24.1 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

KUBWA KULIKO ILIVYOCHOCHEA SAFARI MABADILIKO YANGA

NA MOHAMED KASSARA

MWANGA umeanza kuonekana, ndivyo unaweza kusema, baada ya klabu ya Yanga  kufanya harambee yake iliyopewa jina la ‘Kubwa Kuliko’ kwa mafanikio makubwa, kutokana na kukusanya mamilioni ya fedha taslimu na pamoja na ahadi kutoka kwa wadau mbalimbali wa michezo.

Mbali na fedha zilizochangwa, harambee hiyo ilikuwa jukwaa muhimu katika kuchochea safari ya mabadiliko ya uendeshaji kuelekea kwenye mfumo wa  kisasa zaidi.

Harambee hiyo iliyofanyika Jumamosi iliyopitab katika Ukumbi wa  Diamond  Jubilee jijini  Dar  Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa pamoja na wadau wa soka nchini.

Mgeni Rasmi katika hafla hiyo, alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete alikuwa miongoni mwa wageni wa heshima walioalikwa katika dhifa hiyo.

Hafla hiyo pia ilihudhuruliwa na Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dkt, Harison Mwakyembe na Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda na wabunge mbalimbali mashabiki wa timu hiyo.

Katika harambee hiyo, zaidi ya milioni 900 zilichangwa, zikiwa pesa taslimu pamoja na ahadi mbalimbali kutoka kwa wadau.

Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz aliahidi kuchangia  Sh milioni 200, Kampuni ya GSM, iliahidi kutoa Sh milioni 300, Rais Kikwete Sh milioni tano, Kamati ya Hamasa Sh milioni 50, Kamati ya Utendaji Sh milioni 50 na wabunge mashabiki wa Yanga Sh milioni 40.

Mbunge wa CCM, Mariamu Ditopile Sh milioni moja, Mbunge Afrika Mashariki Sh milioni  1.4, wanawake mashabiki Yanga, Sh milioni moja huku Makonda akiahidi kuipa Yanga ardhi eneo la Kigamboni.

Mpango wa kuichangia klabu hiyo   ulianzishwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kamati ya Hamasa

Mwinyi Zahera ambaye aliwataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuichangia kiasi cha Sh bilioni 1.5 ili zitumike kufanya  usajili wa msimu ujao.

Harambee kwa ajili ya kuichangia klabu hiyo ilizinduliwa jijini Dodoma kabla ya kuhitimishwa jana.

Fedha hizo zitatumika kujenga kikosi imara cha timu hiyo kwa msimu ujao, kulipa mishahara ya wachezaji pamoja na kusadia shughuli za uendeshaji.

Ikumbukwe kuwa Yanga inapitia kigumu tangu kujiweka pembeni kwa aliyekuwa mwenyekiti wao, Yusuf Manji, ambaye alikuwa akitoa fedha kuiendesha timu hiyo.

Tangu kuondoka kwa Manji, Yanga imeshindwa kupata fedha za kusajili wachezaji wazuri na kulipa mishahara, hali iliyosababisha kupokwa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na watani zao, Simba mara mbili mfululizo.

Harambee hiyo ni matumaini pekee kwa klabu  hiyo kutafuta njia mbadala ya kuiendesha timu hiyo kisasa.

Hata viongozi walioalikwa walitumia jukwaa hilo kutoa ushauri kwa uongozi mpya kuhusu kutafuta vyanzo endelevu vya kupata fedha, bila kupitisha bakuli kwa wanachama.

Majaliwa aishauri Yanga ifuate nyayo za Simba 

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema huo ni mwanzo mzuri wa klabu ya Yanga katika kutafuta mfumo mzuri wa uendeshaji wake kama ilivyo kwa wapinzani wao Simba, ambao tayari wamehama kutoka ule wa kadi za uanachama na kuwa umiliki wa hisa.

Majaliwa ambaye, aliichangia Sh milioni 10, aliwataka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo pia kujitokeza kuisaidia.

“Niwapongeze kwa kumalizi ligi mkiwa katika hali mbaya ya kiuchumi, lakini mkiwa katika utulivu wa hali juu, nizitake klabu nyingine  zijifunze kwenu namna ya kuendesha timu bila kuwa na uchumi mkubwa.

  “Hata hivyo nawaomba mtafute njia ya kupata mapato endelevu,nafahamu Yanga na Simba ni klabu kubwa na kongwe nchini na ndizo zenye wanachama na mashabiki waliopungua milioni 20 nchini kote au zaidi, hata hivyo bado hazijaweza kutumia vema fursa ya kuwa na mashabiki wengi katika kuvifanya vilabu vyetu viweze kujitegemea kiuchumi.

“uongozi mpya pamoja na wanachama bado mnajukumu la kuhakikisha amnafanya stadi ya kutosha kujua ni mfumo gani wa uwezekezaji utakaofaa,ili Yanga iweze kujiendesha kisasa zaidi ,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kikwete apigia mstari mabadiliko 

Katika hafla hiyo ,Rais Mstaafu, Kikwete aliutaka uongozi wa klabu hiyo, chini ya Msolla kutengeneza mfumo mzuri wa kuendesha klabu hiyo kisasa zaidi, huku akiwaasa kutoirudisha klabu katika yale iliyopita.

Kikwete ambaye alikuwa mgeni maalumu katika hafla hiyo, alitumia sehemu kubwa hotuba yake kuwaasa viongozi  kutafuta mikakati ya kuiendesha klabu hiyo kisasa pamoja na kuwekeza kwenye soka la vijana.

“Msolla na wenzako, nyinyi ni viongoziu wapya mliochaguliwa, hakikisheni mnaleta usasa katika klabu, tengenezeni mifumo mizuri ya kuiendesha timu ili tusirudi tulipokuwa huko nyuma.

“Wekezeni kwenye soka la vijana ili kupunguza gharama za usajili, hapo zamani tulikuwa na timu nzuri ya vijana  kama hawa kina Sunday (Manara), Mohamed Rishard, Kassim Manar na wengineo, msipowekeza kwa vijana, mtatumia gharama kubwa kusajili wachezaji wa kigeni na makocha kutoka nje,”alisema Kikwete.

Kamati ya Hamasa yatoa mchongo

MwenyekitI wa Kamati ya Hamasa na Uchangishaji ya Yanga,  Anthony Mavunde,  alisema wamependekeza kwa uongozi kuanzisha wiki maalum itakayoitwa ‘Wiki ya Mwananchi’, itakakayokuwa maalum kwa ajili ya wapenzi na wanachama wa Yanga kuitumikia jamii.

Alisema wiki hiyo itakuwa ikifanyika mwezi Agosti kila mwaka na siku ya kilele chake kutafanyika tukio kubwa litakalofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam likiambatana na utambulisho wa wachezaji wao wapya.

Wiki hiyo itaambana na mchezo mmoja wa kirafiki na timu kutoka nje kwa ajili ya kupata fedha, kama wanavyofanya watani zao ,Simba katika tamasha la Simba Day, ambalo limekuwa likiwaingizia fedha ya kutosha kila mwaka.

Simba chini ya mwenyeki wake wakati huo, Hassan Dalali, mwaka 2008, iliasisi tamasha hilo kama chanzo mbadala cha kupata fedha za kuendesha baadhi ya mambo ndani ya klabu hiyo.

“Tumepanga tuwe na Wiki ya Mwananchi’, ambapo wanachama wa Yanga watafanya usafi maeneo mbalimbali kama,hospitali, masoko na kutoa misaada mbalimbali, kabla ya kwenda uwanjani kushuhudia  wachezaji wapya wa timu yao, wakicheza na moja ya timu  kubwa ya Afrika.

Alisema watamuomba Rais, John  Magufuli  awe mgeni rasmi mwaka huu.

 Msola anena mazito

Mwenyekiti wa Yanga, Msolla alisema tayari klabu hiyo imeanza kufanya tathimi ya nembo ya klabu hiyo ili kujua dhamani  yake halisi kabla ya kwenda katika utaratibu wa kujiendesha kisasa.

Alisema mbali hivyo, watahakikisha wanafufua matawi yao yote kwa ajili ya kuongeza wanachama wapya watakaoiongezea pato klabu hiyo.

“Tumeanza mara moja kutathimini dhamani ya nembo ya Yanga ili tukipata mdhamini tujue itakuwaje,lakini pia tuna mpango kabambe wa kukarabati jingo la klabu ili  kuhakikisha wachezaji wetu wanaishi katika jingo hilo msimu ujao.

“Jengo letu pale Jangwani lina vyumba 28 vya kulala, tunatarajia kuvikarabati vyote viwe katika ubora wa hali ya juu ili kupunguza gharama za kupanga hoteli,”alisema Msolla.

Mengine yaliyojiri

Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe alitumia jukwaa hilo kwa kuzitaka  timu kutotumia idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni  katika mchezo mmoja.


“Msimu ujao nataka kuona sheria zinabadilika hasa kwa wachezaji wa kigeni ambao watacheza, ukisajili wachezaji 100 wa kigeni hatuna tatizo ila watakaocheza uwanjani hawatazidi watano ama wanne, na hili nitalisimamia kwa ukaribu.

“Sheria zipo na hazifuatwi, hakutakuwa na ruhusa kwa timu ambayo haina timu ya vijana kushiriki Ligi Kuu Bara, tunataka tujenge timu bora ya Taifa, lazima uwekezaji uwe mkubwa,” alisema Mwakyembe

Katika hafla hiyo, Yanga ilimtatangaza kumsajili mshambuliaji Juma Balinya kutoka Polisi ya Uganda.

Balinya, ndiye kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Uganda iliyomalizika hivi karibuni, akifunga mabao 19.

Awaki mshambuliaji alihusishwa na Simba , kabla ya jana  Yanga kumtambulisha kuwa mchezaji wao mpya.

Pia klabu hiyo ilimtambulisha kiungo Abdurlazizi Makame, baada ya  kumsajili kutoka Mafunzo ya Zanzibar.

Wachezaji wengine ambao wame mwaga wino  Jangwani licha ya  jana kutotambulishwa nini mshambualiaji, Maybin Kalengo kutoka Zambia, Sadney Urikhob (Namibia) na Patrick Shibomana kutoka Rwanda.

Wengine ni beki raia wa  Ghana Lamine Moro , Issa Bigirimana na Seleman Moustafa,  wote kutoka Burundi.

Naye mwanachama mwandamizi wa klabu hiyo, Mwigulu Nchemba aliahidi kushusha kifaa cha nguvu wakati wowote, kama alivyofanya kwa kiungo Feisal Salum (Fei toto).

Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba na Magharibi na Waziri wa Zamani wa Mambo ya Ndani, msimu uliopita aliipa Yanga Fei toto kama mchango wake kwa timu hiyo.

Fei toto alisaini kuijunga na Singida United, lakini baadae Nchemba ambaye pia Rais wa klabu hiyo alimtoa Yanga.

” Kama ilivyokuwa kwa Fei toto, nilimsajili kama sehemu ya mchango wangu kwa Yanga, mwaka huu litakuwepo jembe moja ambalo tayari tumeshamalizana, tutamtangaza siku atakapokuja kufanya kazi kama Fei toto. alisema  Nchemba.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza la Udhamini wa Yanga, Mama Fatma Karume aliwaasa viongozi wa vyama vya soka nchini kuacha kutafuta umaarufu kupitia soka, badala yake waweke mbele maendeleo ya mchezo huo.

Alisisitiza timu za mpira wa miguu lazima zitumike kuwaunganisha Watanzania na sio kutumika kuwagawa.

“Niwaombe viongozi wa vyama vya mpira waache kutafuta umaarufu, wala wasitufanye tukawa na uhasama, mimi nakumbuka Hayati Mzee, Karume aliwahi kuinunulia Yanga nyumba, lakini alifanya hivyo pia kwa Simba, viongozi wa sasa wajifunze kupitia hayo,” alisema Mama Karume.

Mastaa wa zamani hawakuwa nyuma

Mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Sunday Manara aliwataka viongozi wa klabu hiyo kuthamini mchango wa wachezaji wa zamani wa timu hiyo, kwa kuwapa nafasi angalau mbili kwenye Kamati ya Utendaji.

Alisema wachezaji wa zamani wa timu hiyo wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mbalimbali, lakini uongozi na wanachama wamekuwa wagumu kuwasapoti.

“Wachezaji wa zamani hatuthaminiwi, wengi wetu tupo katika mazingira magumu, tunashindwa kumudu hata gharama za matibabu, lakini bado hatupati mchango wowote kutoka kwa klabu yetu tuliyoitumiikia kwa moyo mmoja.

“Tunataka tupewe heshima inayostahili, zitengwe nafasi mbili kwa ajili wa wachezaji wa zamani, ili tutoe mchango wetu wa mawazo, nafasi hizi zinatakiwa kutolewa kwa wale ambao walicheza Yanga kwa maisha yao yote, hii itasadia kuhamasisha hata vijana wanakuja nyuma ,”alisema Manara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles