VETO: DAR ES SALAAM TISHIO KWA MAZINGIRA

0
854
Mwonekano wa jiji la Dar es Salaam

NA MARKUS MPANGALA,

JIJI la Dar es Salaam linasifika kwa mambo mengi mazuri. Uzuri wa jiji hili umekuwa kimbilio la watu wengi kote nchini. Vijana hutoroka miji mingine na kuingia jijini Dar es Salaam. Jiji hilo ni mfano wa miji inayobeba maelfu ya watu wasio na kazi au shughuli rasmi

Ni jiji hilo hilo pia linasifika kwa kiwango kikubwa cha uchafu na miundombinu mibovu nyakati za masika, wimbi la vibaka na ujambazi. Jiji la Dar es Salaam lilipangwa mwaka 1912.

Mwaka 2014 Mtaalamu wa Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Dk Robert Kiunsi aliliambia gazeti moja la kila siku hapa nchini (Si Mtanzania) katika utafiti wake kuhusu ‘Msongamano wa magari Dar es Salaam na mpangilio wa jiji’ kwamba ujenzi wa mji  huo hauna mpangilio bora.

Ripoti ya utafiti wake ilieleza kuwa, Jiji la Dar es Salaam lina wakazi takribani milioni nne kati ya hao, asilimia 60 wameajiriwa katika sekta rasmi ikiwamo biashara, uvuvi, kilimo, kazi za viwandani, useremala na uashi, hivyo wote hufanya kazi katika eneo moja.

Aidha, Takwimu kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi zinaeleza kuwa, asilimia 60 hadi 75 ya wakazi wa Jiji la Dar es salaam, wanaishi katika makazi holela. Asilimia 78 zilizobaki ni eneo lililojengwa bila mpangilio.

Asilimia 21.7 ya maeneo yaliyojengwa kwa mpango, eneo la makazi ni asilimia 13.2, vyanzo vya maji asilimia 4, viwanda 1.3 na taasisi za Serikali ni 3.2.

Ongezeko la watu litachochea ukuaji wa mahitaji na shughuli za kiuchumi hivyo mahitaji ya miundombinu yatakuwa makubwa zaidi na msongamano utakithiri zaidi.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa msongamano wa magari unatokana na sababu nyingi ikiwamo, ukuaji wa uchumi, ongezeko la magari, mpangilio mbovu wa jiji, miundombinu duni, kukosa mpangilio wa mji ulioboreshwa na ongezeko kubwa la watu mijini.

TISHIO LA MAZINGIRA NCHINI

Hapa ndipo palipo kiini cha hoja yangu. Kwa upande wa utajiri Jiji la Dar es Salaam limekuwa tajiri mno, vibopa wanaishi hapa. Kumbi za starehe zipo nyingi. Lakini hatari inayoikumba nchi hii ni uharibifu wa mazingira unaochangiwa na Jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya ufunguzi wa warsha ya kujadili mikakati ya kupunguza matumizi ya mkaa nchini katika Chuo cha Utalii jijini Dar es Salaam ya Novemba 29, 2016 imeeleza bayana juu ya uharibifu wa mazingira.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema, “Wataalamu wetu wanatuonya kuwa kama hatutaanza sasa kutumia nishati mbadala, mahitaji ya mkaa yatafikia takribani tani milioni tano kwa mwaka ifikapo mwaka 2030 kutoka tani milioni 2.4 zilizotumika mwaka 2015. Hii ina maana kuwa tutatumia zaidi ya mara mbili ya matumizi ya sasa kwa kipindi cha miaka kumi na nne hivi ijayo,”

Aidha, Waziri Majaliwa aliongeza kuwa, “Takwimu zinaonyesha kuwa takriban asilimia 54 ya nchi yetu sawa na hekta milioni 48 ni misitu. Asilimia 34.5 ikiwa ni misitu inayosimamiwa na Serikali ya Kuu, asilimia 45.7 ni misitu katika ardhi ya vijiji, asilimia 6.5 inasimamiwa na Serikali za Mitaa; asilimia 7.3 ikimilikiwa na watu binafsi; na asilimia 5.7 ikiwa katika maeneo ya jumla ya umma (general land).

Anasema, “Uharibifu wa Mazingira Pamoja na Mungu kutujalia utajiri huu, Nchi yetu inakabiliwa na changamoto kubwa sana za uharibifu wa mazingira kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ufugaji wa kuhamahama, mifugo kuvamia misitu yetu na kuiharibu pamoja na vyanzo vya maji,”

Baada ya maneno hayo sasa twende mbele tena. Taarifa zinasema; kwa mwaka tunakata ekari 400,000 za misitu ili kutengeneza mkaa. Dare salaam inatumia asilimia 50 ya mkaa huo inamaanisha kwa mwaka ekari 200,000 zinateketezwa ili Dar es Salaam ipate mkaa wa kupikia!

Ndiyo kusema ni sawa na ekari ya 547 za misutu zinateketezwa kwa ajili ya mkaa wa Dar es Salaam peke yake. Na yote hayo yanatokea kwenye jiji la Dar es Salaam ambalo lina vyanzo mbadala vya nishati kwa matumizi ya kupikia.

Vilevile Dar es Salaam inatumia asilimia 50 ya mkaa wote unaozalishwa nchini, japokuwa ndio mkoa wenye vyanzo mbadala zaidi vya nishati.

Dar es Salaam ndio mkoa wenye unasambazaji mkubwa wa umeme pia nishati ya gesi ya kupikia inapatikana kwa wingi. Majaribio kadhaa ya vitendo yameonyesha kuwa matumizi ya gesi kwa kupikia ni nafuu kuliko gharama za mkaa.

Hii inamaanisha kuwa Dar es Salaam ndio kiini cha uharibifu wa mazingira kote nchini kwasababu asilimia 50 ya mkaa unaingia jiji hili. Hiyo ni sawa na kusema nusu ya watumiaji wa nishati ya mkaa wanapatikana katika jiji la Dar es Salaam.

Hapo ndipo ninapoona hatari ya mji huo, na kwamba umebeba uhai wa taifa letu ambao tunaweza kuulinda zaidi iwapo tutahakikisha nidhati mbadala inapatikana.

Takwimu zilizopo zinatisha mno, kiasi kwamba tunapaswa kuishauri serikali kutoa kipindi maalumu kwa kila kaya ndani inayoishi jiji la Dar es Salaam kuhakikisha inanunua jiko la gesi au la umeme na baada ya hapo mkaa uwe marufuku kuingia kwa madhumuni ya kulinda mazingira sasa.

Dar es Salaam inatakiwa kujifunza kwa Mkoa wa Singida ambao unakabiliwa na uhaba wa nyasi za kulisha mifugo (ng’ombe) kwasababu miaka ya nyuma kulikuwa na wimbi la ukataji wa misitu ambalo limesababisha kutoweka kwa uoto wa asili na kusababisha jangwa.

Baruapepe; mawazoni15@gmail.com

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here