29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 18, 2022

Latra waeleza sababu za kupungua ajali za mabasi

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) imesema matumizi ya mfumo wa ufuatiliaji mabasi (VTS), yamewafanya wananchi kuwa na amani wakati wa safari tofauti na mwanzo kwa kupunguza hofu ya kupata ajali.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam hivi karibuni Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara, Johansen Kahatano, alisema mfumo huo pia umepunguza malalamiko ya abiria yaliyokuwa yakifikishwa kwa mamlaka hiyo awali.

Kahatano alisema licha ya kuwapo matukio ya ajali za barabarani, matumizi ya mfumo huo yamepunguza kwa kiasi kukibwa matukio makubwa ya ajali yaliyokuwa yakisababisha vifo na majeruhi wengi na kwamba kwa sasa mwaka unaweza kwisha bila matukio ya aina hiyo.

“Malalamiko ya wasafiri kuhusu mabasi kwenda kasi yamepungua na yamekuwa yanajitokeza mara moja moja. Na hili si faida kwa abiria tu hata wamiliki wamepata unafuu wa zile hasara walizokuwa wakizipata na wengine hata wameamua kupunguza bima kubwa walizokuwa wakikata kwa ajili ya magari yao.

“Faida za kuichumi kwa upande wa wamiliki mfumo huu umepunguza matumizi ya mafuta na vipuli na kusaidia sekta kuwa endelevu kwa kuokoa fedha ambazo zilikuwa zinatumika kununua mafuta na vipuli na kuziwekeza maeneo mengine,” alisema Kahatano.

Pia alisema kuwa mfumo huo umeirahisishia mamlaka hiyo ufuatiliaji na kusaidia kapatikana kwa taarifa sahihi na za haraka tofauti na awali na kwamba mfumo huo imeipatia mamlaka uwezo mkubwa wa kusimamia sekta ya usafirishaji.

Alisema pamoja na mafanikio ya mfumo huo kumekuwapo na changamoto mbalimbali ikiwamo baadhi ya wamiliki wa mabasi kutokuwa na utayari wa kuutumia na kushindwa kuwafuatilia madereva kuhakikisha hawachezei mfumo huo katika mabasi yao.

Kahatano alisema hadi sasa karibu mabasi 5,000 yanayofanya safari kwenda mikoa mbalimbali nchini tayari yamefungwa mfumo huo.

Katika hatua nyingine Kahatano alisema kuanza kukatisha tiketi kwa njia za kielektroniki kutasaidia kukuza mitaji ya wamiliki wa mabasi na kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo.

“Hili ni suala lenye faida kwa pande zote mbili abiria lakini pia kwa mmiliki wa basi. Kwa sasa wamiliki wa mabasi wamekuwa wakiuziwa abiria ambao wanakuja wenyewe stendi lakini wanakutana na wapiga debe wanawauza kwenye mabasi na wao wanalipwa nauli ndogo tofauti na ile iliyopangwa. Sasa huu mfumo utawapunguzia hiyo shida.

“Na hapa ni lazima tufahamu kuwa wapiga debe wanaangalia maslahi yao zaidi, niwashauri wamiliki ni vema waajiri watu wenye elimu wawasaidie kusimamia,” alisema Kahatano.

Kuhusu utekelezaji wa ukatishaji tekiti kielektroniki alisema kwa sasa mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kwa muda wa wiki sita ili kuhakikisha wadau wote muhimu wanafikiwa na kuwezesha mchakato huo kuendeshwa kwa urahisi.

Kuhusu mamlaka hiyo kushindwa kuafikiana mapema na wamiliki wa mabasi kuhusu ukatishaji tiketi kielektroniki alisema hakuna tofauti kati yao bali hali hiyo husababishwa na ugeni wa mfumo huo na kusababisha wamiliki kuwa na mashaka kuhusu ufanisi wake.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,936FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles