23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

HIACE YATUMBUKIA BAHARINI, YAUA WAWILI

BAHARININA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WATU wawili wamefariki dunia baada ya kutumbukia baharini wakiwa ndani ya gari aina ya Toyota Hiace iliyokuwa imebebwa ndani ya Kivuko cha MV Kigamboni, Dar es Salaam.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea jana, wakati kivuko hicho kikipakia abiria katika kituo cha Magogoni.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Brown Mwakalago aliiambia MTANZANIA kuwa lilitokea saa 10 alfajiri ambapo mmoja wa waliofariki dunia ni dada yake, Nice Mwakalago (52) mkazi wa Tukuyu mkoani Mbeya.

Akisimulia tukio hilo, Mwakalago alisema walitoka Mbeya kuja Dar es Salaam kumzika kaka yao na wakati wanapatwa na tukio hilo walikuwa wanaelekea Kigamboni kumalizia msiba.

“Tulikuja kutoka Mbeya na gari aina ya Coaster iliyotufikisha hapa Kivukoni, tukashuka na kuingia kwenye kivuko. Tulikutana na Hiace ambayo ilikuwa inaelekea eneo la Vijibweni, tukapakia mizigo yetu ndani ya gari, tukaamua kukaa nje.

“Baada ya dakika kama moja hivi, wakati kivuko kinaendelea kupakia abiria, dada yangu Nice alisema anajisikia vibaya ndipo dereva wa Hiace akamwambia aingie ndani ya gari apumzike,” alisimulia.

Alisema baada ya muda waliona Hiace hiyo inaserereka kuelekea kwenye maji, wakaanza kupiga kelele lakini hawakufanikiwa kumwokoa.

“Tulishtuka kuona gari inaserereka kuelekea baharini, kwa sababu gari ilikuwa mbele na hakukuwa na kizuizi chochote cha kuizuia… tulipiga kelele, lakini inaonekana wahusika hawakusikia, hadi gari inatumbukia hakuna aliyetoka,” alisema Mwakalago.

UOKOAJI

Akielezea namna vikosi vilivyofanya kazi ya uokoaji, Mwakalago alisema licha ya kuwa eneo la tukio, walishindwa kuanza kazi kutokana na giza.

Alisema kibaya zaidi, timu ya waokoaji haikuwa na vifaa vya kufanya kazi kwenye mazingira hayo.

“Vikosi vya uokoaji vilikuja saa 11 alfajiri, havikuweza kuanza kazi ya uokoaji kutokana na giza, walilazimika kusubiri hadi kupambazuke ndiyo wakaanza kutafuta,” alisema.

Mrakibu Mwandamizi wa Polisi na Mkuu wa Kitengo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Brighton Monyo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kukiri kuwapo changamoto ya vifaa vya uokoaji ikiwamo darubini ya kusaidia kuona mbali.

“Tuliwahi eneo la tukio, lakini bado tuna changamoto ya vifaa vya uokoaji kama vile darubini ya kusaidia kuona mbali na badala yake wanatumia miwani ya kawaida ya maji na kulazimika kupapasa kwa kutumia mikono na kamba,” alisema Monyo.

Alisema licha ya changamoto hizo, walifanikiwa kupata mwili wa dereva wa gari iliyozama saa 3 asubuhi na walikuwa wanaendelea kutafuta gari na mwili wa Nice.

“Huko chini ya maji kuna matope, mawe makubwa, tunafanya kazi kwa kupapasa, tumeweza kuokoa mwili wa mtu mmoja ambaye anasemekana ndiye dereva wa gari iliyozama, mwili wake umepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa utambuzi zaidi,” alisema.

Jitihada za vikosi vya ukoaji kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Zimamoto, zilizaa matunda baada ya kufanikiwa kuokoa mwili wa Nice saa 7:27 mchana.

Akizungumza baada ya kuokoa mwili huo, Monyo alisema ulikutwa ndani ya gari ambayo ilizama mita 14 hadi 15 chini ya maji.

Katika eneo hilo, mkazi mmoja wa Kigamboni, Sigifrid Lyimo, alisema dereva aliyefariki dunia alikuwa rafiki yake ambaye alimtaja kwa jina moja la Dany.

“Leo (jana) saa 9 alfajiri alinipigia simu akaniambia ndiyo yupo Kivukoni anavuka, akifika atanijulisha. Muda ulizidi kwenda hadi saa 3 asubuhi ikabidi nimpigie simu, ikapokewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni askari polisi ambaye aliniambia rafiki yangu ametumbukia baharini.

“Nilishtushwa na kauli hiyo, sikumwamini, aliniomba nifike Kivukoni, nilipofika napiga simu haipatikani,” alisema Lyimo na kusisitiza kuwa rafiki yake ni mkazi wa Yombo Kilakala na ni baba wa mtoto mmoja.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndungulile (CCM), alifika eneo la tukio na kuzungumza  na vikosi vya uokoaji na kusisitiza kuwa atafikisha bungeni kilio chao cha kukosa vifaa.

“Nimezungumza na viongozi wa Wakala wa Umeme na Ufundi (TEMESA), tumeona bado kuna changamoto ya vifaa vya kuokoa na elimu bado inahitajika kwa abiria wa vivuko,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na Jonas Mushi, Esther Mnyika na Herieth Faustine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles