo kurudi kuwa mali za Tanesco ama laa ukisubiri uamuzi wa Ikulu.

Kwa sababu hiyo,  kama Serikali itaendelea na msimamo wake dhidi ya IPTL ndiyo utakuwa mwisho wa miaka 23 ya IPTL.

Kampuni hiyo ua IPTL iliingia chini  tangu mwaka 1994 na kila mwezi imekuwa ikilipwa Sh. bilioni   5.943 na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)  ikiwa ni gharama za uwekezaji mbali na gharama za umeme inaoliuzia shirika hilo,

Novemba 2014, baada ya Bunge kujadili Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilitoa maazimio manane ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kuichukua mitambo ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco.

Siku chache baada ya Bunge kupitisha uamuzi huo ambao ulifanyiwa kazi kwa haraka kwa Profesa Sospeter  Muhongo kujiuzulu nafasi yake.

Wengine ni Profesa Anna Tibaijuka ambaye pia alijiuzulu nafasi ya Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Jaji Frederick Werema aliyejiuzulu nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Eliachim Maswi aliyekuwa Katibu  Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini  alisimamishwa  kazi pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco waliotakiwa kuwajibishwa, kukaa pembeni baada ya muda wa bodi yao kwisha na ikaundwa nyingine.

Naye   Spika wa Bunge wakati huo, Anne Makinda alitangaza kuwa wazi nafasi za wenyeviti wa kamati za Bunge ambao ni William Ngeleja, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Andrew Chenge aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Victor Mwambalaswa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini.

Azimio jingine lililotaka  Harbinder Singh Seth ambaye ni Mwenyekiti wa PAP kufikishwa mahakamani, lilitekelezwa hivi karibuni ambako yeye na mwenzake James Rugemalira wa VIP Engineering, walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka 12 yakiwamo ya uhujumu uchumi na kutakatisha fedha.

Baadhi ya maazimio ambayo yalikuwa hayajafanyiwa kazi ni   lile la pili lilolotaka  Serikali iangalie uwezekano wa kuichukua mitambo ya   IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO.

Mei 11, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, wakati wa maswali ya papo kwa papo bungeni, alimuhoji  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu kutokutekelezwa maazimio hayo ya Bunge kuhusu Escrow.

Akijibu swali hilo, Majaliwa alimuhakikishia Mbowe kuwa Serikali inaheshimu muhimili wa Bunge na kuthamini uamuzi wake.

Alisema  kunahitajika uchunguzi wa kina na yapo mambo ambayo yana umuhimu wa kufikishwa  bungeni hivyo uchunguzi wa Serikali utakapokamilika yatawasilishwa bungeni.

Kwa sababu hiyo, inawezekana kuisha   leseni hiyo ya IPTL sasa, kukachukuliwa kama moja ya njia ya kutekeleza azimio  la lipi la Bunge.

Pia Juni 20 mwaka huu,  akiwa ziarani mkoani Pwani, Rais John Magufuli, alisema serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaolihujumu Taifa ikiwamo kujihusisha na vitendo vya wizi na rushwa na haitakatishwa tamaa na watu wanaolalamika na kubeza juhudi hizo.

“Stiegler’s Gorge, mradi ambao ulifanyiwa utafiti tangu enzi ya Mwalimu  Nyerere  tukautelekeza.

“Nataka tujenge bwawa litakalozalisha umeme utakaotosheleza katika nchi yetu, nchi ya viwanda ili Watanzania wasilalamikie tena suala la umeme, nataka tuachane na umeme wa matapeli wanaokuja hapa wanawekeza kwa lengo la kutuibia.

“Mimi nachukia wezi na kwa kweli wezi watakoma tu, awe mwizi wa Tanzania, awe mwizi wa Ulaya, awe anatoka magharibi, mashariki, kaskazini au kusini, mwizi ni mwizi tu,” alisema  Rais Magufuli.

IPTL imekuwa ikilalamikiwa kuwa ni miongoni mwa miradi inayoiumiza Tanesco, hivyo kauli hiyo ya mkuu wa nchi  inaweza kuwa siyo ishara njema kwa kampuni hiyo.

Kampuni binafsi zinavyoinyonya Tanesco

Moja ya taarifa za Ewura kuhusu kampuni zinazoiuzia Tanesco umeme,  inaonyesha kuwa IPTL inauzia Tanesco kila uniti ya umeme kwa Dola za Marekani senti, 23.1 na kila mwezi inalipwa Capacity Charge ya Dola za Marekani 2,655,786.

Ukikokotoa kiasi hicho kwa wastani wa kila Dola moja kwa Sh 2,238, inafanya kila mwezi IPTL kulipwa Sh bilioni 5.943 ambazo kwa mwaka inakuwa   Sh  bilioni 71.316.

Kwa upande wa Kampuni ya Aggreko ambayo mkataba wake umekwisha, ilikuwa ikiiuzia Tanesco uniti moja ya umeme kwa Dola za Marekani senti 35.8, kila mwezi inalipwa Capacity Charge ya Dola za Marekani 2,084,998.43 ambazo ni wastani wa Sh. bilioni 4.566.

Kiasi hicho kinaamanisha kwamba , kila mwaka Tanesco hulipa kampuni hiyo Sh  bilioni 54.792 na mpaka Desemba, 2014 ilipopunguza uzalishaji kutoka megawati 100 mpaka 50, ilikuwa imelipwa wastani wa Sh  bilioni 164.376.

Nayo  Symbion ambayo mkataba wake umesimamishwa, kwa mitambo iliyo Arusha, Tanesco inauziwa uniti moja ya umeme kwa Dola za Marekani senti 44.4.

Kila mwezi ilikuwa ikilipwa Capacity Charge ya Dola za Marekani 1,866,760 ambazo ni wastani wa Sh bilioni 4.088 kwa mwezi.

Fedha hizo ni wastani wa Sh bilioni 49.056 kwa mwaka na hivyo tangu 2012 mpaka 2014, mkataba wao ulivyoisha walikuwa wamelipwa wastani wa Sh  bilioni 147.168.

Symbion Dodoma ilikuwa ikiiuzia Tanesco uniti moja kwa dola za Marekani senti 42.4 na ilikuwa ikilipwa Capacity Charge ya dola za Marekani 2,252,145 kila mwezi ambazo ni wastani wa Sh bilioni 4.932.

Kwa mwaka ilikuwa ikilipwa Sh. 59.184 na kwa miaka mitatu iliyokaa ilikusanya Sh bilioni 177.552.

Wiki iliyopita, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo, alipotafutwa na gazeti hili   kuzungumzia hatima ya IPTL, alisema mashauriano na serikali bado yanaendelea na ikifika Julai 15 angeweza kuwa na jambo la kusema.

 

MTANZANIA pia ilimtafuta Kamishna wa Nishati, Innocent Luoga,  kujua mazungumzo ya suala hilo yalipofikia   naye alisema:

 

“Natamani kama ningeweza kukujibu  lakini suala hili msemaji wake ni Katibu Mkuu ambaye hayupo.  Lakini tu nikwambia ukweli kwamba kwa sasa lipo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, kwa hiyo siwezi kusema chochote,” alisema.

 

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, alipotafutwa   kuthibitisha kama kweli suala hilo limefika mezani kwa Katibu Mkuu Kiongozi, alisema:

“Hili suala ni la Wizara ya Nishati, kama wamewaambia kuwa wamelipeleka kwa Katibu Mkuu Kiongozi basi watakachojibiwa watawaeleza,” alisema.

 

Kafulila

MTANZANIA ilipomtafuta aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila  kupata maoni yake kuhusu suala la kutaifishwa   mitambo ya IPTL, alisema Serikali haipaswi kuongeza muda wa leseni kwa kampuni hiyo.

“Ni wazi Serikali haipaswi kuongezea kampuni muda wa leseni wakati umiliki wake una utata mkubwa.

“Kwa maana wanaojiita wamiliki siyo wamiliki halali na kwa sababu Bunge limekwisha kuazimia Novemba 2014 mitambo hiyo kutaifishwa ni wazi Serikali kutotekeleza ni sawa na kulipuuza Bunge ambalo ni muhimili mkuu wa dola na maazimio yake yanapaswa kutekelezwa na Serikali kwa lazima.

“Siyo Bunge linaazimia halafu Serikali inajishauri.  Kwa mujibu wa katiba Bunge likishatoa  azimio  Serikali haina namna isipokuwa kutekeleza.

“Kama inaona azimio la Bunge linavunja Sheria serikali iombe tafsiri ya Mahakama na siyo yenyewe kuwa inachuja maazimio ya Bunge na kuamua lipi itekeleze na lipi ipuuze,” alisema Kafulila.

 

1 COMMENT

  1. Serikali itaifishw IPTL ‘FASTA’ Kwa vile bunge lilishamua kwamba huo mtambo uchukuliwe na serikali tangu 2014, serikali ilichelewa sana kuchukua hatua hiyo. TANESCO (yaani Serikali) inadaiwa fedha yote ambayo Benki ya Standard Chartered inadai IPTL lakini kwa vile fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti ya ESCROW ili zitumike kulipa madai kama hayo zimeshachukuliwa na ITPL, basi ni LAZIMA huo mtambo utaifishwe. Hiyo kampuni ya IPTL imetuibia sana kwa kutulipisha capacity charge hata wakati ambapo umeme ulikuwa hauzalishwi. Hesabu za kweli zikipigwa, tutakuwa tunadai fedha nyingi sana kuliko thamani ya mitambo yote ya IPTL.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here