22.7 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Jaji awachia kina Mbowe kwa hoja tisa

JNi baada ya kukaa mahabusu kwa miezi mitatu

KULWA MZEE Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

NDEREMO na vifijo vimetawala Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, baada ya mahakama hiyo kutamka kwamba rufaa ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko ya kupinga kufutiwa dhamana imeshinda nzima nzima na warufani waachiwe huru kwa dhamana mara moja.

Hukumu hiyo ilitolewa jana mbele ya Jaji Sam Rumanyika baada ya kusikiliza hoja za rufaa iliyokatwa na kina Mbowe dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini na majibu ya mawakili wa Serikali.

“Ni bahati mbaya sana rufaa hii ina miezi mitatu na siku saba mahakamani, ndio inaamuliwa leo (jana) pamoja kwamba ilifunguliwa chini ya hati ya dharura,” hayo aliyasema Jaji Rumanyika saa saba kamili alipoanza kusoma hukumu.

“Rufaa hii nzima nzima imeshinda, warufani waachiwe huru kwa dhamana mara moja, naamuru kumbukumbu zote za mahakama ya chini zirudi ili kesi iendelee kusikilizwa.

“Kwa aina hii ya kesi na mazingira yake warufani waripoti kila mwisho wa mwezi mahakamani, wasisafiri bila kibali cha mahakama, masharti mengine yatabakia kama yalivyo.

“Mahakama ya chini kutoa amri ya washtakiwa kuripoti polisi kila Ijumaa ya kila wiki ni kukimbia majukumu yake,” Jaji Rumanyika.

Alisema kufuta dhamana ya washtakiwa si tu kwamba haikuwa sahihi, bali ni uamuzi uliofikiwa kabla ya muda, haukupaswa kutekelezwa kwani kama ni kuzaliwa mtoto basi ni njiti.

“Kufutwa kwa dhamana hakukupaswa kufanyika, hii rufaa mpya iliyonistaajabisha kuliko rufaa zingine nilizowahi kuziona, kama msingi wa jumla mamlaka za mahakama, majaji na mahakimu kuamua kuhusu dhamana za washtakiwa mamlaka zao ziko kisheria, utashi utumike kwa tahadhari.

“Kwa maoni yangu majaji na mahakimu wanapoangalia kufuta dhamana kwa washtakiwa wazingatie misingi tisa kwamba kesi inadhaminika, kutoa dhamana ni tafsiri dhahiri ya mahakama ya dhana ya katiba ya kuwa mtu hana hatia mpaka mahakama itakapomhukumu vinginevyo, kufuta dhamana kunahitaji sababu kubwa kuliko sababu za kumpa mtu dhamana .

“Nne mahakama izingatie ukubwa wa kosa kutoa masharti ya dhamana , masharti ya dhamana yawekwe bila kuleta hisia kuwa mpango ni kunyima mtu dhamana, mahakama izingatie adhabu kwa makosa yaliyopo mbele yake ili pale ambapo mshatakiwa akitiwa hatiani asiwe ameadhibiwa mara mbili.

“Sababu ziwe zinakubalika mahakama yeyote duniani, mahakama izingatie msongamano uliopo gerezani na je kutoa dhamana au kufuta dhamana kunachangia au kupunguza msongamano gerezani na tisa mahakama izingatie kuwa uhuru wa mshatakiwa hauna mbadala,” alisema Jaji Rumanyika.

Jaji Rumanyika alisema ni hatari mahakama kushindwa kutoa sababu kwanini inamnyima mshtakiwa dhamana na ni hatari inapofuta dhamana bila sababu za msingi wakati dhamana ni faraja ya kimahakama, aliyeitoa hawezi kuichukua kwa matakwa yake.

“Kutokana na viapo vilivyowasilishwa mahakamani kusapoti warufani wafutiwe dhamana, warufani hawakupewa nafasi ya kuwasilisha kiapo kinzani, hawakusikilizwa, viapo hivyo vyote na yaliyomo vinaondoshwa katika kumbukumbu za mahakama nchini.

“Warufani hawakuwasilisha kiapo kinzani bado mahakama iliendelea kusikiliza hoja zote wakati pale ambapo hakukuletwa kiapo kinzani inapaswa kusemwa yale ya kisheria tu na yale ya ukweli wa mambo atawaachia wengine lakini katika kesi hii yote yalizungumzwa,” alisema Jaji Rumanyika.

Alisema dhamana ni mkataba wa utatu kati ya mahakama, washtakiwa na wadhamini, kama mkataba ndio huo, pale anaposhindwa kufika mahakamani mshtakiwa, mdhamini akashindwa kutoa sababu kwanini fungu lake la dhamana lisichukuliwe, hapo dhamana ya mshtakiwa inaweza kufutwa.

“Amri ya kufuta dhamana inakuja baada ya fungu la dhamana kuchukuliwa kama si hivyo ni sawa na kufunga mkokoteni mbele ya punda badala ya nyuma,”alisema.

Warufani waliwakilishwa na jopo la mawakili akiwemo Peter Kibatala na Jeremaya Ntobesya huku Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, Paul Kadushi, Wakili wa Serikali Jackline Nyantori, Simon Wankyo na Salim Msemo.

Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana Novemba 23, mwaka jana. Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine wanaoshtakiwa nao katika kesi ya jinai namba 112 ni Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk.Vincent Mashinji.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari mosi na 16 mwaka 2018.

SALUM MWALIMU

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, amesema Mahakama Kuu imeonyesha ni kimbilio la haki kwa kusahihisha mahakama za chini zinazokosea.

Akizungumza makao makuu ya chama hicho Kinondoni Dar es Salaam jana, alisema walikuwa na imani kubwa ya kushinda kwani waliamini mahakamani ni mahala patakatifu pa kutafsiri sheria.

“Hukumu ni hukumu ingawa tulikuwa na imani kubwa ya kushinda, Mahakama Kuu imeonyesha ni kimbilio la haki kusahihisha pale mahakama za chini zinapokosea,” alisema Mwalimu.

Hata hivyo alisema Mbowe na Matiko watazungumza na vyombo vya habari mwishoni mwa wiki hii kuwaeleza Watanzania kile walichopitia.

“Miezi mitatu si midogo kukaa ndani, tunadhani ili tuwapate wakiwa vizuri tuwaache watulie na mwishoni mwa wiki tutakutana na vyombo vya habari.

“Mwenyekiti anahitaji kupewa ‘briefing’ ya vitu vilivyoendelea wakati alipokuwa hayupo na akija kuzungumza atakuwa na taarifa za kutosha,” alisema.

KIWANGA, LIJUALIKALI

Anaripoti Ashura Kazinja kutoka Morogoro, kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imetupilia mbali ombi la kupinga dhamana lililotolewa na upande wa Jamhuri dhidi ya wabunge Suzan Kiwanga na Peter Lijualikali pamoja na wanachama saba wa Chadema.

Mahakama hiyo ilitupilia mbali shauri  hilo baada ya kujiridhisha kuwa maombi yaliyotolewa na upande wa Jamhuri si halali na hayakukidhi vifungu vya sheria, baada ya kuweka kifungu kisichoendana na  kutoa dhamana kwa washtakiwa hao kwa masharti mawili.

Wabunge hao Suzan Kiwanga wa Mlimba na Peter Lijualikali wa Kilombero na wafuasi wengine saba wa Chadema wamepatiwa dhamana kwa masharti ya kila mmoja  wao kuwa na wadhamini wawili, mmoja akisaini bondi ya Sh milioni 3.750 na wa pili awe na mali isiyohamishika na yenye thamani ya Sh milioni tano.

Awali wakili wa upande wa utetezi Hekima Mwasifu, aliiomba mahakama hiyo kutoa dhamana yenye masharti nafuu kwa washtakiwa hao kutokana na makosa yote yanayowakabili kudhaminika.

Akitoa uamuzi mdogo Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro, Elizabeth Nyembele, alisema anakubaliana na upande wa utetezi kuwa kiapo hicho kina mapungufu katika kusikiliza pingamizi hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulishindwa kuonyesha kifungu maalumu katika kutetea ombi lao na kwamba kifungu walichotumia ni elekezi tu.

Hakimu Nyembele alisema shauri la upande wa Jamhuri la kuitaka mahakama kutumia mamlaka yake katika suala hilo si sahihi, kutokana na kwamba mahakama si wakati wote inaweza kutumia mamlaka yake kutenda haki, kuamua kutoa dhamana.

Hata hivyo wabunge hao pamoja na wenzao saba wamerudishwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 22, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,580FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles