KLOPP: COUTINHO HAENDI KOKOTE

0
512

LONDON, England


KOCHA wa timu ya Liverpool, Jurgen Klopp, amesema nyota wake, Philippe Coutinho, ni mchezaji muhimu katika timu hiyo na kila mtu anafahamu hivyo si rahisi kuondoka.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil ambaye Januari mwaka huu aliongeza  mkataba mpya wa miaka mitano na nusu kuendelea kubaki katika klabu hiyo, inaaminika amekuwa kwenye rada za Barcelona tangu miezi 12 iliyopita.

Coutinho alikuwa nyota wa mchezo Kombe la Premier League Asia walioshinda dhidi ya Leicester City, akifunga bao moja na kutengeneza lingine kwa Mohamed Salah kwa ushindi wa 2-1.

Kufuatia kiwango kikubwa cha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 katika mechi ya Hong Kong, Klopp amesisitiza kuwa Coutinho haendi kokote majira ya joto.

Klopp alinukuliwa na mtandao wa Mirror akisema: “Kila mmoja anafahamu kwamba, Phil Coutinho ni mchezaji muhimu kwetu. Najua kwamba anajisikia vizuri zaidi ya vizuri na huru kuwa Liverpool.

“Anaipenda klabu na mji wa Liverpool, pia jambo hili lipo dhahiri. Na kwa sababu ameweza kucheza namna ile usiku wa leo, kipindi kigumu cha maandalizi ya msimu baada ya majukumu yote, inavutia. Hiyo inaonyesha ni mchezaji muhimu.”

Klopp alipoulizwa jinsi gani mazungumzo yake na Coutinho yalikuwa, aliongeza: “Naam, tumeongea  lakini hayawahusu.”

Coutinho amefunga mara 13 na kutoa pasi 13 za mabao 2016-17 na kuisaidia Liverpool kumaliza nafasi ya nne Ligi Kuu Uingereza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here