24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Kwanini mbio za mwenge bado zipo?

mwengeNIKIWA binti mdogo wakati nasoma shule ya msingi miaka ya 1980, nilizoea kusikia na kuimba wimbo mmoja ambao niliupenda sana mpangilio wake wa ala za muziki, na sauti zilizokuwa zikisikika. Huu si wimbo mwingine, bali ni wimbo ambao ulihusu alama kubwa sana ya Taifa letu: Mwenge wa Uhuru.

Wimbo ulikwenda namna hii: “Sisi tumekwisha uwasha Mwenge, tumekwisha uwasha Mwenge. Na kuuweka juu ya mlima, Mlima Kilimanjaro. Kuwasha Mwenge, Kuwasha Mwenge na kuuweka Kilimanjaro; Kuwasha Mwenge, Kuwasha Mwenge na kuuweka Kilimanjaro.”

Naam. Niliupenda mahadhi yake na nakumbuka hata tukiwa sekondari, tulitakiwa kuchangia shilingi tano za mafuta ya taa kwa ajili ya Mwenge huo. Tulijivunia Mwenge huu na tuliaminishwa pia kwamba una maana kubwa sana kwa Taifa letu.

Siku za hivi karibuni, hata hivyo, Watanzania wengi wanaonekana wameuchoka Mwenge. Imefikia hatua kwamba picha zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha Mwenge wa Uhuru na chini yake kukiwa na maneno: Mtumishi hewa namba moja. Picha hiyo imesambazwa sana na kuendelea kusambazwa kwake kunaweza kutafsiriwa kwamba watu wengi wanakubaliana na kauli hiyo ya kuwa kweli alama hii ya Taifa ni mtumishi hewa namba moja.

Wapo pia, nikiwamo mimi, ambao tulidhani kwamba baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani, basi angeufutilia mbali Mwenge, kwa maana ya kufuta kabisa hizi mbio za Mwenge ambazo zimekuwa zikifanyika kila mwaka. Huenda wengi wetu tulifikiri hivi kutokana na sababu mbalimbali ambazo zinasababisha tudhani kwamba Mwenge huu wa Uhuru hauna faida.

Bahati nzuri, niliposikia kwamba Mwenge haujafutwa, bado upo na utaendelea kukimbizwa mwaka huu, nikaamua kujiuliza maswali kadhaa. Kwanini hasa mbio hizi za Mwenge wa Uhuru hazijafutwa?

Kwa kuanzia, naomba nitofautishe vitu viwili hapa: Kuna Mwenge wa Uhuru, halafu kuna Mbio za Mwenge wa Uhuru. Ni mambo mawili tofauti. Ili kuelewa tofauti ya mambo haya mawili, nadhani inatupasa kurudi kwenye historia.

Kwa ninavyoelewa, Mwenge wa Uhuru ulianza Disemba 9, 1961, siku ya Uhuru wa Tanganyika. Wakati bendera ya Malkia wa Uingereza ikishushwa Uwanja wa Taifa, bendera ya Tanganyika ilipandishwa, sambamba na Mwenge wa uhuru kuwashwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro. Hiyo inadhihirisha kwamba Mwenge wa Uhuru una maana kubwa sana kwa uhuru wa nchi hii.

Kwa mujibu wa tovuti ya Serikali ya Tanzania, Mwenge wa Uhuru huzunguka nchi nzima ukiwa na ujumbe wa matumaini, upendo, heshima na amani. Mwenge huo huanzia katika mkoa wowote utakaochaguliwa kila mwaka na mbio hizo hufika tamati Oktoba 14, siku ambayo Taifa huadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Vilevile, tovuti ya Serikali inaongeza kwamba Mwenge huwa na ujumbe tofauti kila mwaka, kulingana na vipaumbele vya maendeleo vya mwaka husika.

Historia pia inatueleza kwamba siku Mwenge wa Uhuru ulipokuwa ukiwashwa juu ya Mlima Kilimanjaro kwa mara ya kwanza, Mwalimu Nyerere alisema maneno yafuatayo: “Tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu; ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini; upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.”

Mwenge huo uliwekwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro na Luteni Kanali, Alexander Nyirenda. Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba Mwenge una umuhimu mkubwa katika kuijenga Tanzania yenye umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa watu wote.

Hiyo ilikuwa Disemba 9, 1961 na tangu mimi nilipokuwa na ufahamu wa kuweza kuwaza mwenyewe, nimekuwa nikisikia kila mwaka kukiwa na mbio za Mwenge. Nadhani lengo lake ni kujikumbusha kuhusu wajibu wetu kama wananchi kuwa na umoja, mshikamano, upendo na amani.

Leo hii, mwaka 2016, wananchi wengi sana wanaonekana hawana imani na mbio za Mwenge. Wana sababu zao za msingi kabisa, ambazo pengine zingefaa kuangaliwa. Sababu moja kubwa ni kwamba mbio za Mwenge zinamaliza tu hela kutokana na Mwenge huo kuwashwa kwa mafuta ya taa. Hela inayotumika kuzunguka nchi nzima ni kubwa sana, pamoja na posho na usafiri kwa wale wakimbiza Mwenge wote.

Sambamba na hilo, ni ukweli usiofichika kwamba Mwenge ukilala kwenye eneo fulani, basi eneo hilo usiku huo kutakuwa na kucheza ngoma usiku kucha, pamoja na vitendo vya wazi kabisa vya zinaa. Ukiwauliza wahudhuriaji, watakueleza kwamba ifikapo asubuhi, kondomu zilizotumika huokotwa kwa wingi na zinaweza kujaza ndoo kadhaa. Ikumbukwe kwamba hizo ni zilizotumika. Kuna uwezekano mkubwa kwamba wapo watu ambao hata hawakutumia kabisa kondomu. Ni alama mbaya sana, kwani mbio za Mwenge wakati mwingine hutumika kama upenyo wa kufanya zinaa isiyo salama.

Lakini vilevile, swali lingine ambalo watu wengi wamekuwa wakijiuliza, ni: Hivi kweli wananchi wanafahamu maana na umuhimu wa Mwenge? Sisi tuliokwenda shule miaka ya 80 na 90, kabla ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, tulikuwa tukielezwa sana kuhusu Mwenge na kulazimika kuchangia. Lakini, watoto wetu wanaosoma sasa hivi wanaelewa chochote? Wanafahamu kuhusu historia ya Mwenge na Nyirenda kuuwasha juu ya Mlima Kilimanjaro? Wanajua kuhusu kauli ya amani, upendo, mshikamano na matumaini iliyotolewa na Baba wa Taifa? Wanamfahamu hata huyo Baba wa Taifa na umuhimu wa kuuzima Mwenge Oktoba 14?

Haya ni maswali ambayo nadhani ofisi husika inatakiwa kuyapatia si tu majibu, bali kuyafanyia mkakati ili Taifa lielewe maana ya Mwenge na umuhimu wake.

Hivi, watu wanajua kwamba Mwenge ni alama ya Taifa, na kwamba upo kwenye ngao ile ijulikanayo kama ‘Bibi na Bwana?’ Watu wanaelewa kwamba Mwenge ukifutwa, maana yake ni kwamba unakuwa umefuta historia ya nchi na huenda hata ile ngao ya Taifa itabidi ibadilishwe kwa kuwa imebeba alama za Taifa?

Kila siku nasema, kwanini hatuwi wabunifu? Kwani ni lazima kuukimbiza Mwenge kila mkoa, wilaya na kata kila mwaka? Hakuna njia nyingine mbadala ya kuelimisha watu juu ya Mwenge na maana yake kwa Taifa? Hakuna ubunifu wowote wa kusaidia hata watoto wetu kujua kuna kitu kinaitwa Mwenge wa Uhuru na umuhimu wake kwa Taifa? Ni lazima kukimbia tu kila mwaka? Yaani yale yaliyofanywa miaka ya 70 yaendelee kufanywa hadi leo?

Kama mbio hizi za Mwenge wa Uhuru zipo tu kufuata utaratibu wa kila mwaka bila ya wananchi kukumbushwa umuhimu wake na watoto kufundishwa maana yake, basi hakuna atakayekuwa na kosa atakayeuita Mwenge huo mtumishi hewa namba moja.

Mwisho…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles