23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MIAKA 53 YA MUUNGANO WA DAMU NA CHOKOCHOKO ZA VIONGOZI

Mwalimu Nyerere akichanganya mchanga Zanzibar na Tanganyika ikiwa ni ishara ya muungano baina ya mataifa hayo

 

Na Tobias Nsungwe,

WATANZANIA wana kila sababu ya kujivunia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwani umewafanya watu wa Tanzania na visiwani kuwa kitu kimoja. Ni ukweli usiofichika kwamba watu wengi wa visiwa vya Pemba na Unguja  asili yao ni mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Kwa hiyo Jumatano ijayo nchi itakuwa inasherehekea miaka 53 ya Muungano wa watu wenye asili na damu moja ambao hapo awali walikuwa wametenganishwa na minyororo ya ukoloni na au mabadiliko ya kijiografia. Si dini wala rangi inaweza kuwatenganisha watu wa Bara na visiwani kwani wanaunganishwa kwa ushemeji, uwifi, ujomba au itikadi za kisiasa. Ndio maana vyama vyote vya siasa lazima viwe na wanachama kutoka pande zote za muungano.

Mwaka jana Rais Dk. John Magufuli, aliagiza Watanzania kusherehekea siku hiyo kwa kupumzika nyumbani au kufanya kazi zao nyingine. Alifuta utaratibu wa kuadhimisha siku hiyo kwa magwaride ya jeshi na halaiki za wanafunzi.

Mwaka huu sherehe hizo zitafanyika makao makuu ya nchi, Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri. Mgeni rasmi atakuwa Rais Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (JWTZ). Safari hii kunatarajiwa kuwa na gwaride la jeshi letu na maonesho mengine kama ilivyo kwa miaka yote.

Muungano huu umepitia misukosuko mingi lakini mara zote imejidhihirisha wazi kwamba wananchi wa kawaida toka pande mbili wanajihisi kuwa watu wa nchi moja. Ndio maana wanafanya biashara pamoja, wanasafiri pamoja, wanafanya kazi pamoja, wanasoma pamoja, wanasali pamoja na zaidi ya hayo wanaoleana. Si jambo la ajabu tena kuona kijana toka visiwani Zanzibar akimuoa binti toka mkoani Iringa, Kagera au Mbeya au mwenyeji wa Kilimanjaro akimuoa binti toka Pemba au Nungwi! Kwa jinsi hii muungano hasa miongoni mwa wananchi wa kawaida unazidi kuota mizizi.

Huzisikii kelele za kutaka kuhatarisha uhai wa muungano kutoka kwa wananchi.

Tunaambiwa kuwa zaidi ya Wazanzibari 500,000 wanafanya biashara zao Tanzania Bara na pia wapo wananchi wengi toka bara walioweka makazi yao visiwani. Katika miaka ya karibuni inaonekana kwamba wakati wananchi wengi wanauvutia ndani muungano ni viongozi ndio wamekuwa wakiuvutia nje. Baadhi ya kauli na matendo ya viongozi ndio vimekuwa vikichochea mawazo ya kuuchukia muungano.

Ili muungano wowote ujengeke katika misingi imara, lazima kila upande ukubali kupoteza hiki na kupata kile na kukubali kutoa sadaka kwa ustawi wa nchi iliyoundwa baada ya nchi mbili huru kuungana. Ni kama ndoa… Katika  hadithi ya ndoa mume na mke wanakuwa wamekubaliana kutoa sehemu ya uhuru wao ili kufanikisha uhusiano huo uwe wa kudumu. Akitokea mmoja wao akataka apewe uhuru wake wote, basi ujue ndoa iko hatarini!

 Na muungano ni hivyo hivyo. Haiwezekani sehemu moja ya muungano ipewe uhuru wake wa awali halafu muungano uendelee. Si rahisi hata kidogo! Katika siku za hivi karibuni umezuka mjadala mkali kutaka ifafanuliwe kama Zanzibar ni nchi au la.

 Tanganyika na Zanzibar zilifunga ‘ndoa’ mwezi Aprili mwaka 1964 na hivyo zote kupoteza hadhi zake kama nchi (sovereignty) na kuzaliwa nchi ambayo sasa inaitwa Tanzania. Wakati tunasherehekea miaka 53 ya muungano wetu tusisahau kwamba Zanzibar imegawanyika sana hasa baada ya utata kuhusu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais mwaka 2015 na matokeo ya chama cha CUF kususia uchaguzi wa marudio mwezi Marchi 2016.

Hali hiyo imeifanya CCM kuunda Serikali peke yake huku Baraza la Wawakilishi likijaa kijani tupu. Hili si jambo la kujivunia hata kidogo kwani ukweli ni kwamba chama cha CUF kina ushawishi mkubwa sana katika visiwa vya Unguja na Pemba. Hali ya kisiasa iliyopo visiwani kwa sasa inazidi kupandikiza hisia za ubaguzi na hasa kuuchukia muungano. Nasema wanaohubiri kuuchukia muungano si wananchi bali baadhi ya viongozi.

  Baadhi ya viongozi wa Zanzibar ama kimya kimya au kwa uwazi wamekuwa wakililia visiwani kuwa nchi kamili. Tayari wamedai wimbo wa taifa wamepata. Wametaka bendera sasa wanayo. Na kinachoendelea sasa ni baadhi ya viongozi kutaka Zanzibar kuwa nchi huku wakiorodhesha visingizio kibao kama kutaka kuifanya Zanzibar kuwa Singapore au Dubai ya Afrika!

Malumbano haya ya baadhi ya Wazanzibari kutaka wapewe hadhi ya kuwa nchi kamili yanachagizwa sana na baadhi ya viongozi wa Zanzibar ingawa siku zote huwa hawataki kujionyesha wazi. Viongozi hawa hujivisha joho la muungano pale wanapolinda masilahi yao hasa ya kulinda vyeo vyao ndani ya Serikali au chama.

Ajabu ya wengi wa viongozi wanaohubiri ubaguzi wakistaafu utumishi wa umma au kwenye vyama vyao wanajenga nyumba zao na kuweka makazi yao ya kudumu Tanzania bara hususani Dar es Salaam au Dodoma.

Alipokuwa akihutubia Bunge mwezi Novemba mwaka juzi, Rais Magufuli aliapa kuulinda muungano. Alitamka wazi kutambua juhudi za waasisi wa taifa hili yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume na mchango waliotoa katika kuunda taifa hili linaloitwa Tanzania.

Rais Magufuli alisema pia kwamba angepambana na wote waliokuwa na nia ya kuwagawa Watanzania kwa misingi ya dini, eneo, ukanda, rangi, itikadi au ukabila. Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, naye ametamka mara nyingi kwamba ataulinda na kuuenzi muungano.

Wiki hii wakati tunasherehekea muungano ni wakati wa viongozi wetu wakuu kutafakari jinsi ya kutatua kile kinachoitwa kuwa ni kero za muungano. Ni wakati pia wa kutafakari jinsi ya kutatua matatizo ya kisiasa visiwani Zanzibar kwani ndiyo yanayoamsha hisia za kuununia muungano mara kwa mara.

Ni wakati wa CUF kutafuta njia ya kumaliza mgogoro wa ndani ili baadaye warudi kundini kushiriki katika ujenzi wa taifa kwa kushirikiana na wenzao wa CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi na vyama vingine. Ni wakati pia wa kufikiria mustakabali wa nchi yetu ambayo bado inakabiliwa na changamoto za uchumi, kisiasa na usalama wa ndani. Matukio ya askari kuuawa, hofu ya ugaidi, watu kutekwa na tishio la njaa yatutafakarishe sikukuu kama hizi.

Hakuna wa kuwatenganisha watu wa Tanzania Bara na visiwani kwani ni kitu kimoja na wameishi kwa amani kwa miaka mingi. Wanasiasa waache kujenga hisia za ‘usisi’ Tanganyika au mawazo ya kujitenga visiwani. Viongozi wa kisiasa waache kuuchokonoa muungano huo kwa visingizio vyovyote vile kwani ni vigumu kuuvunja muungano wa damu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles