25.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Kwaheri Kibonde 

1972 – 2019

Na ANDREW MSECHU

-DAR ES SALAAM

PIGO jingine sekta ya habari. Ndivyo unaweza kusema baada ya Kampuni ya Clouds Media Group (CMG) kumpoteza mtangazaji wa kipindi cha Jahazi, Ephrahim Kibonde (47) siku chache baada ya kifo cha Mkurugenzi wake wa Vipindi na Uzalishaji, Ruge Mutahaba.

Kibonde ambaye alikuwa MC kwenye msiba wa Ruge, amekutwa na umauti jana alfajiri katika Hospitali ya Bugando mkoani Mwanza.

Mtangazaji huyo alikuwa miongoni mwa waombolezaji waliomsindikiza Ruge hadi katika maziko yake wilayani Bukoba.

Taarifa za msiba huo zilithibitishwa na uongozi wa Clouds Media pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.

“Mtangazaji wa Clouds Fm, Kibonde amefariki dunia hapa Mwanza, alianza kusumbuliwa na presha alipokuwa Bukoba kwenye msiba wa marehemu Ruge Mutahaba na kuhamishiwa Mwanza,” alisema Mongella.

Taarifa ya awali iliyotolewa na Mkuu wa Vipindi wa Clouds FM, Sebastian Maganga, inaeleza kuwa taratibu zinafanyika kupanga mipango ya msiba huo.

“Ni pigo kubwa kwa familia ya Clouds Media Group, kwa familia ya Kibonde. Lakini kama tulivyoshikamana kwenye msiba wa Ruge, naomba tushikamane kwenye msiba huu,” alisema Maganga.

HOSPITALI YA BUGANDO

Taarifa iliyotolewa jana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Thomas Rutachunzibwa, ilieleza kwamba jana saa 11:30 alfajiri, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, ilipokea mwili wa marehemu Kibonde.

“Ndugu Kibonde aliugua ghafla akiwa kwenye mazishi ya Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media (Ruge Mutahaba), alipata matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Kagera, baadaye Hospitali ya Uhuru jijini Mwanza na wakati akipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa matibabu zaidi umauti umekumkuta njiani.

“Tunatoa pole kwa ndugu jamaa wa Ephrahim Kibonde na familia ya Clouds Media na Watanzania wote,” alisema Dk. Rutachunzibwa katika taarifa yake.

KUSAGA: TUMEZIDISHIWA MAUMIVU

Akizungumzia kifo cha Kibonde, Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga, alisema wamepoteza mtu mwingine muhimu katika uendeshaji wa vipindi, muda mfupi baada ya kumpoteza Ruge.

Alisema Kibonde alikuwa mfanyakazi mwenye bidii na aliyejituma, ambaye aliondoka kumsindukiza mkuu wake wa kazi lakini bahati mbaya naye hakurudi.

“Kwa kweli ni pigo kubwa kwetu. Tukiwa bado tuko kwenye majonzi haya ya kumpoteza Ruge, Kibonde naye anatuacha tena. Inaumiza sana, ila mapenzi ya Mungu yatimizwe.

“Kwa sasa ofisi inashughulikia kusafirishwa kwa mwili wa Kibonde kutoka Mwanza ambapo utawasili saa nne usiku (jana) na kupelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, kwa ajili ya taratibu za maziko zinazoandaliwa na familia yake,” alisema.

Kusaga alisema mwili wa Kibonde unatarajiwa kuzikwa Jumamosi.

BABA MZAZI AZUNGUMZA

Baba mzazi wa Kibonde, Samson Kibonde alisema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwanaye.

Alisema alipata taarifa za mwanaye kuugua ghafla akiwa katika maziko ya Ruge huko Bukoba Jumatatu wiki hii na aliendelea kupewa matumaini na madaktari kuwa hali yake inaendelea vizuri, hadi usiku wa jana alipoelezwa kuwa amefikishwa katika Hospitali ya Bugando.

“Tuliendelea kuambiwa kuwa madaktari wa Bugando wameshagundua tatizo la uvimbe tumboni, kwahiyo wanashughulikia tatizo hilo.

“Tukapewa tumaini kuwa ni tatizo linalotatulika. Bahati mbaya alfajiri ya leo (jana) tukapata taarifa kuwa ameaga dunia,” alisema.

Alisema maziko ya Kibonde ambaye ni mtoto wao wa pili yatafanyika kabla ya kumalizika wiki hii, lakini uamuzi rasmi utatolewa kupitia vikao vya familia leo baada ya mwili wake kuwasili Dar es Salaam jana usiku.

WAFANYAKAZI WENZAKE

Mtangazaji George Bantu ambaye alikuwa akiendesha kipindi cha Jahazi pamoja na Kibonde, alisema anakumbuka kwa mara ya mwisho alizungumza naye siku aliyokuwa akiondoka kwenda Kagera kwa ajili ya maziko ya Ruge.

“Kwa upande wa kipindi tumekosa mtu muhimu. Alikuwa mtu wa aina yake, mcheshi, mwenye aina ya kipekee ya sanaa ya kukosoa na kuchagiza mada kwa namna ya kumfanya msikilizaji avutwe kuendelea kusikiliza kipindi,” alisema.

Alisema kwake yeye anaona amempoteza mwalimu, kaka, rafiki na mfanyakazi mwenzake, ambaye sasa anampa hamasa ya kutekeleza majukumu yake kwa nguvu zaidi ikiwa ni sehemu ya kumuenzi.

Mtangazaji B Dozen alisema Kibonde alikuwa mjuzi wa mambo mengi ambaye alikuwa kama kioo chake kutokana na tabia yake ya kutokuwa na kinyongo.

“Nakumbuka wakati akiondoka kwenda Kagera, neno la mwisho nilimwambia ‘be strong’ kwa sababu alionekana mwenye majonzi sana. Alikuwa ni rafiki na aliweza kukaa na watu wa aina zote, naona hilo ndilo lililomjenga zaidi,” alisema.

ALILIWA KILA KONA

Kutokana na kifo cha mtangazaji huyo mahiri wa redio na vipindi mbalimbali vya mashirika ya umma ikiwamo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Watanzania mbalimbali wakiwamo viongozi na wasanii wamemlilia.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alitoa pole kwa familia na uongozi wa Clouds Media Group kutokana na msiba huo.

“Innalillahi Wainna Ilaihi Rajiun. Huu ni msiba mzito kwa familia ya wanahabari. Poleni Clouds, ni njia yetu sote lakini baada ya msiba wa Ruge kwenu huu ni mtihani Allah huwaletea waja wake. Mitihani huwapima imani, hii ni njia mojawapo ya kukumbusha na kupima imani watu,” alisema Bashe.

Alisema anawatia moyo Clouds, lakini pia hasa familia na watoto wa marehemu ambao wamepoteza baba na Mwenyezi Mungu amjalie pumziko la amani na heri.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Kibonde.

“Nimepokea habari za kifo cha Ephraim Kibonde kwa masikitiko makubwa sana. Pole zangu kwa familia ya Kibonde na familia, Clouds Media kwa msiba huu. Kazi ya Mola haina makosa na wafiwa Mungu awapitishe salama katika mtihani huu mkubwa,” alisema Zitto.

Mbunge wa Iramba Magharibi, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema kutokana na msiba huo anatoa pole kwa familia ya marehemu na Clouds Media.

“Umetangulia kaka, pole Clouds Media, poleni wanafamilia kwa msiba huu mzito. Sisi tulikupenda sana, ila Mungu amekupenda zaidi, pumzika kwa amani kaka yetu na rafiki yetu Ephrahim Kibonde, Mungu wa faraja anyooshe mkono wake awape faraja ya kweli familia ya Kibonde na ndugu zetu Clouds Media,” alisema.

Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule (Chadema), alisema habari ya kifo cha Kibonde imemshtua sana.

Mwanahabari Maulid Kitenge, alisema kuwa ametoka mbali na Kibonde wakati wa uhai wake na msiba huo uliomfika ni kazi ya Mungu.

“Tumetoka mbali sana Ephrahim Kibonde. Mungu amekuchukua ni kazi yake Mola haina makosa,” alisema.

WASANII

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Abwene Yesaya ‘AY’, alisema ameshtushwa na taarifa za kifo cha Kibonde.

“Nimeshtushwa sana na taarifa ya kifo chako kaka yangu, pumzika kwa amani kaka yangu Ephrahim Kibonde. Tumeshirikiana kwenye mengi ya kikazi na familia, pumzika kwa amani wakukaja. Tusali sana hatujui siku wala saa, mbele ni giza ila sala ndio taa,” alisema.

Judith Wambura ‘Jaydee’ alisema msiba huo ni jambo zito kwa wote wenye ukaribu wa Kibonde.

“Hili ni jambo zito kwa watu wenye ukaribu na Ephraim Kibonde. Tunakaa tunakunywa, tunacheka siku nyingine mmoja wetu anatwaliwa.

“Mwenyezi Mungu wa rehema ukawafariji watoto, ndugu, jamaa na marafiki kwa pigo hili. Tunashukuru kwa kila jambo, RIP my brother (shemejiiii),” alindika Jaydee katika ukurasa wake wa Instagram.

MWISHO WA SAFARI

Machi 4, mwaka huu kwenye mazishi ya Ruge Mutahaba yaliyofanyika katika Kijiji cha Kiziru, Bukoba mkoani Kagera, Kibonde ndiye aliyekuwa mtangazaji wa shughuli za mazishi zilizokuwa zikiendelea na hapo mwisho wake ulianza kudhihiri.

Akiwa msibani hapo, inaelezwa kuwa Kibonde alianza kujisikia vibaya wakati wa shughuli za mazishi ya mfanyakazi mwenzie, rafiki yake wa muda mrefu Ruge.

Kibonde alianza kuishiwa nguvu na dada wa marehemu Ruge alimsaidia kwa kushirikiana na baadhi ya watu waliokuwepo karibu na kumwingiza ndani na kuanza kumpepea.

Alipoona hali inazidi kuwa mbaya, dada huyo alimwita Dk. Isack Maro ambaye ni mtangazaji wa kipindi cha Njia Panda na Afya Cheki kwa ajili ya huduma ya kwanza.

Dk. Maro alimpatia huduma ya kwanza na kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.

Siku ya pili (Jumanne), ilibidi wenzake waliokuwa wana ratiba ya kusafiri kurudi Dar es Salaam baada ya kumaliza maziko, walilazimika wamwache Bukoba ili aendelee na matibabu zaidi.

Akiwa anaendelea na matibabu hospitalini hapo, hali yake ilizidi kuwa mbaya, wakafanya uamuzi wa kumwamishia Hospitali ya Uhuru jijini Mwanza, na wakati akipelekwa Hospitali ya Bugando jana asubuhi kwa matibabu zaidi umauti ukamkuta.

ATABIRI KIFO CHAKE

Akiwa katika mahojiano na Michuzi Media Group wakati wa msiba wa Ruge, Kibonde alitamka maneno ambayo yalionekana ni wazi kama utabiri wa kifo chake.

“Turudi kwa Mwenyezi Mungu na kukumbuka kwamba sisi binadamu hatuna lolote katika ulimwengu huu. Kama si leo kesho, kama si keshokutwa huwezi jua muda gani na siku gani wakati wako utafika, nawe safari yako itakuwa imefika,” alisema Kibonde.

MSIBA WA MKE WAKE

Kibonde amefariki dunia ikiwa imepita mwaka mmoja tangu alipofiwa na mke wake Julai 10, mwaka jana.

Mke wa Kibonde, Sara Kibonde alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam na kuzikwa Julai 14, mwaka jana katika makaburi ya Kinondoni.

Sara alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani hadi umauti unamkuta.

 Juzi zikiwa zimepita saa chache tangu alipozikwa Ruge, katika ukurasa wa mtandao wa Instagram, Kibonde aliposti picha ya marehemu mke wake bila kuandika maneno yoyote.

Sara katika maisha yake ya ndoa na Kibonde walifanikiwa kupata watoto watatu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,526FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles