DANIEL Mtuka ni Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki ambalo awali lilikuwa likiongozwa na Kaptein Mstaafu John Chiligati. Mtuka aliweza kuibuka na ushindi wa kura 33,012 katika Uchaguzi Mkuu uliopita huku mpinzani wake kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Emmanuel Alute akipata kura18,281.
MTANZANIA limefanya mahojiano na Mtuka ambaye pia alipata kuwa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. Endelea…
MTANZANIA:Â Hebu tueleze historia yako ya kiutendaji kabla hujaingia katika siasa?
MTUKA: Nilikuwa mtumishi wa umma katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) tangu mwaka 1998 hadi 2015.
Niliteuliwa kuwa Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mbeya na kufanya kazi kwa muda wa miaka mitatu na baada ya hapo nilihamishwa na kuteuliwa kuwa Kamanda wa taasisi hiyo Kanda Maalumu Mkoa wa Dar es salaam.
MTANZANIA:Â Ni changamoto gani ulizokumbana nazo ulipokuwa Takukuru?
MTUKA : Hapa nitaelezea kwa urefu kwa sababu changamoto nyingi zipo kwenye chombo hiki hasa kwa upande wa utendaji na mazingira hasa rasilimali fedha pamoja na vitendea kazi kama magari kwa ajili ya kufuatilia taarifa mbalimbali tunazoletewa.
Fedha za kujaza mafuta kwa ajili ya kwenda kufanya oparesheni kwa mfano mtu anachukua rushwa katika eneo ambalo lipo pembezoni mwa mji, ni kazi kubwa kwa sababu huwezi kufika eneo hilo bila usafiri.
Changamoto nyingine ni utoaji wa taarifa zisizo kamili ambazo zinatolewa nusu nusu hali inayosababisha kushindwa kufuatilia kutokana na kwamba wananchi ni wachache wanaojitolea kwenda kutoa ushahidi mahakamani hasa katika kesi za rushwa za kuomba na kupokea ambazo mara nyingi ushahidi wake ni lazima mtoa taarifa awe tayari kwenda mahakamani kwa sababu watuhumiwa wanaokamatwa wapo kwenye mtego.
Changamoto nyingine ni ucheleweshwaji wa kibali kutoka kwa Mkurungenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP) wakati tunapotaka kupeleka kesi mahakamani.
Kifungu cha (15) cha sheria namba 11 cha mwaka 2007 kinataka Takukuru kupeleka jalada la uchunguzi, ukishakamilika kwa DPP ili ajiridhishe na akishajiridhisha arudishe Takukuru ndipo ipeleke kesi.
Kosa la kuomba na kupokea rushwa  kifungu cha (57) cha sheria namba 11 ya mwaka 2007 ya Takukuru kinatakiwa kirekebishwe kwa sababu kina mapangufu.
MTANZANIA: Unadhani nini kifanyike ili kutokomeza rushwa?
MTUKA: Rushwa ni tatizo lakini kuna mpango wa kutokomeza katika nchi yetu, kuna vituo vimeanzishwa kwa ajili ya elimu juu ya rushwa na watu wana uelewa wa jambo hili.
Kikubwa kinachotakiwa ni kurekebisha kifungu cha (25) cha rushwa ya ngono cha sheria namba 11 nwaka 2007 ambavyo adhabu iliopo ni ndogo.
Adhabu ya rushwa ya ngono faini isiyozidi Sh milioni tano au kifungu cha miaka isiyozidi mitatu au vyote kwa pamoja.
MTANZANIA: Katika utendaji wako uliwahi kushughulikia kesi za rushwa ya ngono?
MTUKA : Katika hilo watu hawana ushirikiano wala sijawahi kupata kesi kama hiyo katika Mkoa wa Dar es Salaam hawasemi ila nikiwa Mbeya niliacha kesi ikiwa mahakamani kwa sababu mlengwa alitoa ushirikiano kwa Takukuru.
MTANZANIA: Ni kitu gani ambacho hutakisahau ulipokuwa Takukuru?
MTUKA: Kwanza najivunia na sitaweza kusahau katika maisha yangu, niliweza kusimamia jengo la Takukuru makao makuu Upanga ambalo gharama ilipangwa kwenye tenda Sh bilioni 41.
Kwa mujibu wa tathimini ya tenda haikuongezeka fedha yoyote zaidi ile iliyopangwa ya Sh bilioni 41 ni nadra sana kuongeza katika ujenzi wa jengo hadi leo, huwa nikiliona najivunia sana.
MTANZANIA: Ni kitu gani kilichokusukuma ukaingia kwenye siasa?
MTUKA: Kwa kuwa nilitumia Serikali nikaona sasa ni wakati wa kuwatumikia wananchi wa Manyoni Mashariki.
MTANZANI: Unauzungumziaje mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopita kwa upande wako?
MTUKA: Mchakato wa uchaguzi mwaka jana ulikuwa mgumu kwa sababu kulikuwa na mwamko, wanaopenda kuwa wanasiasa walikuwa wengi.
Katika kura ya maoni ndani ya chama washiriki tulikuwa wengi, kulikuwa na vita kwenye chama na ukimaliza huku lazima tena kushindana na wapinzani.
Hii ni mara ya pili nashiriki kwenye Uchaguzi Mkuu, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2010 ambapo nilishindwa kwenye kura za maoni na nikashika nafasi ya pili lakini mwaka jana nilipambana na nikafanikiwa kupita kwenye kura za maoni.
MTANZANIA: Unauzungumziaje mchakato wa upitishaji wa majina katika kura za maoni ndani ya CCM?
MTUKA: Ni wa kawaida lakini chama kinatakiwa kufuata mapendekezo ya wananchi na chama kisiweke mtu ambaye wanamtaka wao.
Chama ngazi ya Kata, Wilaya, Mkoa hadi Taifa wawe wanaacha matakwa ya wananchi wasibadilishe jina la aliyeshinda kwenye kura ya maoni kwa sababu wenye maamuzi ni wananchi.
MTANZANI: Ulikumbana na changamoto gani wakati wa kampeni?
MTUKA: Changamoto nilizokumbana nazo ni mchuano mkubwa, timu, rasilimali, magari ya kuzungukia maeneo mbalimbali kumbuka Jimbo la Manyoni Mashariki ni kubwa huwezi kumaliza kwa siku kumi walizopanga .
Changamoto nyingine ni suala la fedha ambalo ni tatizo kwenye siasa kwa Watanzania, ukimaliza kutoa sera zako unasikia wanakwambia mheshimiwa unatuachaje…ninawaomba wapiga kura wabadilike fedha si maendeleo bali kilicho muhimu ni sera.
MTANZANIA: Ulitumia kiasi gani cha fedha katika kampeni zako?
MTUKA: Nilitumia zaidi ya Sh milioni 20. Tayari nimerejesha kwenye chama kuna fomu maalumu ambazo huwa tunajaza matumizi uliyotumia kwenye kampeni.
MTANZANIA: Msajili wa vyama vya siasa alitoa bajeti ya kuanzia Rais, Mbunge na Diwani, kuna fedha ambazo anatakiwa kutumia kwenye kampeni, je huoni kama umepitiliza kiwango?
MTUKA: Inategemeana na ukubwa wa jimbo, ukinipangia bajeti kuwa nitumie kiasi fulani itakuwa kichekesho zaidi kwa sababu tugharamia vitu kama mafuta, kula na magari ya kukodi hapo lazima gharama iongezeke.