23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 10, 2022

Kocha Yanga apewa onyo kali

Theresia Gasper -Dar es salaam

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), imetoa onyo kwa Klabu ya Yanga, baada ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Luc Eymael kutoa matamshi yasiyofaa.

Onyo hilo limeenda sambamba na kuutaka uongozi ya Yanga kumuelimisha na kusimamia nidhamu kwa ujumla.

Kamati hiyo ilikutana Januari 20, ili kupitia matukio mbali mbali ya michezo ya Ligi Kuu.

Hatua hiyo imekuja kutokana na kitendo cha mwamuzi  Hans Mabena kugoma kumpa mkono kocha huyo, tukio lililotokea wakati wa mchezo kati ya Yanga na Azam uliochezwa Jumamosi iliyopita Uwanja wa Taifa,  Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Yanga ililala bao 1-0, huku beki wake Ally Sonso alilimwa kadi nyekundu.

“Katika kikao hicho moja ya maamuzi yaliyotolewa ni Klabu ya Yanga kupewa onyo baada ya kocha wake  kutoa matamshi yasiyofaa, pia wamepewa maelekezo ya kumuelimisha kocha wao na kusimamia nidhamu,” ilieleza taarifa hiyo.

Yanga pia imetozwa faini ya Sh. 500,000, adhabu hii pia imetolewa kwa Tanzania Prisons, kutokana na kutowakilisha majina ya vikosi vya timu zao kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo wao uliochezwa Desemba 29 mwaka jana, Uwanja wa Samora Iringa.

Yanga imepigwa faini nyingine ya Sh. 500,000 kutokana na mashabiki wake kurusha chupa za maji wakati wa mapumziko ya mchezo wao na Simba uliochezwa Januari 4 mwaka huu, Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Wanajangwani hao wametozwa faini nyingine ya Sh.200,000 kwa kutotumia chumba rasmi kilichoandaliwa kwa ajili ya kubadilishia nguo, adhabu hiyo ni kwa mujibu wa  Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.

Pia wachezaji watatu wa Yanga,  Mrisho Ngassa, Ramadhani Kabwili na Cleofas Sospeter,  kila mmoja amepigwa faini ya Sh.laki tano na kufungiwa mechi tatu kama ilivyo kwa wachezaji wa Mbeya City, Kelvin John na Majaliwa Shaban kwa kosa la kugoma kuingia vyumbani.

Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Klabu ya Coastal Union, Salum Perembo, amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)kwa kosa la kutaka kuingia uwanjani na kuwashambulia waamuzi huku akitoa maneno makali.

Tukio hilo lilijiri  Januari 11 mwaka huu, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Njombe Mji imepoteza mchezo dhidi ya Friends Rangers, baada ya kuwa na wachezaji pungufu ya saba, wakati wa mchezo uliofanyika Januari 19, Uwanja wa Karume, Dar es salaam.

Kutokana na hilo Friends imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.

Timu ya Mkamba Rangers, imepoteza mchezo dhidi ya Villa Squard, baada ya timu hiyo kufanya udanganyifu wa leseni kwa kubandika picha za wachezaji wengine katika leseni halali zilizotolewa na TFF.

 Mchezo huo uliyofanyika Desemba 10, mwaka jana.

Viongozi wa Mkamba Rangers,  Katibu Azizi Mfayeka, meneja wa timu, Kelvin John  na Kocha, Rashid Tuli  wamepelekwa Kamati ya Maadili ya (TFF) kwa kitendo cha udanganyifu wa leseni za wachezaji.

 Villa Squard imepewa pointi tatu na mabao matatu kwa mujibu wa Kanuni Namba 14(36)kuhusu taratibu za mchezo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,395FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles