24.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Rais ngangari hawezi kukatishwa tamaa

Magufuli+PHOTONI takribani miezi mitano tangu tumpate Rais mpya wa Awamu ya Tano. Awamu ambayo inaongozwa na mtoto wa mfugaji tena  msomi mbobevu wa Sayansi Dk. John Pombe Joseph Magufuli.

Rais Magufuli ambaye kitaaluma ni Mwalimu mbali na kubebwa na historia yake ya nyuma inayomchora kama kiongozi mfuatiliaji na muwajibikaji, tangu apewe rungu la kuiongoza dola ameonekana kuwa kivutio kikubwa kwa wananchi hasa wala mlo mmoja kwa siku.

Mtindo wake wa uongozi wenye kubeba vionjo vya ‘Tumbua majipi’ siyo tu umemfanya awe maarufu kwa muda mfupi ndani ya Watanzania bali hata mataifa ya nje amekuwa gumzo vijiweni, maofisini, mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

Ni vigumu kutambua siri inayombeba Magufuli kuonekana anang’ara dakika za mwanzo wa mchezo japo dakika tisini si haba. Inawezekana ni namna anavyopiga chenga kuelekea kwenye nyavu kwamba kwa muda mrefu wananchi walikuwa wamemkosa mchezaji hodari ukizingatia waliyemtumainia alishatangulia  mbele ya haki.

Pamoja na uzuri wa Mheshimiwa Magufuli kucheza kwa kasi ili apate bao la mapema ndani ya dakika tano za mwanzo, naanza kupatwa na wasiwasi kwa namna mashabiki wake wanavyomshangilia huku wakipiga vuvuzela badala ya  kuangalia ni wapi mchezaji huyu anaweza kujikwaa na kupata maumivu.

Nasikitika sana maana tangu Rais Magufuli aanze kuongoza nchi pamekuwapo na kauli nyingi kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwamo wananchi wa kawaida, viongozi wa dini, wasomi  na wanasiasa kwa ujumla wanaodai kuwa kiongozi huyu atiwe moyo ili asije akakata tamaa.

Kwenye tamasha la Pasaka lililoandaliwa na Msama Promotions na kufanyika Machi 27, mwaka  huu katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye alikuwa  mgeni rasmi katika  tukio hilo Nape Nnauye alisema Watanzania wamuunge mkono Rais katika harakati zake ili asikate tamaa.

Wakati Nnauye akisema hayo,  hata viongozi wengine kama Mwenyekiti wa Wazazi wa CCM Taifa, Abdalah Bulembo na msemaji wa chama hicho, Sendeka kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisisitiza hivyo kwamba Rais asikatishwe tamaa.

Si hao tu waliosema hivyo bali  hata shirikisho vyuo vya elimu ya juu Seneti Mkoa wa Dar es Salaam liliwahi kutoa  tamko lake kwa kumuhakikishia, Dk. Magufuli kuwa watashughulika na yeyote atakayejaribu kupanga kuihujumu au kuikwamisha Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake hususani ya kupambana na ukwepaji kodi, ubadhirifu na usimamizi wa uwajibikaji kwa nguvu zote.

Hizo ni miongoni mwa kauli chache  ambazo zimetolewa kwa siku za hivi karibuni kama njia mojawapo ya kumuunga mkono Rais anayeonekana kuchukia machukizo yanayowachukiza wachukizwaji.

Kimsingi kila binadamu hapa duniani mwenye damu na nyama  akifanya jambo jema hujihisi vizuri  akipewa motisho za vitu au nyama ya ulimi ili aweze kusonga mbele na hii ndiyo asili ya maumbile yetu.

Lakini pamoja na binadamu kuhitaji kutiwa moyo katika safari yake, kuna haja ya kuchukua tahadhari katika mazingira ambayo yanaweza kusababisha mtu huyo asipate nafasi ya kukosolewa walau kidogo.

Wahenga waliosema, ‘Mgema akisifiwa tembo hulitia maji’  hawakukosea  maana  binadamu aliyezaliwa na mwanamke asipopata changamoto  katika maisha mara nyingi hubweteka na kujikuta akiboronga.

Sisemi kuwa ni vibaya kumpongeza Rais katika harakati zake ukizingatia nchi yetu maji yalikuwa yamefika shingoni, lakini itakuwa ni makosa makubwa kiongozi huyu kumchukulia kama Malaika Gabrieli kwamba kila jambo analolifanya ni sahihi.

Ni  kutomtendea haki Rais kumchukulia kama yai lisilostahili kutikiswa ili kuepuka lisipasuke, kumbe lingetikiswa kati ya mayai mengi ndipo tungegundua ubora wake kama linafaa kwa matumizi.

Muigizaji, mtangazaji, mwanasiasa na Mwandishi wa habari raia wa Uingereza, Mark Thomas aliwahi kusema, ukosoaji ni mrejesho wa yale unayoyafanya ili kujua kama uko sahihi au la.

Kwa mantiki hiyo kama wananchi hawataki kuona Rais akikosolewa ni hatari sana kwani kiongozi huyu anaweza kutumbukia kwenye shimo ambalo watu wake walikuwa wanafahamu lakini wakanyamaza wakidhani kwa kufanya hivyo ni kumlinda. Thomas anaendelea kusema kuwa ukosoaji ni mfumo wa mawasiliano kwa maana ya kwamba wakosoaji hutaka kukupa mrejesho wa kile unachokifanya kwao, ndiyo kusema ni fursa kwako kujifunza zaidi kuhusu watu unaowafanyia kazi na kujua namna ya kuwapa utoshelevu.’’

Je, ni kwa namna gani Rais ataweza kujipambanua kama yuko sahihi au la kama kila anayetaka kumkosoa ataoneka ni msaliti asiyemtakia mema ? Ni kwa namna gani kiongozi huyu atapata nafasi ya kujifunza mambo mapya kama kila jambo alifanyalo litaonekana ni mvinyo ?

Madhara ya kutomkosoa kiongozi ni makubwa kuliko watu wanavyofikiria. Ikumbukwe Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete kabla na wakati anaingia madarakani wananchi wengi walisahau kuwa ni  binadamu na kubakia wanambatiza majina ya utukufu badala ya kumkosoa kama njia ya kumsaidia.

Ben R. Mtobwa katika kitabu chake cha ‘Kikwete safari ya Ikulu’ ukurasa wa 28 hadi 40  ameonyesha baadhi ya wananchi waliotoa mtazamo wao kuhusu ujio wa Kikwete. Prince M. Bagenda  ‘Kikwete ni mtu mstaarabu,’ Kajubi Mukajanga: “Namfahamu JK kama mtu mcheshi, rahisi kuingilika (accessible) na kuongea naye, mwenye tabasamu muda wote, lakini pia mtu madhubuti anayejiamini.

Wengine ambao hawakuficha hisia zao ni Methodius Kilaini  sasa hivi  Askofu Msaidizi Kanisa Katoliki  Jimbo  la Bukoba, “Kikwete ni chaguo la Mungu, kwani maombi yetu ya muda mrefu yamesikika” na Moses Kulola aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT sasa Marehemu: “Tunamkubali Kikwete kama mtu wa watu na Mungu ametuchagulia, nipo tayari hata kampeni”

Hakika binadamu ni popo, wazabizabina na wazandiki maana wengi waliompongeza Rais Kikwete na kumuona kama mafuta ya senene huku wakishindwa kumuonyesha njia sahihi hatimaye  wamekuwa wa kwanza kumlaumu makanisani, misikitini na kwenye vyombo vya habari kwamba ameharibu nchi.

Kuna msemo usemao, ‘Ukubwa ni jaa’ hivyo Rais Magufuli usiwachukie wanaokukosoa, kukubeza na hata kukutukana  mwishowe ukaamua kuwaziba midomo kwa kuwafungia magazeti, luninga na  redio  bali uwapende maana wanakusafishia njia. Kumbuka wanaokusifia  bila kukuonyesha njia mwisho wa siku wanaweza kugeuka Yuda Iskariote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles