23.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Lugumi hali tete

lugumi*Vigogo Mambo ya Ndani wahojiwa kwa saa saba

*Wapambe wake wafanya maigizo kwa waandishi Dar

NA WAANDISHI WETU, DODOMA/DAR ES SALAAM

SAKATA la mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi, limezidi kuwa tete baada ya vigogo wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhojiwa kwa saa saba na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) mjini Dodoma jana, huku mmiliki wake, Said Lugumi akiwapiga chenga waandishi wa habari Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA mjini Dodoma jana, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeishi Hilaly, alisema kamati yake iliwahoji vigogo wawili wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kwa sababu wao ndio watendaji wakuu.

Alisema watendaji waliowekwa kitimoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi (D/IGP), Abdulrahman Kaniki.

Aeshi alisema licha ya kuwahoji viongozi, suala hilo bado ni zito na kamati yake itatoa maazimio yatakayofikiwa leo saa sita mchana.

“Tumewahoji watendaji hawa wakuu wa wizara, suala hili bado zito tunawaomba muwe na subira kesho (leo), tutawapa taarifa za maazimio yatakayokuwa yamefikiwa na kamati yangu.

“Mpaka sasa kazi ni ngumu mno, tunaendelea kutafuta ukweli wa jambo hili, hawa walikuja na wataalamu wao.

“Kikubwa kila hatua ambayo tunafikia, lazima tumwarifu Spika wa Bunge ambaye ndiye anayetoa uamuzi juu ya jambo lolote linalohusu Bunge. Siwezi kusema lolote leo (jana), naomba mridhike na hili ninalowaambia kwanza,” alisema Aeshi.

Alipoulizwa Aeshi kama Lugumi ameitwa mbele ya kamati yake, hakuweza kuzungumza baada ya ofisa mmoja wa Bunge kumfuata na kuambiwa anaitwa kwa Spika.

KATIBU WA BUNGE

Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA ilipomtafuta Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah ambaye suala la Lugumi bado lipo PAC, alisema kamati hiyo, ikimaliza kazi yake itatoa taarifa za maazimio yaliyofikiwa.

KATIBU MKUU AGOMA

Waandishi walipomfuata Meja Jenerali Rwegasira ili kujua alichoitiwa na kuhojiwa na Kamati ya Bunge, aligoma kwa kusema hayuko tayari kuzungumzia suala hilo.

“Siko tayari kuzungumzia suala hili, kwanza nikiongea mnaninukuu vibaya kwa maneno ambayo sijasema,” alisema Meja Jenerali Rwegasira na kuondoka.

 

MAIGIZO YA LUGUMI

Jijini Dar es Salaam, mfanyabiashara anayemiliki kampuni hiyo, Said Lugumi, ameitisha mkutano wa waandishi wa habari uliogeuka kama maigizo baada ya ‘kupotea’ ghafla na badala yake wakaibuka waliotajwa kuwa wapambe wake.

Waandishi walijitokeza kwa wingi kwenye chumba cha mkutano kuanzia saa 5:00 asubuhi ambapo walitangaziwa kuwa mzungumzaji mkuu atakuwa Lugumi.

Wakati waandishi wakiandelea kumsubiri, mwandaaji wa mkutano huo, Benny Kisaka aliwaambia kuwa Lugumi na watendaji wake wamewasili eneo hilo, lakini kwa kuwa muda bado, wamekwenda ofisini kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Jambo Concept, Juma Pinto kwa ajili ya kusubiri muda ufike.

Katika hali ya kushangaza, Kisaka aliwakabili waandishi na kuwataka waondoke ukumbini, warudi saa 9:00 alasiri kwa sababu Lugumi na wenzake wana mazungumzo.

“Waandishi nawaomba muondoke mrudi saa 9, tena mzingatie muda ili tuwahi kumaliza tuendelee na majukumu mengine ya kazi,” alisema Kisaka.

Ilipofisa saa 9 mchana, alijitokeza Mhariri wa gazeti la Sauti Huru, Albert Kawogo na kuwaambia waandishi kuwa Lugumi amepata dharura, ameelekea mkoani Dodoma ambako ameitwa na viongozi wa Serikali na kuwataka wachukue taarifa iliyoandaliwa na waondoke eneo la mkutano.

Baada ya kusema hivyo, waandishi walimuuliza Kawogo, nani mwenye dhamana ya kujibu maswali ya waandishi yaliyoandaliwa kwa ajili ya Lugumi.

Akijibu, Kawogo alisema: “Hakuna mtu mwenye mamlaka ya kujibu maswali yanayomhusu Lugumi, nasisitiza mnapaswa kuondoka kwenye ukumbi, hakuna tena mkutano.

“Lugumi hawezi kuja tena kwenye mkutano huu, amepata dharura anakwenda Dodoma, ameitwa huko na viongozi wa Serikali, chukueni ‘press release’ muondoke, hakuna mkutano tena, mimi sina mamlaka ya kumjibia maswali yake, ndiyo maana ametoa press release, mtasoma humo.”

Alipomaliza kusema hayo, aligawa karatasi hizo kwa waandishi wa habari na kuondoka bila ya kutoa maelezo yoyote yanayohusu sakata hilo, hali iliyosababisha kujitokeza minong’ono ya waandishi wakihoji kwanini Lugumi hakutokea kwenye mkutano huo na Kawogo ni nani yake.

TAARIFA ILIYOTOLEWA

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Lugumi, Juma Sabury, ilisema Lugumi hahusiki na tuhuma zinazoelekezwa kwake.

Kampuni hiyo inadaiwa kuingia mkataba na Jeshi la Polisi mwaka 2011 na kupewa zabuni ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo 108 nchini kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Lakini hadi sasa, kampuni hiyo imefunga mashine hizo katika vituo 14 tu Dar es Salaam na kulipwa Sh bilioni 34 ambazo ni sawa na asilimia 99 ya fedha zote.

Taarifa hiyo ya Sabury inasema kampuni hiyo imetekeleza mkataba huo kwa kushirikiana na wabia wao.

Alisema kama kuna mgogoro katika utekelezaji wa mkataba huo, jeshi hilo lilipaswa kuwasilisha taarifa ya malalamiko kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili aweze kuingilia kati.

“Kwa mujibu wa mkataba wetu, hatupaswi kujitokeza hadharani kulalamika, tunatakiwa kuwasilisha malalamiko yetu kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), siyo sisi wala jeshi hilo,” alisema Sabury.

Sabury alikiri mwaka 2011, kampuni hiyo iliingia mkataba na jeshi hilo kwa kufunga mitambo  ya utambuzi kwa kutumia alama za vidole katika vituo vya polisi nchi mzima, vikiwamo vya Tanzania Bara na Zanzibar.

“Mkataba huu tuliutekeleza kwa kushirikiana na wabia wetu katika kuhakikisha mitambo hiyo inafungwa kwenye vituo hivyo,” alisema.

Alisema kumekuwa na tuhuma nyingi zinazotolewa kwenye vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii zikimhusisha Lugumi kuwa ametoroka nchini na kuwataka wananchi kuzipuuza akidai ni fitina tu.

“Said Lugumi hajawahi kutoroka wala kukamatwa nje ya nchi, yupo anaendelea na majukumu yake kama kawaida, hizo taarifa zinazosambazwa si za kweli, ni huzushi na kwamba zinapaswa kupuuzwa,” alisema.

TAKUKURU NA LUGUMI

Jalada la mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi limetua mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili uchunguzi zaidi.

Akizungumza na MTANZANIA juzi, Msemaji wa Takukuru, Tunu Mleli, alisema jalada la uchunguzi dhidi ya kampuni hiyo liko mikononi mwao na wakikamilisha watawasilisha kwenye mamlaka nyingine za kisheria kwa ajili ya hatua zaidi.

Taarifa hii imeandaliwa na Bakari Kimwanga (Dodoma), Patricia Kimelemeta na Grace Shitundu (Dar es Salaam)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles