23.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Afcon nchini Misri itawakosa mastaa hawa

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO 

IJUMAA wiki hii kivumbi cha michuano ya Mataifa ya Afrika kinatarajia kuanza kutimua vumbi huko nchini Misri kwa mataifa 24 kuoneshana ubavu.

Katika Mataifa hayo, wachezaji mbalimbali wameitwa kwenye vikosi vyao kwa ajili ya kwenda kulipigania taifa lao. Kuitwa kwao kunatokana na kile walichokifanya kwenye klabu zao hasa kwa msimu uliomalizika.

Wapo wachezaji ambao walikuwa kwenye kiwango kizuri kwenye klabu zao huku wakiwa na ndoto za kuonekana kwenye michuano hiyo, lakini hawatokuwepo kutokana na matatizo mbalimbali.

SPOTIKIKI leo inakuanikia mastaa ambao walikuwa wanatarajiwa kuonekana kwenye michuano hiyo lakini itashindikana kutokana na kupata majeruhi.

Eric Bailly 

NI beki wa kati wa klabu ya Manchester United pamoja na timu ya taifa ya Ivory Coast. Alikuwa kwenye kikosi kilichotwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka 2015, lakini safari hii atakuwa nje ya kikosi kutokana na kuumia vibaya goti akiwa na klabu yake ya Man United.

Mchezaji huyo aliumia katika mchezo dhidi ya Chelsea kabla ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu ambapo mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa timu ya Ivory Coast umeamua kuwaita walinzi wengine kama vile Simon Deli, Cheick Comara na Ismael Traore kwa ajili ya kuziba nafasi hiyo.

Naby Keita 

Nyota huyo wa mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Liverpool, lakini mchezaji huyo raia wa nchini Guinea alipata majeruhi katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali dhidi ya Barcelona.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp aliweka wazi kuumia kwa mchezaji huyo kutamfanya awe nje ya uwanja kwa kipindi kirefu, lakini uongozi wa timu ya taifa ya Guinea umemuita mchezaji huyo kikosini.

Mbali na kuwa majeruhi, lakini madaktari wa Guinea wanapambana kuhakikisha mchezaji huyo anakuwa sawa na kucheza michuano hiyo, lakini inasemekana kuwa uwezekano ni mdogo.

Keagan Dolly 

Huyu ni mshambuliaji wa pembeni wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana pamoja na klabu ya Montpellier inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ufaransa.

Mchezaji huyo alipata tatizo la nyonga katika mchezo wa michuano ya COSAFA dhidi ya Botswana. Kutokana na hali hiyo kocha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini akaliondoa jina lake baada ya kupokea taarifa kutoka kwa madaktari wa timu ambao waliweka wazi kuwa, hawezi kuwa sawa katika kipindi hicho cha michuano hiyo

Musah Nuhu 

Huyu ni nyota wa timu ya taifa ya Ghana ambaye anacheza katika safu ya ulinzi, ameachwa kwenye kikosi cha timu hiyo baada ya kuumia wakati wa mazoezi ya kujiandaa na michuano hiyo.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa timu hiyo ya taifa ilitangaza kuachana na mchezaji huyo na kumrudisha kwenye klabu yake ya St. Gallen kwa ajili ya kwenda kufanya mazoezi mepesi.

Mchezaji huyo aliumia wakati kikosi hicho kipo United Arab Emirates. Wachezaji wengine ambao hawatokuwa na timu hiyo kutokana na majeruhi ni pamoja na Harrison Afful, Nicholas Opoku, Daniel Amartey na Jeffrey Schlupp.

Abdoul Cisse 

Huyu ni mlinda mlango wa timu ya taifa ya Ivory Coast. Wiki moja iliopita chama cha soka nchini humo kilitangaza kuachana na mlinda mlango huyo kwenye michuano ya Afcon.

Chama hicho kimeripoti kuwa, mchezaji huyo ameumia vibaya goti la kulia, hivyo anaweza kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Yves Bissouma 

KOCHA wa timu ya taifa ya Mali, Mohamed Magassouba, ameweka wazi kuwa, watamkosa kiungo wao Yves Bissouma kwenye michuano hiyo ya Afcon baada ya kuvunjika bega.

Nyota huyo ambaye anakipiga katika klabu ya Brighton ambayo inashiriki Ligi Kuu nchini England, mashabiki wa Mali walikuwa na imani ya timu yao kufanya vizuri kutokana na uwepo wake, lakini wataikosa huduma yake.

Ben Amor 

Huyu ni mmoja kati ya wachezaji ambao wadaiwa watakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na tatizo la goti. Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Tunisia na klabu ya Etoile du Sahel, aliumia akiwa na klabu hiyo katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali wa michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Zamalek.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, alianza kupata majeruhi mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi.

Achraf Hakimi 

Ni nyota wa timu ya taifa ya Morocco na klabu ya Borussia Dortmund, ambapo anaitumikia klabu hiyo kwa mkopo akitokea Real Madrid. 

Beki huyo alipata majeruhi katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Wolfsburg mapema Aprili mwaka huu. mchezaji huyo aliripotiwa kuvunjika mfupa wa vidole vya miguu.

Kocha wa Morocco, Herve Renard, alilitaja jina la mchezaji huyo katika kikosi cha awali huku akiamini anaweza kupona mapema jambo ambalo hadi sasa hawana uhakika na mchezaji huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles