25.2 C
Dar es Salaam
Monday, December 2, 2024

Contact us: [email protected]

Kifo cha Akwiline chaibuka kesi ya kina Mbowe

KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

SHAHIDI wa nane katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake nane, Mrakibu wa Polisi Benard Nyambali amedai kifo cha Akwilina Akwiline, kilisababishwa na kupigwa risasi, lakini hajui kati ya waandamaji 350 hadi 500 nani alikuwa na bunduki, isipokuwa anafahamu polisi watano walikuwa na silaha aina ya SMG.

Nyambali alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alipokuwa akihojiwa na Wakili Peter Kibatala.

Shahidi huyo alidai katika uchunguzi wake alibaini katika maandamano kulikuwa na kifo cha binti aitwaye Akwilina Akwiline.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Dk. Zainabu Mangu katika ushahidi wake, Nyambali alidai waandamanaji Februari 16 mwaka 2018 wakiwa maeneo ya Mkwajuni, walikuwa na fimbo, mawe na chupa za maji.

Alidai hakusema chochote kuhusu waandamanaji hao kati ya 350 hadi 500 kuwa na bunduki eneo la tukio, na hakueleza katika ushahidi wake kuwa washtakiwa aliowaona walikuwa na bunduki.

Washtakiwa aliodai kuwaona katika maandamano hayo maeneo ya Mkwajuni ni Mbowe, Halima Mdee, John Mnyika na Dk. Vicent Mashinji.

Shahidi huyo alidai hakukuwa na bunduki yoyote wala maganda ya risasi yaliyokutwa eneo la tukio kama kielelezo.

Alidai hakusema chochote katika ushahidi wake kuhusu kufanyika kwa ukaguzi wa silaha wanazomiliki kihalali waandamanaji hao kati ya 350 hadi 500.

Pia shahidi huyo alidai hakusema chochote kuhusu Mbowe, Mnyika, Mdee na Dk. Mashinji kama walikuwa na silaha siku ya tukio na kama silaha zao zilikaguliwa kubaini ipi ilitumika kumpiga Akwiline.

“Nafahamu kwamba Mbowe ana silaha aina ya Bereta, lakini sijui kama siku ya tukio alikuwa nayo ama la.

“Katika eneo la tukio polisi wanaofika watano walikuwa na silaha aina ya SMG,” alidai.

Alidai marehemu Akwiline alipigwa risasi ya kichwa akiwa ndani ya daladala akielekea katika safari zake.

Akihojiwa na Wakili Dk. Zainabu, alidai wakati wa uchunguzi kulikuwa na majalada mawili, na moja lilikuwa la mauaji na jingine la maandamano.

Shahidi huyo alidai hakushughulika na uchunguzi wa kifo cha Akwiline, kifo hicho kilifanyiwa uchunguzi na kundi lingine.

Alidai maandamano yalisabishwa na hotuba za viongozi katika Viwanja vya Buibui na kwamba yeye alikuta vurugu maeneo ya Mkwajuni hadi polisi waliwatimua waandamanaji kwa kurusha mabomu ya machozi.

Shahidi huyo alidai katika kufanya tathmini ya uchunguzi wake baada ya maandamano, katika tukio alikuta chupa za maji, mawe, fimbo na meza za wafanyabiashara zikiwa zimebinuliwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo wanadaiwa kufanya maandamano bila kibali, kushawishi wananchi kuichukia Serikali na uchochezi, matukio yanayodaiwa kufanyika Februari 16 mwaka 2018 wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Kinondoni.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

KESI YA MSINGI

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na 16, mwaka huu wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai, ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa Februari 16, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam Bulaya alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Ilidaiwa Februari 16, Barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni ,Wilaya ya Kinondoni kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Kwamba siku ya tukio la kwanza na la pili, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, kwenye mkutano wa hadhara mshtakiwa Heche anadaiwa alitoa lugha ya kuchochea chuki, alitamka matamshi kwamba “kesho patachimbika upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii, wizi unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano, watu wanapotea, watu wanauawa wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome, ” alinukuliwa na kudaiwa kuwa maneno yaliyoelekea kuleta chuki kati ya Serikali na Watanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles