22.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Kubenea, Mdee wasomewa maelezo mahakamani

mdee-kubeneaNa Patricia Kimelemeta -DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewasomea maelezo ya awali (PH) washtakiwa wanane wakiwamo, wabunge watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) katika kesi ya kumpiga na kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam(RAS),Theresia Mmbando.

Akisoma maelezo hayo mbele ya Hakimu, Huruma Shaidi, Wakili wa Jamhuri, Frola Massawe aliwataja washtakiwa hao kuwa ni pamoja na Halima Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga), Saed Kubenea (Ubungo), aliyekuwa Diwani wa Kata ya Saranga, Ephreim Kinyafu, Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema na mfanyabiashara Rafii Juma.

Wakili Massawe alidai mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo Februari 27, mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee, ulioko wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam ambako kulikuwa na uchaguzi wa meya na msadizi wake.

Alidai kuwa,katika ukumbi huo,kulitolewa taarifa ya kutokuwepo kwa uchaguzi huo kutokana na kuwepo kwa zuio kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo liliwataka kutofanya uchaguzi huo mpaka zuio hilo litakapomalizika ndipo uchaguzi ufanyike.

Alidai kuwa, mshtakiwa wa kwanza ambaye si mbunge (Rafii Juma), hakuridhishwa na taarifa hiyo  ndipo aliposhirikiana na washtakiwa wengine kwa kumvamia, kumpiga na kumchania nguo RAS Mmbando hali iliyosababishia majeraha.

Alidai, baada ya kutokea kwa vurugu hizo, polisi waliingilia kati na kumuuliza kama aliweza kuwafahamu waliompiga, baada ya kuulizwa hivyo, alidai kumfahamu mshtakiwa wa pili, ambaye ni Halima Mdee.

Alidai kuwa, baada ya hapo, polisi walilazimika kuchukua daftari la mahudhurio ya siku hiyo na kuanza kuita majina mmoja baada ya mwingine na kupiga gwaride la utambulisho ambalo lilimsaidia kuwatambua washtakiwa wote na kukamatwa na kuwafikisha polisi na mahakamani.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, washtakiwa hao walikubali taarifa zao binafsi lakini walikana shtaka linalowakabili.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulidai kuleta mashaidi 16 ambao watatoa ushaidi kwenye kesi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Shaidi alihairisha kesi hiyo hadi Novemba 14 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,415FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles