24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

KUMBUKA: SIASA INAWEZA KUNIPA UKATIBU MKUU UN

Kumbuka akiwapungia mkono wageni waliohudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu maswala ya kisheria uliofanyika mjini
Geneva, Uswisi mwaka jana

 

Na EVANS MAGEGE,

JINA la Lameck Kumbuka halina umaarufu mkubwa katika medani za siasa za nchi hii, lakini limepata kuonekana katika makala mbalimbali za kimataifa zinazochapishwa kwenye magazeti tofauti tofauti hapa nchini.

Huyu ni kijana ambaye ni mzaliwa wa Ngara mkoani Kagera, kwa sasa anaishi mjini Geneva nchini Uswisi akifanya kazi na mashirika mbalimbali ya kimataifa.

Kumbuka ni miongoni mwa wagombea 431 waliojitokeza ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania nafasi ya uwakilishi wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Jina lake lilikwama katika hatua ya mwanzo kwa kuwa alikuwa ni miongoni mwa watu ambao hawakufanikiwa kupita kwenye chujio la CCM katika kinyang’anyiro hicho.

MTANZANIA Jumapili lilipata fursa ya kufanya naye mahojiano ikiwa ni saa chache kabla ya kupanda ndege na kurejea nchini Uswisi.

Katika mahojiano hayo maalumu, Kumbuka alizungumza mambo mengi, kubwa likiwa ni kiu yake ya siasa za nchi hii kwa kusema kwamba kupitia CCM anaamini siku moja atakuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN).

MTANZANIA Jumapili: Umetoka nchini Uswisi kwa lengo la kushiriki mchakato wa kuwania nafasi ya uwakilishi wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kupitia (CCM). Nini kilichokusukuma kuja kuwania nafasi hiyo?

KUMBUKA: Ni imani ya sasa inawapa watu kujiamini kwamba hata nisipoweza sasa nina imani mchakato utakaotumika utakuwa huru na haki.

Kwa sababu mchakato utakuwa huru na haki basi nami ninaweza nikaenda kwa sababu nikikosa itakuwa ni haki yangu kukosa na nikipata itakuwa ni haki yangu kupata.

Na ndio maana uligundua kwamba kwa mara ya kwanza wagombea waliojitokeza ndani ya chama ilikuwa ni zaidi ya mara 10 ya wagombea waliokuwa wanajitokeza mwanzo.

Hali hiyo inatokana na sababu vijana wengi wana imani kwamba katika uongozi wa Mwenyekiti wetu Rais Magufuli, amejitahidi kukiweka chama kuwa cha haki kwa masikini na watu wote ambao wana nia njema na nchi.

Sababu nyingine ni kujiamini kwamba mimi najua ninatosha katika nafasi hiyo kwa kigezo cha elimu yangu, uzoefu wa kikazi kama ninavyokwambia ninaongea Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Kihispania, pia nimewahi kufanya kazi na mashirika ya Umoja wa Mataifa kwenye kambi za wakimbizi wa Burundi na Rwanda, naongea lugha nane.

Nina shahada ya uzamili katika masuala ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa na shahada nyingine ya Uzamili ya Sheria (LLM),  nimefanya kazi na makampuni mengi ya kimataifa. Nimefanya kazi na UN, nimefanya kazi na Msalaba Mwekundu (RED CROSS), pia, nimefanya kazi katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania UN kule Geneva.

Nimefanya kazi na Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) n.k, kwa hiyo nikichanganya uzoefu huo najiona ni mtu sahihi kuwania ubunge wa EALA ili kupigania masilahi ya nchi yangu kimataifa.

MTANZANIA Jumapili: Kutokana na imani yako na jinsi idadi kubwa ya watu walivyojitokeza kuwania nafasi ya ubunge wa EALA, ni kweli demokrasia imekua ndani ya CCM?

KUMBUKA: Naamini kwamba demokrasia ndani ya chama na mikakati ya kukijenga upya chama ili kiwe na watu wa aina tofauti tofauti hasa vijana wanaoaminika kukipeleka chama mbele kwa sasa ipo zaidi ya huko nyuma tulikotoka.

Huu si mtazamo wangu tu, hata vijana wengine wengi wanatambua hilo na ndio maana walikuwapo zaidi ya 400 waliojitokeza.

MTANZNAIA Jumapili: Umeingia kwenye ulingo wa siasa, nini hasa unacholenga katika ulingo huo?

KUMBUKA: Nimeingia kwenye ulingo huu kwa sababu hatujawahi kuwa na Mtanzania wa mfano ambaye yuko kwenye nafasi za juu za katika Umoja wa Mataifa (UN).

Kwa mfano hatujawahi kuwa na Mtanzania ambaye ni Katibu Mkuu wa UN kama ilivyokuwa kwa Kofi Annan kutoka Ghana.

Hatujawahi kuwa na Mtanzania ambaye ni Kamishna katika kitengo cha UNHCR kama ilivyokuwa kwa Katibu Mkuu wa sasa wa UN, Antonio Guterres ambaye amekuwa Kamishna wa juu wa UNHCR kwa miaka mingi, pia amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Ureno kwa hiyo kama umebobea vizuri katika mambo ya kimataifa na nchi yako ikakutambua na ikakupa nafasi katika utawala, kwa mfano uwe waziri wa mambo ya nje, waziri katika nafasi yoyote au mbunge na una elimu ya kutosha na ushawishi mbele za watu pia uwezo mkubwa wa kutengeneza mtandao utachaguliwa tu.

MTANZANIA Jumapili: Unaamini kwamba kupitia CCM unaweza kuwa Katibu Mkuu wa UN?

KUMBUKA: Kuna namna nyingi si tu kupitia CCM, ila inawezekana kabisa na hiyo mimi nailenga tena kwa muda mrefu sana na hata kama ikitokea isipatikane lakini iwapo nafasi moja kubwa kabisa ndani ya UN ambayo ninaweza nikasimama naamini ninaweza.

Na ujue hizi zote ni nafasi za kisiasa na historia inaonyesha mtu pekee ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa UN bila kupitia siasa za nchi yake ni Kofi Annan, lakini wengine wote walipita kwenye siasa za nchi zao kwanza.

MTANZANIA Jumapili: Umesema una uwezo wa kuzungumza lugha nane, umeeleza pia umeishi na kutembelea  nchi nyingi sana. Je, ulipenda kujifunza hizo lugha?

KUMBUKA: Kwa tabia yangu napenda sana kuongea na ninapokutana na watu ninajihadhari nisiweze kuyatawala maongezi kwa sababu huwa ninaamini kuwa busara ipo kwenye kusikiliza na si kuongea. Kwa hiyo ninaweza kusema sina aibu ya kuongea hivyo popote ninakokwenda napenda kujifunza lugha ya eneo hilo.

MTANZANIA Jumapili: Unaishi nchini Uswisi kwa miaka saba sasa, vipi ushiriki wako na Watanzania wengine katika kuleta maendeleo hapa nchini?

KUMBUKA: Watanzania hawako wengi, nimefanya na mashirika ya kimataifa huko, Watanzania hawapatikani katika ajira za jumuiya mbalimbali za kimataifa. Wakati Tanzania inatoa ada ya uanachama wa UN lakini ukijiuliza Watanzania wanaifaidi vipi, je, ni uwezo mdogo wa kujielekeza kwenye fursa za kimataifa? Nimepata kujiuliza maswali mengi.

Unaweza kuhudhuria mkutano wa jumuiya fulani ya kimataifa, ukijitambulisha kama ni Mtanzania kuna wakati unajikuta watu wanakushangaa na kutaka kupiga picha nawe kana kwamba wewe ni maonyesho, hali hiyo inatokana na ukweli kwamba hakuna Watanzania wanaojichanganya katika mambo hayo.

Unaweza kukuta kitengo fulani ndani ya jumuiya moja ya kimataifa ina wafanyakazi zaidi ya 500 au 600, ukiuliza kuna Watanzania wangapi unaweza usipate hata mmoja.

Lakini ukiuliza Wanyarwanda wako wangapi unaweza kuambiwa wako hata watano, Wanigeria utaambiwa wako hata 10, Waganda utaambiwa wako 10.

Sasa hapa kuna swali huwa najiuliza, kwanini nchi itoe ada ya uanachama wa UN lakini bado wananchi wake wasichangamkie fursa kuifaidi ada ya nchi vizuri?

Mazingira yako kwa sisi Watanzania kupenya na kushiriki ajira za mashirika ya kimataifa na fursa hiyo inaweza kusaidia maendeleo ya nchi yetu maana sisi Waafrika utamaduni wetu ni kusaidiana.

MTANZANIA Jumapili: Lakini katika nchi hizo mabalozi wa Tanzania si wapo nini ushiriki wao katika kupigia debe fursa za ajira kwa Watanzania?

KUMBUKA: Kama mabalozi wapo  wana majukumu mengi, lakini pia wana mchango mkubwa sana kutafuta fursa kwa Watanzania, inategemea vitu vingi kama ushawishi na ufadhili nchi inayotoa katika miradi.

Marekani, nchi za Ulaya Magharibi,  Scandnavia  na China zinafadhili mara nyingi sana UN, hivyo raia wake wanapewa kipaumbele.

Lakini bado kuna idadi ya uwakilishi kutoka nchi zinazoendelea na hizo nafasi ndio inabidi Watanzania wazichangamkie kwa nguvu zote. Nafasi nyingine ni makubaliano pia.

Lazima uwepo muda, utashi na rasilimali za kuwezesha ushawishi wa kumshawishi  kiongozi yeyote mfano Mkurugenzi wa kitengo fulani cha UN kwa kumwambia taarifa zenye utafiti kuwa labda kitengo chake hakina Mtanzania hata mmoja anayefanya kazi lakini kuna Wakenya watano au Wanigeria 50, lakini Tanzania ina wataalamu kadhaa wenye uwezo wa kufanya kazi za kitengo chako.

Na akamwambia wape nafasi za ajira Watanzania hao ili nasi tukupe ofa ya kukupigia kura katika uchaguzi fulani. Unajua viongozi wa mashirika ya kimataifa hupatikana kwa kupigiwa kura na mabalozi au wawakilishi kutoka nchi wanachama.

Kwa mfano kwa sasa tunahangaika kumpata Mkuu wa Shirika la Afya Duniani na tungefurahi huyu rais wa Ethiopia anayegombea ashinde ili tuwe na Mwafrika kwa sababu Margareth Chan anayemaliza muda wake ni Mchina na Mcanada.

Kwa hiyo mtu anayeteuliwa kuwa balozi ana nafasi ya kutumia kura yake katika maamuzi yoyote yale ya kimataifa kama keki kwa Watanzania wote.

Napenda kukuhakikishia kuwa ajira kwenye mashirika ya kimataifa zipo nyingi sana kinachotakiwa Watanzania wenyewe kuzichangamkia na ikifika sehemu msaada wa mabalozi unahitajika hapo ndilo jukumu lao ni kuwatafutia fursa Watanzania.

MTANZANIA Jumapili: Kwa hiyo unamaanisha kuwa mabalozi wetu hawana ushawishi wa kuwatafutia Watanzania ajira kwenye ngazi za kimataifa?

KUMBUKA: La hasha, nimesema kuna mambo mengi kama mchango na ushawishi wa nchi husika japo mabalozi nao wana nafasi yao inapofikia hatua fulani. Balozi hawezi kukuandalia CV (wasifu) na kukutafutia tangazo la kazi.

Kikubwa Watanzania tujiamini, tuwe na uthubutu wa kuingia katika masuala ya kimataifa kwa sababu unaweza kumwona mkurugenzi fulani wa shirika la kimataifa ukahisi ana uwezo wa kukupatia kazi kumbe kuna mtu mdogo chini yake anasimamia mfano mradi uliodhaminiwa na Serikali ya Oman na huyo akakupa kazi hata ya miezi mitatu ukaanzia hapo. 

Unajua UN ndiyo ina wadau sasa kama inapatikana fursa ya namna hiyo wenzetu wazungu wanajua kubebana kwa sababu wanapenda kufahamu mipango ya miradi mbalimbali ijayo hivyo huwataarifu watu wao wa karibu hasa wanafunzi wajifunze masuala yatakayoendana na miradi hiyo.

Nimekwambia unakuta kuna shirika fulani la UN labda linataka kwenda kufanya kazi Oman miaka mitatu ijayo, unakuta mzungu anamwambia nduguye ajifunze Kiarabu na pia ajifunze taaluma itakayoendana na mambo yatakayofanyiwa kazi katika utekelezaji wa mradi huo. Kwa mantiki hiyo zinapotangazwa nafasi za kazi, unakuta kazi inawatafuta wao kwa sababu wameshajiimarisha kielimu na kiujuzi, wanabebana kiakili sana.

Lakini pia mabalozi wetu nalilia sana wapewe baadhi ya mafungu, inawezekana wanatamani sana kusaidia baadhi ya watu wao lakini lile fungu kidogo la kusaidia halipo.

MTANZANIA Jumapili: Kwa mujibu wa maelezo yako je, hayo mazingira yanadhihirisha balozi zetu zina ukiritimba?

KUMBUKA: Siwezi kusema zina ukiritimba lakini kuna mambo mawili hapa, Watanzania wenyewe wanaoishi kule wamejiwekea fikra za kujitenga na hawataki kutembelea ubalozi tofauti na nchi nyingine ambapo watu wake hupenda kutembelea ubalozi wao mara kwa mara.

Naweza kusema elimu ya Watanzania ni ndogo kwa sababu kuwa watu wanaamini baadhi ya sekta zimeundwa kwa ajili ya watu fulani tu.

Lakini mimi sijui huu uthubutu nimeutoa wapi kwa sababu huwa naamini hata kesho ninaweza nikawa rais ingawa nimetoka katika familia ambayo haijawahi kuwa na mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa kwa sababu huwa sina ile kasumba ya kuamini watu fulani wao lazima waweze mimi nisiweze.

Nawashauri vijana wajiamini na wathubutu kwa kila fursa hata wakikukosa wasikate tamaa. Wasipothubutu watu wa nje watakuja kwetu na kuchukua fursa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles