Waliokamatwa wakifanya biashara ya ngono, wateja wao wahukumiwa jela

0
854

RAMADHAN HASSAN – DODOMA        

MKAZI wa Nzuguni jijini Dodoma, Paschal George (28), amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kufanya ngono na kahaba.

Pia makahaba watano wamehukumiwa kifungo cha miezi mitatu na sita jela na kuchapwa viboko vitatu kwa kosa la kufanya ukahaba maeneo ya Jiji la Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema George walimkamata Septemba 8, mwaka huu usiku eneo la Uhindini, Kata ya Viwandani jijini hapa akifanya ngono na kahaba ambaye hakumtaja jina.

“Huyu tulimkamata usiku na amepatikana na hatia, na amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela,” alisema Kamanda Muroto.

Pia Kamanda Muroto alisema wanawake watano wamehukumiwa kifungo baada ya kufikishwa mahakamani na kukutwa na hatia ya kufanya vitendo vya ukahaba.

Alisema wanawake hao waliwakamata majira ya usiku katika Mtaa wa Uhindini, Kata ya Viwandani jijini hapa, kwa tuhuma za kufanya ukahaba ambao ni kosa chini ya kifungu namba 176 (a) (f) (g) cha kanuni ya adhabu sura ya 16.

 “Watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani ambapo walisomewa shtaka hilo na kupatikana na hatia na kuhukumiwa kama ifuatavyo; mwanamke mmoja alikiri kosa na kuhukumiwa kifungo jela cha miezi mitatu.

“Wanawake wanne walikana kosa, wametolewa ushahidi na kuhukumiwa kifungo jela bila ya kulipa faini, na mwanamke mmoja aliyekutwa akifanya ngono na mwanaume hawa wamehukumiwa kifungo cha miezi sita jela na viboko vitatu kila mmoja,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here