32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Takukuru Kinondoni yaanza na matapeli wa viwanja

SAIDI IBADA (TUDARCo) – DAR ES SALAAM

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, imemfikisha mahakamani Katibu wa Kamati ya Urasimishaji, Nyakasangwe Malevu (33) kwa kosa la kuomba rushwa ya Sh milioni 2.5.

Malevu ambaye ni Mkazi wa Nyakasangwe, Kata ya Wazo, Dar es Salaam na Katibu wa Kamati ya Upimaji wa Viwanja Mtaa wa Nyakasangwe, anatuhumiwa kuomba rushwa hiyo na kupokea kiasi cha Sh 500,000 kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007.

Alidaiwa kuwa Agosti 14, alimtaka mtoa taarifa (jina limehifadhiwa) ampatie fedha hizo ili aweze kumpatia sehemu ya kiwanja ambacho kilikuwa cha mtoa taarifa kabla ya upimaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Theresia Mnjagira, alisema Malevu alidai sehemu ya kiwanja hicho iligaiwa kwa mtu mwingine baada ya upimaji kitendo ambacho ni kinyume na sheria.

Theresia alisema mlalamikaji alitoa taarifa ofisini kwao Agosti 16, mwaka huu ambapo uchunguzi ulifanyika na kubaini kuwa tuhuma hizo ni za kweli.

“Takukuru Mkoa wa Kinondoni iliandaa mtego wa rushwa na kumkamata mtuhumiwa Agosti 20 saa 10 jioni eneo la Mwenge Lukani Pub baada ya kupokea Sh 500,000,” alisema Theresia.

Katika tukio linguine, Takukuru Kinondoni imewafikisha mahakamani watuhumiwa wawili; Omary Abdallah (40) na George Joseph Barongo (37) kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa.

Theresia alidai Abdallah aliyekuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Magomeni na mkazi wa Kijitonyama alifikishwa mahakamani kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh 703,000.

Alidai Februari 12, 2017, Abdallah alimtaka mtoa taarifa (jina limehifadhiwa) ampatie Sh 1,000,000  ili aweze kumsaidia kwenye kesi ya mirathi iliyokuwa mbele yake kinyume na taratibu.

“Mlalamikaji alitoa taarifa Takukuru Mkoa wa Kinondoni Machi 10, 2017 ndipo uchunguzi ulifanyika na kubaini kuwa tuhuma hizo ni za kweli,” alidai Theresia. Pia alisema uchunguzi wa tuhuma zote mbili umekamilika na watuhumiwa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kujibu tuhuma zinazowakabili

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles