28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

KUOSHA MIGUU SOKONI YAWA DILI DAR

Mjasiriamali, Sarafina Mohamed, anayeosha miguu ya watu waliochafuka na tope katika Soko la Mabibo (mahakama ya ndizi) akihudumia wateja wake kwa Sh 500, Dar es Salaam jana. Picha na LOVENESS BERNARD

 

 

NA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

MVUA inayoendelea katika jiji la Dar es Salaam na kusababisha masoko mengi kujaa tope na uchafu mwingine, imegeuka kuwa fursa kwa vijana na wanawake ambao wamejipatia ajira ya kuosha miguu watu wanaokwenda kununua mahitaji mbalimbali sokoni.

Juzi MTANZANIA lilishuhudia watu wanaotoka ndani ya soko la Mabibo maarufu ‘mahakama ya ndizi’ lililopo Wilaya ya Ubungo wakiosha na wengine kuoshwa miguu yao kwa   ujira wa  kati ya Sh 100 na Sh 500.        

Mmoja wa wabunifu hao, Sarafina Mohamed, aliliambia MTANZANIA jana kuwa ameamua kufanya kazi hiyo baada ya mvua kuanza kunyesha mfululizo na kuathiri biashara yake ya awali ya kuuza maji ya kunywa maarufu kama ‘maji ya kandoro’ pamoja na sigara.

“Kutokana na miundombinu ya soko kuwa mibovu na matope kuwa mengi ambayo yanasababisha wateja kuchafuka, nilibuni njia hii ambayo inanipatia hadi Sh 30,000 kwa siku.

Hata hivyo alisema baada ya wenzake kuona anapata wateja wengi, waliamua kumuiga na kuanzisha ‘kijiwe’ kingine kama hicho sokoni hapo.

 “Nilikuwa nauza maji ya kandoro na sigara ndani ya soko baada ya mvua kuwa kubwa biashara hiyo ikakosa wateja hivyo nikawa nawaza wateja wanavyotoka sokoni hapa wakiwa wachafu na kuchafua wengine pamoja na magari wanayotumia,” alisema Sarafina.

Alisema alianza kama majaribio na ndipo aligundua kuwa kazi hiyo inampa kipato kizuri kila kukicha hasa mvua ikinyesha.

“Tofauti na nilivyokuwa nauza maji ya kunywa kipato changu kimeongezeka kwani kwa siku naingiza hadi Sh 30,000.

“Mteja akinawa mwenyewe analipia Sh 100 lakini ninapomnawisha analipa Sh 500, hivyo anapokwenda nyumbani au kupanda daladala anakuwa msafi na hachafui wengine,” alisema Sarafina.

Alisema amekuwa akinunua maji kwa kila ndoo moja Sh150 na mara nyingi hutumia Sh 9,000 kwa siku kununua maji.

“Nimeweza kutoa ajira kwa vijana wanne ambao hunisaidia kufuata maji bombani na wateja wanapokuwa wengi huwanawisha pia,” anasema Sarafina.

Alisema kwa kazi hiyo inamsaidia kununua sare za shule za watoto wake na pia husaidia hata chakula kwa familia yake hata kama mume wake atapungukiwa.

“Imenijengea uwezo wa kuhifadhi fedha kila siku Sh 20,000 hivyo ninaamini msimu wa mvua ukiisha nitakuwa na fedha nyingi ambazo zitaniwezesha kufanya biashara nyingine kubwa,” alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles